23.6 C
Dar es Salaam
Thursday, May 9, 2024

Contact us: [email protected]

WATOTO HAWAPASWI KULAZWA KWENYE MAKOCHI KWA MUDA MREFU

Na MWANDISHI WETU


WAZAZI wengi wana imani fulani katika suala la jinsi ya kuwalaza watoto wakati wamesinzia. Wazazi wanaowalaza watoto wao wakiwa wamelalia matumbo yao (kulala kifudifudi) wanadai kuwalaza watoto kwa migongo yao (chali) huwafanya wasipumue vizuri na wengine hudai huwafanya watoto wasitulie. Imani hizi zinachangiwa na kukosa elimu, utamaduni na mapokeo kutoka kwa wanafamilia.

Mtoto kulalia mgongo (kulala chali) wakati akiwa usingizini hupunguza hatari ya kifo cha ghafla (Sudden Infant Death Syndrome/SIDS) pamoja na kifo kinachotokana na kukosa pumzi wakati mtoto amelala vibaya na kuziba njia ya hewa. Nchini Marekani ni asilimia 43.7 tu ya kina mama wanaowalaza watoto wao chali wanapokuwa usingizini.

Madaktari bingwa wa watoto wanapendekeza wazazi kulala chumba kimoja na watoto wachanga ingawa wanaweza kulala vitanda tofauti. Kitanda anacholala mtoto mchanga kinapaswa kiwe na godoro lenye ubora mzuri (lisilobonyea kiurahisi au linalobonyea na kurudi haraka), kitandikwe vizuri kwa kunyooka kabisa yaani kisiwe na nguo kitandani kama shuka nzito (mablanketi) na mito ili kumlinda mtoto na kufunikwa na vitu hivyo kwenye njia ya hewa na kumkinga na joto lililopitiliza. Watoto hawapaswi kulazwa kwenye makochi na sofa kwa kusinzia muda mrefu.

Ili kuwasaidia wazazi kutambua ni usingizi kiasi gani unafaa kwa watoto wao, wataalamu  wa masuala ya usingizi walikutana na kutoa mapendekezo ya muda wa kulala kwa watoto yaliyoidhinishwa na kuungwa mkono na makundi mbalimbali ya kitaaluma wakiwamo madaktari bingwa wa watoto. Watoto wa miezi minne hadi 12 wanapaswa kulala hadi saa 16. Watoto wa mwaka mmoja hadi miaka miwili wanapaswa kulala kati ya saa 11 hadi 14. Watoto wa mika mitatu hadi miaka mitano wanapaswa kulala saa 10 hadi 13. Watoto wa miaka sita hadi miaka 12 wanapaswa kulala saa 9 hadi 12. Kwa upande wa vijana ni saa 8 hadi 10.

Matatizo ya kutolala vya kutosha kwa mtoto husababisha matatizo ya afya ya akili kwa mtoto na kushindwa kujifunza vizuri, kuwa na tabia ya ajabu na matatizo mengine ya kiafya kama kiribatumbo (obesity). Lakini pia, kulala kupita kiasi huongeza uwezekano wa magonjwa ya kisukari na akili na kuongezeka uzito kupita kiasi. Kuna sababu nyingi zinazosababisha watoto kukosa usingizi wa kutosha usiku, ikiwamo matumizi ya vifaa vya kieletroniki kama simu janja, video na kompyuta.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles