25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

LISSU AFICHUA SIRI KUWATEGA POLISI

Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu, akizungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, baada ya kugoma kutoka katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma kwa hofu ya kutaka kukamatwa jana. Picha na Ramadhan Hassan

NA WAANDISHI WETU – DAR/MIKOANI

MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), amejikuta aking’ang’ania ndani ya Mahakama ya Wilaya ya Dodoma akikwepa kukamatwa na polisi.

Hatua hiyo iliwafanya askari waliokuwa wamepiga kambi nje ya mahakama hiyo, kujikuta wakikwama kumtia nguvuni mbunge huyo ambaye anadaiwa kutoa matamko yenye utata dhidi ya Serikali na Rais Dk. John Magufuli.

Hata hivyo hatua hiyo inaelezwa kuwa huenda ilikuwa na ujumbe dhidi ya Serikali, huku ikiibuka hofu mhimili huo unaosimamia haki kuwekwa kwenye mtego kwa mwanasheria huyo kukamatwa bila agizo la mahakama.

Alipoulizwa Lissu sababu za kung’ang’ania mahakamani, alisema kuwa hakuna maana yoyote kisheria, bali ameamua kufanya hivyo kwa sababu ndiyo sehemu salama kwa nchi zinazoheshimu utawala wa sheria duniani kokote.

“Nimeamua kung’ang’ania mle ndani kwa kuwa ni salama zaidi… mbali na mahakama, kwingine ambako ningeweza kwenda ambapo ni salama ni msikitini au kanisani, kwenye nchi zinazoheshimu demokrasia na utawala bora hawawezi kukukamata,’’ alisema Lissu.

Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alisema dunia nzima kama utakuwa umekimbilia mahakamani ni sehemu salama, huwezi kukamatwa na askari.

Alisema aliingia mahakamani hapo saa 2 asubuhi kuwatetea wateja wake ambao ni walimu walioamua kukishtaki Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Wilaya ya Dodoma na kulazimika kukaa humo kwa saa saba.

Alisema baada ya kumalizika kwa kesi hiyo saa 8:23 mchana, alilazimika kubaki ndani ya mahakama kutokana na taarifa aliyodai  kupewa ya kukamatwa na askari waliokuwa nje.

Lissu alisema kuwa alilazimika muda wote kuwa na mazungumzo na viongozi wa Chadema waliofika mahakamani hapo baada ya kupata taarifa za kukamatwa kwake.

Hali hiyo ilizua taharuki na kumfanya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa kufika mahakamani hapo saa 10:04 jioni akiwa na mlinzi wake na kumtaka Lissu aondoke ndani ya mahakama hiyo kwani hakuna atakayemkamata.

Mazungumzo kati ya Lissu na Kamanda Mambosasa yalikuwa kama ifuatavyo:

Lissu: Kamanda nipo Dodoma hapa tangu juzi, nipo mahakamani naendesha kesi, naambiwa kuwa polisi wananisubiria nje wanikamate, nikasema kama ndiyo hivyo  siku ile nilikamatiwa getini bungeni na siku nyingine nilikamatiwa nyumbani, nikasema ‘this time’ nipo kazini.

Kamanda: Niliwatuma mimi?

Lissu: Uliwatuma wewe?

Kamanda: Wale waliokukamata niliwatuma mimi? Mimi sina ‘issue’ na wewe wala Afande Inspekta Jenerali (IGP) hana ‘issue’ na wewe, likitokea jingine tutakwambia, leo hakuna.

Lissu: Asante

Kamanda: Sasa kwa nini unajiweka ndani?

Lissu: Nimekwambia sababu zilizonifanya  niwe hapa.

Kamanda: Nimekwambia wamekuchanganya na ngoja nikutoe wasiwasi, mimi kama ningekuwa nakutafuta, nakukamatia hapa hapa mahakamani, kwani hili ni jengo la mahakama.

Lissu: Eeeh.

Kamanda: Yaani hapa sio kwamba huwezi kukamatwa.

Lissu: Nilisema hivi, mara hii nitakamatiwa mahakamani, ndivyo nilivyosema labda kwa vile umesema niko salama basi.

Kamanda: Walionipigia ni kina nani? Kuna watu walinipia ni waandishi, nilichowaambia nipo mbali labda kama mmeenda kuwinda, hivyo kuna askari wa wanyama pori wanawatafuta.

Lissu: Nimekusikia.

Kamanda: Tafuteni mambo mengine, hili halipo, habari ndiyo hiyo.

Lissu: ‘Ok I’m free’.

Baada ya mazungumzo hayo kati yake na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lissu aliondoka katika eneo hilo la mahakama saa 10:12 jioni.

Awali akizungumza na waandishi wa habari ndani ya mahakama hiyo, Lissu alisema amechoka kuona nchi namna inavyoendeshwa.

Alisema jana asubuhi alipokea taarifa kutoka kwa mke wake kuwa polisi walifika nyumbani kwake Dar es Salaam, wakiwa wanamtafuta.

“Wakaambiwa sipo nyumbani kwa sababu tangu juzi nipo Dodoma kwa sababu ya hii kesi iliyoanza kusikilizwa jana (juzi) walivyoambiwa sipo wakaondoka. Wakati kesi hii inaendelea, nikaletewa ujumbe unaosema kwamba askari waliovalia kiraia wa hapa Dodoma wametumwa kuja kunikamata baada ya kesi hii kumalizika,’’ alisema.

Alisema pamoja na hali hiyo, yeye ni wakili ila kwa nchi inayoendeshwa kwa misingi ya utawala wa sheria, mawakili huwa hawakamatwi mahakamani wakati wakifanya kazi zao.

Rais huyo wa TLS alisema haitakuwa mara yake ya kwanza kukamatwa na kwamba kwa mwaka huu itakuwa mara yake ya nne, huku akidai tangu Juni mwaka jana itakuwa mara yake ya saba au ya nane kutiwa mbaroni.

Lissu alisema katika siku za nyuma viongozi wa ngazi za juu wa polisi walikuwa wakitumia njia za kiungwana za kumwambia anahitajika polisi, lakini kwa sasa imekuwa hali tofauti.

“Mfano mwaka jana kabla sijafunguliwa kesi ya uchochezi, ile inayohusu gazeti la Mawio ambayo washtakiwa tupo wanne, washtakiwa wenzangu watatu, waandishi wa habari wale walisomewa mashtaka yao mwezi wa nne.

“Na RCO wa Kanda Maalumu ya Dar es Saalam, Camilius Wambura, alinipigia simu na akaniuliza nipo wapi, nikamwambia nipo bungeni, akaniuliza ‘ratiba yako ikoje’ nikamwambia nikitoka bungeni nitaenda Masasi katika kesi ya uchaguzi ya mbunge wetu Cecil Mwambe kisha nitaenda Kilombero kwa Lijualikali.

“Kamanda Wambura aliniambia kwamba watasubiri nikamilishe hayo majukumu na kweli nilipomaliza tarehe 26 Juni, Jumatatu iliyofuata ya tarehe 28, nilienda polisi na kesho yake nikapelekwa mahakamani kuungwaniswa na wale watuhumiwa watatu,’’ alisema.

Mwanasheri huyo mkuu wa Chadema, alisema hawezi kukimbia Tanzania kwani ndipo watu walipomchagua kuwa mbunge.

“Na Mkubwa Rais Magufuli aliishasema ukifukuzwa bungeni anatusubiria nje, kwa hiyo hayo ni maelekezo ya Serikali yake kuhakikisha wapinzani wanakamatwa, wanadhalilika na mikutano inazuiliwa,’’ alisema.

Pamoja na hali hiyo, alisema kwa sasa ahofii jambo lolote kwani unapokuwa katika mapambano ya kidemokrasi, kunyanyaswa na kudhalilishwa na vyombo vya dola ni jambo la kawaida, hasa katika mazingira ya sasa ya nchi.

“Kila Mtanzania mwenye nia njema na mwenye akili timamu apaze sauti kupinga huu ujinga unaofanywa,’’ alisema.

 MAJALIWA ATOA ONYO

Wakati hayo yakiendelea, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema Serikali itawashughulikia watu wote wanaotoa matamshi ya kichochezi bila ya kujali nyadhifa zao.

Amesema ni vema watu wakawa makini na kujiepusha kutoa matamshi ambayo yataathiri mfumo wa maisha kwa wananchi wengine.

Hayo aliyasema jana wakati wa ibada ya mazishi ya Linah Mwakyembe, mke wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, iliyofanyika Kyela mkoani Mbeya.

“Tutashughulika na watu wote wanaotoa matamshi ya kichochezi, popote walipo bila ya kujali uwezo wao, vyeo vyao na mamlaka walizonazo,” alisema.

Aliwaomba viongozi wa dini waendelee kuliombea taifa na viongozi wake na kwamba Serikali inawategemea na iko pamoja nao.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo baada ya Askofu wa Kanisa la Evarinjerical Brother Hood, Rabison Mwakanani kuonya vitendo vya baadhi ya watu kumtukana Rais Dk. John Magufuli.

Alisema ni vema watu hao wakajifunza namna ya kuwasilisha hoja zao bila ya kutumia lugha za matusi.

“Rais Dk. Magufuli amefanya mambo mengi makubwa kwa ajili ya maendeleo. Wanaofanya hivyo wasidhani kama wanamtukana Rais tu, bali wanawatukana Watanzania wote waliomchagua wakiwemo viongozi wa dini,” alisema Askofu Mwakanani.

MASHINJI, WENZAKE WASOMEWA MASHTAKA MAWILI

Wakati huo huo, viongozi tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akiwamo Katibu Mkuu, Dk. Vicent Mashinji, jana wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Ruvuma kujibu mashtaka mawili yanayowakabili.

Viongozi hao, wamesomewa mashtaka yanayowakabili na Wakili wa Serikali Mwandamizi Mkoa wa Ruvuma, Renatus Mkude ambaye alikuwa akisaidiwa na Shaban Mwigole, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Ruvuma, Simon Kobelo.

Wakili Mkude, aliwataja washtakiwa wengine kuwa ni Cecil Mwambe (Mwenyekiti wa Kanda ya Kusini ambaye pia ni Mbunge wa Ndanda mkoani Mtwara), Philberth Ngatunga (Katibu wa Kanda ya Kusini), Irineus Ngwatura (Mwenyekiti Mkoa wa Ruvuma) na Delphin Gazia (Katibu Mkoa wa Ruvuma).

Wengine ni Zubeda Sakuru (Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Ruvuma), Sanguru Manawa, (Katibu wa Oganaizesheni na Mafunzo), Curthberth Ngwata (Mwenyekiti Wilaya ya Nyasa) na Charles Makunguru (Katibu Mwenezi Wilaya ya Nyasa).

Mkude alidai kuwa washtakiwa wote kwa pamoja wanashtakiwa kwa makosa mawili.

Kosa la kwanza wote kwa pamoja, wakiwa wilayani Nyasa tarehe isiyofahamika walikula njama ya kutenda kosa ambalo lingeweza kusababisha uvunjifu wa amani ndani ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Alisema kosa la pili, inadaiwa Julai 15, mwaka huu katika mji wa Mbambabay,  washtakiwa wote kwa pamoja walifanya mkusanyiko usio halali, ambao ungesababisha uvunjifu wa amani kwa jamii.

Aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo unaendelea na aliiomba ipange tarehe nyingine ya kutajwa. Washtakiwa wamekana mashtaka yote.

Kwa upande wake, Hakimu Kobelo alisema dhamana ya washtakiwa iko wazi hivyo kila mmoja anapaswa kuwa na wadhamini ambao ni wakazi wa Songea mjini wanaotakiwa wapeleke uthibitisho kutoka kwa maofisa watendaji wa mitaa wanayoishi.

Pia washtakiwa hao, wametakiwa kudhaminiwa kwa Sh milioni 2. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 20, mwaka huu  itakapotajwa tena.

Wakati taratibu za kukamilisha dhamana zao zikiendelea, washtakiwa walirudishwa mahabusu kwa taratibu za kiusalama kutokana na kile kilichodaiwa kuwapo mkusanyiko wa watu hadi taratibu zitakapokamilika ambazo zinafanyiwa kazi na mawakili wa upande wa washtakiwa, Edison Mbogoro, Dickison Ndunguru na Banabasi Pomboma.

Hata hivyo, viongozi hao jana wamelala gerezani kutokana na kushindwa kukamilisha dhamana.

Akizungumzia hali hiyo, Wakili Mbogoro alisema Mashinji na wenzake wamefunguliwa kesi ya Jinai namba 173 ya 2017 na upande wa Jamhuri haukuwa na pingamizi juu ya dhamana.

“Ilikuwa ni barua ya wadhamini wawili wawili ambao walikamilisha nyaraka zao, lakini mahakama iliomba kuzipitia ili kupata uhakiki wa nyaraka hizo.

“Hadi sasa tulikuwa tumekaa tunasubiri nyaraka za wadhamini ziweze kuthibitishwa, lakini hadi sasa saa tisa sidhani kama litatekelezwa kwa leo kwa kuwa muda umeenda ni hadi hapo kesho,’’ alieleza Mbogoro.

Naye wakili Pomboma alisema wameshangazwa na kilichotokea. Walimtafuta wakili wa Serikali na hakimu wakawa wanaondoka kwa kupishana katika eneo la mahakama.

Alisema mazingira hayo ya kutokuwapo kwa watendaji ambao wamepewa dhamana, bado hayajawa ‘comfortable’ kwao na hawajui ni mazingira gani yamewafanya wasiwepo kiasi cha kwamba wateja wao wameshindwa kupata haki yao.

Habari hii imeandaliwa na RAMADHAN HASSAN (DODOMA), ASHA BANI (DAR ES SALAAM) na NA AMON MTEGA (SONGEA)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles