28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

TAKUKURU KUTOA DONGE NONO KWA ATAKAYETOA TAARIFA ZA HANS POPE

Bethsheba Wambura, Dar es Salaam



Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imewataka aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya utendaji ya Klabu ya Simba, Hans Pope na mkurugenzi wa kampuni ya Ranky Infrastructure & Engineering, Franklin Lauwo, wajisalimishe wenyewe katika ofisi zao kutokana na tuhuma za makosa mbalimbali ya rushwa yanayowakabili.

Akizungumza ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo, Naibu Mkurugenzi Mkuu TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungu, amesema juhudi mbalimbali za kuwatafuta watu hao zimegonga mwamba hivyo wanatakiwa watii amri na kujisalimisha wao wenyewe.

Naibu mkurugenzi huyo amesema Pope anatuhumiwa kwa kosa la kutoa taarifa za uongo kwa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), kuhusiana na malipo ya kodi.

Kati ya Machi 10,2016 na Septemba 30, 2016, mshitakiwa huyo akishirikana na washitakiwa wenzake, Evans Aveva na Geofrey Nyange walitoa maelezo ya uongo kwenye ofisi za TRA, kwamba klabu ya Simba imenunua nyasi bandia kutoka Ninah Guangzhou Trading Limited kwa thamani ya dola za kimarekani 40,577.

“Ukweli ni kuwa nyasi hizo zilinunuliwa dola za kimarekani 109,499 lengo ikiwa ni kukwepa kulipa kodi ya mapato sahihi kwa TRA,” Ameeleza.

Amesema kwa upande wa Lauwo anashtakiwa kwa kosa la kufanya biashara ya ukandarasi na aliupata kwa njia ya rushwa kwa sababu hakuwa na sifa na sio mkandarasi ambae amesajiliwa na bodi ya makandarasi nchini.

“Kati ya Machi na Septemba 2016, mshitakiwa alifanya kazi ya ukandarasi wa ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa klabu ya Simba uliopo Bunju, Kinondoni kwa thamani ya zaidi ya bilioni mbili wakati hajasajiliwa na bodi ya makandarasi, kisheria kufanya kazi hiyo,” amefafanua.

Aidha Brigedia Mbungu ameongeza kwamba mtu yeyote atakayesaidia kutoa taarifa za ukweli zitakazosaidia kupatikana kwa washitakiwa hao atapewa zawadi nono.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles