24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

NEC yapuliza kipenga uchaguzi 2020

Grace Shitundu, Dar es salaam

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imepuliza kipenga cha kuanza mchakato wa uchaguzi mkuu 2020 kwa kuzialika taasisi na asasi zenye nia ya kutoa elimu ya mpiga kura kupeleka maombi yao.

Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unatarajiwa kufanyika tena mwaka huku ikiwa ni ngwe ya pili ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Kwa mujibu tangazo lililotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi, Gerald Mwanilwa mwisho wa kupokea maombi ni  Januari 20, mwaka huu.

Kaimu Mkurugenzi huyo alisema NEC imezialika taasisi hizo kwa mujibu wa  kifungu cha 4C cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.

Alisema kifungu hicho kinaeleza kwamba Tume ina majukumu la kutoa elimu ya mpiga kura nchi nzima, kuratibu na kusimamia watu wanaotoa elimu hiyo.

“Kwa mantiki hiyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inapenda kuzialika Taasisi au Asasi zenye nia ya kutoa elimu ya mpiga kura kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kuwasilisha maombi yao Tume ya Taifa ya Uchaguzi” alieleza katika sehemu ya tangazo hilo.

Pamoja na kuziita taasisi na asasi zenye nia lakini kuna vigezo ambavyo taasisi hizo zinatakiwa kukidhi pindi zitakapowasilisha maombi.

Miongoni mwa vigezo hivyo ni pamoja na kuwa na usajili kwa mujibu wa Sheria za Tanzania.

“Iwe imefanya kazi Tanzania si chini ya miezi 6 toka kusajiliwa kwake, miongoni mwa watendaji wake wakuu watatu, wawili wanapaswa wawe Watanzania.

“Iwe haina taarifa za kuvuruga amani au kuchochea fujo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na katika nchi yoyote na iwe tayari kujigharamia katika kutoa Elimu ya Mpiga Kura”alisema Mwanilwa katika tangazo hilo.

 Aidha, maombi hayo yanatakiwa kuambatanishwa na cheti cha usajili, katiba ya taasisi au asasi, majina ya viongozi wa juu wa taasisi au asasi, anuani kamili ya makazi (Physical Address) na namba za simu za Ofisi na viongozi sambamba na ratiba na maeneo wanayotarajia kutoa Elimu ya Mpiga Kura.

Alisema Tume haitahusika na utolewaji wa fedha za kugharamia shughuli za kutoa elimu ya mpiga kura.

Aidha,  alisema tume itafuatilia taasisi au asasi zitakazopewa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura kwa lengo la kuona kama elimu hiyo inatolewa kwa kufuata taratibu zilizowekwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles