23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Mwili wa Mapalala kusafirishwa kijijini kwao

MWILI wa aliyekuwa mmoja wa waanzilishi wa Chama Cha Wananchi (CUF), James Mapalala unaotarajiwa kusafirishwa mwishoni mwa wiki tayati kwa maziko yatakayofanyika Jumatatu ijayo kijijini kwao Ussongwe mkoani Tabora.

Akizungumza na MTANZANIA nyumbani kwake Oysterbay Kinondoni, Dar es Salaam jana, mtoto wa marehemu Bernard James amesema \taratibu zinaendelea kufanyika nyumbani kwa marehemu ambapo siku ya Jumamosi asubuhi heshima za mwisho zitatolewa nyumbani hapo.

Alisema baadaye mwili utapelekwa Kanisa la St.Peter’s Oysterbay kwa misa na heshima za mwisho ambapo kutasomwa pia wasifu wake.

Alisema baba yao alianza kusumbuliwa na saratani ya kibofu cha mkojo ambapo alipata tiba hospitali mbalimbali.

“Tatizo kubwa lililokuwa linamsumbua ni saratani ya kibofu cha mkojo lakini miezi michache ya hivi karibuni alipata  fangasi za koo zilizosababisha kushindwa kula vizuri na hali yake ikaanza kudhoofu,”alisema Mapalala.

Alisema marehemu amezidiwa katika kipindi cha miezi mitatu na alikuwa akipatiwa matibabu  Hospitali ya Kairuki ambako alilazwa kwa muda wa wiki mbili na juzi saa 5 asubuhi alifariki dunia.

Alisema marehemu amezaliwa Februari mosi,1936, ameacha mjane, watoto, wajukuu na vitukuu.

Alianza masomo yake Ussongo mkoani Tabora, Shule ya Msingi Ussongo baadaye akajiunga na Ujiji Middle School, kisha akasoma Chuo cha Ualimu Murutunguru Nansio Ukerewe.

Baadaye alijiendeleza kujielimisha kupitia fursa mbalimbali.

Pia aliwahi kuwa mkandarasi wa majengo mbalimbali na kuwa Mwalimu wa Mbulu Middle School Kahama kwa miaka kadhaa.

Aliwahi kusoma Chuo cha Ufundi Murutunguru (TTC), Nansio Kisiwa cha Ukerewe.

Pia aliwahi kuwa Ofisa Ugavi wa Serikali na mnunuzi wa Mifugo ya Serikali ambayo ilikuwa ilitoka Kiomboi Singida ambayo ililetwa Tanganyika Packers kazi aliyoifanya kwa miaka kadhaa.

Alisema marehemu enzi hizo aliwahi kufanya shughuli za kilimo cha mpunga katika mashamba ya baba yake,baadaye kuacha na kujishughulisha na biashara.

Alisema baba yao alikuwa mmojawapo wa makandarasi wa kwanza wa kiafrika ambapo alijenga ofisi ya bima Singida, kituo cha afya Ihanja, Singida, ofisi ya Tanzania Rural Development Center, Singida, ofisi ya mapato Singida,kisha akatunukiwa kujenga Kijiji cha Michezo Uwanja wa Taifa, Temeke,Dar es Salaam kwa bahati mbaya fungu la fedha za Serikali hazikutosha kumalizia mradi huo, mradi ukasimama hadi leo hii.

Kisiasa

Marehemu Mapalala alikuwa na uelewa mkubwa  wa akili na ilifika wakati akaona kuna fursa endapo kutaanzishwa vyama vingi vya siasa na ndipo alipoandika barua ya ushawishi kwa rais wa wakati huo Hayati Mwalimu Julius Nyerere ili kuomba uwepo wa mfumo wa vyama vingi.

Alisema katika kipindi hicho marehemu hakuwahi kuwa mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),  alipoona fursa hiyo alifanya jitihada za kuanzishwa kwa vyama vingi na kufanikiwa baada ya miaka kadhaa.

“Nakumbuka wakati huo miaka ya 1980, baba baada ya kuandika barua hiyo akawa anaita vikundi vya watu mbalimbali na kuwahamasisha kuanzishwa vyama vingi…alipoenda kusambaza barua hizo mkoani Singida akakamatwa na polisi,”alisema Mapalala.

Alisema baadaye alikamatwa na kuwekwa kizuizini kwa muda wa mwaka mmoja mkoani Lindi,kisha akahamishiwa Kisiwa cha Mafia ambako alipangishiwa chumba na Serikali na kuzuiwa kutoka kisiwani humo.

Alisema alikaa huko kwa miaka miwili ndipo akaachiwa huru na kutokana na shinikizo la kampeni zake za kisiasa, utawala wa Rais Ally Hassan Mwinyi ukaruhusu mfumo wa vyama vingi nchini.

Alisema wakati huo, tayari Mapalala alikuwa ameanzishwa  Chama Huru cha Wananchi (CCW) na  Shaban Mloo na Seif Sharif Hamad wakanzisha Kamahuru.

Baadaye viongozi wakaungana pamoja na kuanzisha Chama Cha Wananchi (CUF), ambapo Mapalala alikuwa mwenyekiti.

Alisema wakati huo, Mapalala akiwa anaendelea na kampeni mkoani Tanga baadhi ya viongozi walifanya mkutano  Dar es Salaam na kumpindua mwenyekiti wao, kumteua Ibrahim Lipumba.

Aliongeza kuwa kuona hivyo miaka ya 1990 akaanzisha chama chake cha Haki na Usawa (Chausta), ambacho kilishamiri na baadaye kufifia ambapo Msajili wa Vyama vya Siasa aliamua kukifuta katika orodha ya vyama.

Marehemu Mapalala ni mtoto wa mwisho kati ya watoto sita wa marehemu Divina Sinzo na Bernad Mapalala ambaye alikuwa katekista aliyesaidia wazungu kueneza dini ya Katoliki pamoja na kuwatafutia maeneo.

Wazazi wake walifariki dunia akiwa na umri mdogo wa miaka minane na ndipo alipoanza kujitafutia elimu na maisha.

Alisema watamkumbuka baba yao kwa kutopendwa kuburuzwa na kuchukua uongo ambapo alikuwa akipenda mambo yote yawe yananyooka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles