MUUNGANO VYAMA VYA UPINZANI BURUNDI WAMEGUKA

0
523

 


BUJUMBURA, Burundi

Mwanasiasa mkongwe na mashuhuri wa upinzani nchini hapa, Agathon Rwasa, amejiengua katika muungano wa vyama vya upinzani, akiwa mbioni kusajili chama kipya cha siasa.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), katika mkutano na wafuasi wake wasiopungua 500 kutoka mikoani, wameshawakilisha mapendekezo mbalimbali kwa mujibu wa sheria ili wafikishe maombi yao kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani kwa usajili wa chama chao cha National Liberty Front Amizero y’Abarundi.

Katika taarifa hiyo ya BBC, Rwasa amesema itawalazimu wanasiasa wa upinzani kujidhatiti katika vyama vyao ili baadaye kujiweka pamoja wakati wa mpambano wa uchaguzi kwa mujibu wa katiba mpya.

Pia, amewataka wafuasi wake kuwa watulivu, wavumilivu na kuchangia kwa hali na mali kuanzia sasa hivi hadi itapofikia uchaguzi mkuu miaka miwili ijayo.

Kwasasa, Rwasa ni Makamu Spika wa Bunge akiwakilisha mseto wa vyama vya upinzani wa ‘Amizero y’abarundi’.

Muungano huo katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2015, ulishika nafasi ya pili ukitanguliwa na chama tawala CNDD FDD cha Rais Pierre Mkurunziza.

Rwasa amewahi kuishi uhamishoni katika nchi jirani ya Tanzania kwa takribani miaka 20 alipotoroka uongozi wa Watutsi wachache.

Mazungumzo ya Amani ya Arusha yaliwawezesha wanasiasa wa kabila kubwa la Wahutu kurejea nyumbani, lakini Rwasa alitoroka tena nchini mwaka 2010 wakati CNDD FDD ikiongoza kabla ya kurejea tena mwaka  2013.

Alijiunga na Bunge baada ya uchaguzi wa 2015 uliosusiwa na upinzani na inasemekana kwamba  iwapo chama chake kitasajiliwa, anasadikiwa kuwa mpinzani mkubwa kuliko wengine dhidi ya chama tawala CNDD FDD.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here