23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA AZINDUA UMEME WA GRIDI LINDI, MTWARA

Na MWANDISHI WETU-LINDI


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amefanya uzinduzi wa umeme wa gridi wa taifa kwa mikoa ya Lindi na Mtwara huku akiwataka wakurugenzi wa halmashauri nchini kuhakikisha wanafikisha umeme kwenye vituo vya kijamii, zikiwemo shule na hospitali.

Agizo hilo alilitoa jana wakati akizungumza na mamia ya wananchi na viongozi wa mikoa ya Lindi na Mtwara baada ya kuzindua kituo cha kuunganisha umeme wa gridi ya taifa katika Kijiji cha Mahumbika, Wilaya ya Lindi.

“Wakati tukizindua miradi kama hii, niwasihi wakurugenzi wa halmashauri wahakikishe kuwa umeme unapelekwa kwenye taasisi za kutolea huduma, zikiwemo shule zote za msingi na sekondari. Wakurugenzi tekelezeni hilo.

“Tunataka umeme huu upelekwe kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati. Na kama kuna visima vya maji katika maeneo yenu navyo pia vipelekewe umeme. Hatutaki kusikia wananchi wanakosa maji eti kwa sababu dizeli imekwisha,” alisema.

Alisema malengo ya Rais Dk. John Magufuli na Serikali yake ni kutaka Watanzania watumie umeme huo kukuza uchumi wao kupitia biashara za saluni, kuuza maji baridi au vinywaji baridi.

Pamoja na hilo, pia aliwataka wakazi wa mikoa hiyo washikamane kulinda miundombinu ya umeme ili iweze kuwa endelevu na isaidie vizazi vijavyo.

“Kuna baadhi ya watu wanajihusisha na biashara ya vyuma chakavu na wanang’oa vifaa ili wakauze bila kujali ni hasara gani wanasababisha. Ninawasihi wananchi wenzangu, kila Mtanzania awe mlinzi wa mwenzake kwenye miundombinu ya umeme.

“Ukiweza pita pale kwa wauzaji na uchungulie aina ya vifaa anavyouza kama ni vipya au ni chakavu kweli. Ukikuta kuna vifaa vyetu vya umeme vinauzwa huko, toa taarifa polisi naye atachukuliwa hatua kwa sababu sheria zipo,” alisema Majaliwa

Awali akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na hadhara hiyo, Waziri wa Nishati,  Dk. Medard Kalemani alisema miezi mitatu iliyopita hapakuwa na nyaya wala nguzo za umeme kutoka Lindi kwenda Mtwara lakini mafundi wa TANESCO wamejitahidi kuifanya kazi hiyo ndani ya muda mfupi.

“Lazima tuwapongeze vijana kwa sababu wamefanya kazi kubwa na nzuri na wala hatujatumia washauri waelekezi. Ndani ya miezi mitatu, wamejenga laini yenye urefu wa kilometa 80 kutoka Mtwara hadi Mahumbika.

“ Na kutoka hapa, watajenga laini yenye urefu wa km. 120 kwenda Ruangwa ambayo pia itaunganishwa kwenda Liwale na Nachingwea,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles