24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa aagiza wakuu wa wilaya kusaka watoto wasioenda shule na wazazi wao

Na Mwandishi wetu-Singida

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amewataka wakuu wa wilaya za Itigi na Ikungi na wakurugenzi wao wafanye msako kwenye stendi za mabasi ili kuwabaini watoto wasiokwenda shule.

Majaliwa alitoa agizo hilo kwa nyakati tofauti juzi wakati akihutubia wananchi waliojitokeza kumsikiliza kwenye mikutano ya hadhara aliyoifanya kwenye wilaya hizo.

Alisema Serikali ya awamu ya tano imeondoa michango kwenye sekta ya elimu na kwa maana hiyo watoto wenye umri wa kwenda shule wanapaswa wawe shuleni.

“Michango ya hovyohovyo haipo. Vinginevyo, fedha ambazo wazazi mmeokoa, peleka kwa mtoto. Mnunulie sare, kiatu kizuri, begi la shule na madaftari. Ale vizuri asubuhi na aende shule.

“Hatutarajii kuona vijana wadogo wanauza biashara kwenye vituo vya mabasi. Mkurugenzi chukua OCD siku moja nenda kwenye miji yenu midogo, saka watoto wote wanaofanya biashara stendi.

“Watambue wazazi wao, halafu kamata wajieleze ni kwa nini wanawaacha watoto wao waende kuhangaika stendi badala ya kwenda shule. Tunataka kila mtoto wa Kitanzania aende shule,” alisema Majaliwa.

Alisema Serikali imetoa maelekezo kwamba kila kijiji kiwe na shule ya msingi na kila shule lazima iwe na darasa la awali ili watoto wenye umri wa miaka minne hadi mitano waanze shule.

Katika hatua nyingine Majaliwa amekagua shamba la mfano la korosho lenye ukubwa ekari 12,000 lililopo kijiji cha Misigati, wilayani Manyoni na kusema ameridhishwa na uamuzi wa wilaya hiyo kuwa na zao mbadala la biashara.

 Akizungumza na wananchi na baadhi ya watumishi wa Halmashauri hiyo waliokuwepo eneo hilo, Majaliwa alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi kwa kulibeba wazo hilo na kuhakikisha linatimia.

 “Nimpongeze Mkuu wa Mkoa kwa kulibeba jambo hili, lakini nikuombe wewe na viongozi wenzako mhamasishe wengine walime zaidi zao hili kwa sababu korosho ni zao kubwa duniani na tena zao hili lina bei nzuri kimataifa,” alisema.

Alisema anatambua kwamba timu ya wataalamu kutoka kituo cha utafiti wa kilimo cha Naliendele, Mtwara imeshawasili Manyoni ili kufanya utafiti za zao hilo na jinsi linavyoweza kuzaa mara mbili kwa mwaka.

 “Kwa kawaida, mkorosho mmoja hutoa kilo 40 za korosho kwa msimu mmoja, kwa hiyo kwa misimu miwili mtapata kilo 80. Ninawasii limeni korosho kwa ajili ya watoto wenu ambao wako darasa la pili au la tatu. Mkulima ukianza kuvuna, utaendelea kuvuna kwa miaka 20 mfululizo na kwa hiyo hao watoto hawatahitaji kulipiwa ada wakiwa chuo kikuu sababu korosho itakuwa inawalipia,” alisema.

Pia aliwataka wakulima wanaolima zao hilo wilayani Manyoni, waunde ushirika wao ambao utawasaidia kuagiza dawa kwa pamoja ama kuuza kwa pamoja.

Hivyo, amemwagiza Afisa Ushirika wa Wilaya hiyo, Bi. Yusta Philipo ahakikishe anasimamia jambo hilo kuanzia sasa.

 Mapema, akitoa taarifa juu ya mradi huo, Meneja wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Kanda ya Kati, Ray Mtangi alimweleza Waziri Mkuu kwamba mradi wa kilimo cha korosho unajumuisha mashamba makubwa mawili ambapo shamba la Misigati lina ukubwa wa ekari 7,000 na lile la Mikwese lina ekari 5,000.

 Alisema watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa kitaifa wamekuwa wakifika shambani hapo ili wajifunze mbinu mpya za kuzalisha korosho kwenye maeneo yao.  Pia alisema Halmashuri yao imetenga eneo la ujenzi wa viwanda na kwamba hadi sasa wanazo ekari 50 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kubangua korosho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles