23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

LISSU: MUNGU ALISEMA SITAKUFA

Mwandishi Wetu


KWA mara ya kwanza tangu ajeruhiwe kwa risasi Septemba 7, mwaka huu, sauti ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), imesikika.

Lissu ambaye amelazwa katika Hospitali ya Nairobi alitumia dakika tatu kutoa shukrani zake kwa Mungu kwa kusikia maombi ya waja wake na hivyo kutimiza siku 42 hadi sasa akiwa hai.

Pia Lissu aliwashukuru watu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ambao wamejitoa kwa hali na mali katika kumsaidia wakiwamo madaktari na wauguzi.

Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika  (TLS), alisema kama si mkono wa Mungu uhai wake ulikuwa umekatishwa nyumbani kwake mjini Dodoma.

“Watanzania wenzangu mimi ni Tundu Lissu, nazungumza kutoka kitanda cha Hospitali ya Nairobi. Kwanza kabisa naomba nitoe shukrani zangu kwa Mungu wetu kwa mapenzi, Mungu  wetu wa maisha, Mungu wetu wa uponyaji kwa kuniweka hai mpaka hapa nilipo.

“Kama isingekuwa Mwenyezimungu, maisha yangu yangeishia nyumbani kwangu Dodoma siku ile.

“Lakini Mwenyezimungu huyu wa uponyaji, Mwenyezimungu alisema huyu hatakufa, naomba nishukuru kwa hilo kwanza.

“Pili Watanzania kwa mamilioni yao kila mahali walipo, walioko Tanzania, walioko nchi za nje, walioko mataifa mbalimbali duniani nao vilevile walipaza sauti makanisani, kwenye mikutano ya hadhara, misikitini, na kumwomba Mungu maisha yangu yapone.

“Nafikiri sitakosea nikisema kwamba niko hai kwa sababu ya maombi ya mamilioni ya Watanzania hawa vilevile.

“Tatu tangu nimeletwa Kenya watu wengi sana siwezi kuwataja wote, wamekuja kuniona na kunipa pole hospitalini, wananchi wa kawaida kabisa wa Tanzania , kuna mama amesafiri kutoka Iringa simkumbuki hata jina, amekuja akaniambia mhesimiwa nataka nikufanyie tu maombi.

“Watanzania wote wa aina hii kwa upendo wake mkubwa. Tumesaidiwa sana na wote hawa ambao nimewataja na wale wengine ambao sijawataja.

“Vyama vya kitaaluma karibu vyote duniani, ambavyo vina ushirika na Chama cha Mawakili cha Tanganyika  (TLS) ambacho mimi ni rais wake pamoja na TLS yenyewe wamejitolea kwa upendo mkubwa sana, kwa ukarimu mkubwa sana,  kuhakikisha kwamba ninapata tiba au ninasafirishwa na mambo ambayo yanahitaji kufanyika yanafanyika.

“Nimepata message (ujumbe mfupi) za kuungwa mkono kutoka mataifa ya Marekani, Uingereza, Australia, Newzeland, Ubeligiji, Ujerumani, Kenya yenyewe, pamoja na nchi nyingine.

“Lakini kuna kundi ambalo sijalisema ambalo linahitaji kutajwa kipekee kabisa, madaktari, wauguzi, wafanyakazi wa kawaida wa hospitrali ya Nairobi, Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, pamoja na wafanyakazi wa tiba kutoka taasisi zingine ambao kwa njia mbalimbali walishiriki katika kuniponya, wote hawa nawapa pongezezi zangu za dhati kabisa,” alisema.

MUDA MFUPI BAADA YA PICHA KUANZA KUSAMBAZWA

Jana jioni muda mfupi baada ya Chadema kuanza kusambaza picha hizo za Lissu, mitando ya kijamii ilizizima kwa watu mbalimbali kueleza walivyoguswa kumwona hadharani mwanasheria huyo.

Picha hizo zilianza kusambazwa jana saa 10 jioni ambapo zilimwonyesha Lissu akitabasamu na kupungia mkono akiwa hospitalini Nairobi, Kenya.

Nyingine zilimwonyesha akiwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, Aisha Luja, huku nyingine zikimwonyesha akiwa na kaka yake.

Baada ya picha hizo kuanza kusambazwa kwenye mitandao, watu mbalimbali walianza kutoa maoni yao huku idadi kubwa wakiendelea kumwombea apone haraka.

Maoni mbalimbali yaliyoandikwa kwenye mitandao ya kijamii yalisomeka hivi; “Mungu tabibu wa matabibu hakika atamponya kondoo wake, amina,” aliandika Joseph Kapyela.

Tupilike Mwakangale aliandika; “Ahsante Mungu kwa kumtendea mema, waliotenda dhambi hii watalaaniwa wao na vizazi vyao”.

Naye Jonas Masambai aliandika; “Mungu ni mwema na ni mwaminifu ndio maana amemwepusha na kifo mzalendo wa kweli wa Tanzania. Ni Mungu pekee aliye na ukuu na nguvu zaidi ya yeyote ndiye aliyeamua Lissu awe hai mpaka sasa,” aliandika.

Maoni mengine ni ya Pendo Gamasa aliyeandika; “Mungu akupe nguvu zaidi na awalinde wale waliofanya ukatili huo ili washuhudie ukuu wako na wajifunze kuwa kama Mungu hajaamua basi binadamu hana nafasi.

Remmy Mwinuka aliandika; “Haijawai tokea mwenye haki akaachwa na Mungu. Imeandikwa sitakufa bali nitaishi ili niyasimulie matendo ya Mungu.

Elias Mohamed aliandika; “Kama ni watu wasiojulikana basi huenda hatuwajui sisi tu, lakini Mungu anawajua na wasipotubu muda si mrefu nao watadhalilika na kufedheheka,” aliandika.

MTATIRO

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro alisema; “Risasi zaidi ya 38 za shambulizi, risasi zaidi ya 10 mwilini, kupoteza asilimia 97 ya damu, oparesheni 17 mwilini na bado yuko imara na mwenye furaha. Watesi wake wanateseka mara 100.

“The True Legend Mungu wako ni mkuu ni wa kuogopwa na kusujudiwa daima, tabasamu lako ni mabomu ya nyuklia kwa wabaya wako.

Mwisho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles