24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

MAHAKAMA YATISHIA KUFUTA UCHAGUZI WA MARUDIO KENYA

NAIROBI, KENYA

MAHAKAMA ya juu nchini Kenya jana iliionya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) irekebishe kasoro zilizochangia kuufuta uchaguzi wa urais wa Agosti 8, vinginevyo haitasita kufuta uchaguzi ujao wa marudio.

Wakati Septemba Mosi, Jaji Mkuu David Maraga  alipotangaza kufuta ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta akieleza kwa ufupi sababu za kufanya hivyo, jana alisoma hukumu kamili juu ya sababu zilizowafanya majaji wanne kufuta matokeo hayo.

”Hukumu hii inapaswa kuwa fundisho kwa IEBC kujitazama na kurekebisha makosa na iwapo kasoro zitajirudia, hukumu kama hii itatolewa tena bila kusita,” alisema.

Katika maelezo yao Maraga, naibu wake Philomena Mwilu na Jaji Isaac Lenaola, walieleza kubaini kiwango cha kasoro na ukosefu wa uhalali wa matokeo kuwa mkubwa na wa makusudi.

Walisema walifuta uchaguzi wa urais baada ya Tume kushindwa kujibu hoja zinazotokana na ushahidi uliowasilishwa na muungano wa upinzani wa NASA uliofungua kesi hiyo.

“Ni wazi kasoro zote hizi na nyingi zilitosha kuathiri uhalali wa uchaguzi wa urais,” Jaji Maraga alisema.

Pamoja na kwamba matokeo ya urais yalikuwa yakioneshwa katika televisheni, majaji walisema IEBC ilishindwa kuufahamisha umma yanakotoka matokeo hayo na kusisitiza matokeo ya uchaguzi si kuhusu namba.

“Kwa upande wetu, uchaguzi si kuhusu namba; matukio, bali mchakato halali wa kidemokrasia,” majaji walisisitiza.

Walimtuhumu Mwenyekiti wa Tume, Wafula Chebukati kwa kutangaza matokeo ya mwisho bila uwapo wa fomu namba 34A kitendo ambacho ni ukiukaji wa Sheria ya Uchaguzi.

Tume iliendesha uchaguzi wa urais usio halali, usiothibitishwa na wenye uwazi kidogo, majaji walisema.

“Kati ya ‘Fomu 34 Bs’  290 zilizotumika kutangazia matokeo ya urais, 56 kati yao hazikuwa na alama za usalama. Alama za usalama zilipotelea wapi?” alihoji Jaji Maraga.

Majaji waliona kuwa kushindwa kwa tume kuwa wazi kukaguliwa kwa mtambo wa kusambaza matokeo licha ya kutumia mabilioni ya dola za walipa kodi kulikuwa uthibitisho kuwa Tume ilificha kitu.

“Agizo letu la kuitaka iwaachie wapinzani kukagua mtambo lilikuwa fursa nzuri kwa IEBC kuishinda hoja ya mlalamikaji, lakini waligoma hata kutii agizo la mahakamar” alisema Jaji Mwilu.

Aidha alisema mawakili wa utetezi wa IEBC waliupotosha mhimili wa mahakama na kuwaacha majaji bila chaguo jingine zaidi ya kukubiliana na mlalamikaji kuwa uchaguzi ulichakachuliwa.

Aidha Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati anapaswa kuwajibika kwa kushindwa kueleza kwanini matokeo ya urais hayakusambazwa kwa namna inavyotakiwa kikatiba.

Mahakama inasema IEBC ina wajibu wa kuhakikisha mfumo wa kupiga kura, kuhesabu na kujumuisha matokeo unakaguliwa na u sawa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles