JPM APIGILIA MSUMARI VITUO VYA MAFUTA

0
1211
Rais Dk. John Magufuli, akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Shule ya Seminari Katoke iliyopo Biharamulo mkoani Kagera jana wakati wa ziara ya siku mbili aliyofanya mkoani humo, ambapo alizindua Barabara ya Biharamulo, Kagoma na Lusaunga yenye urefu wa kilomita 154. Kulia ni Mkewe, Janeth Magufuli. Picha na Ikulu
Rais Dk. John Magufuli, akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Shule ya Seminari Katoke iliyopo Biharamulo mkoani Kagera jana wakati wa ziara ya siku mbili aliyofanya mkoani humo, ambapo alizindua Barabara ya Biharamulo, Kagoma na Lusaunga yenye urefu wa kilomita 154. Kulia ni Mkewe, Janeth Magufuli. Picha na Ikulu

Na MWANDISHI WETU, BIHARAMULO

RAIS Dk. John Magufuli ametoa siku 14 kwa wamiliki wa vituo vyote vya mafuta nchini wawe wameanza kutumia mashine za kielektroniki za kutolea risiti.

Alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na wananchi wa Biharamulo mkoani Kagera muda mfupi kabla ya kufungua barabara ya lami ya Kagoma – Biharamulo – Lusahunga.

Kauli hiyo ya Dk. Magufuli imekuja siku chache baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuvifungia kuuza mafuta vituo vyote ambavyo havitumii mashine za kielekroniki za kutolea risiti (EFDs) na kusababisha uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo katika mikoa mbalimbali nchini.

Katika agizo lake, Dk. Magufuli amewataka Waziri wa Fedha na Mipango, Philip Mpango na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kuhakikisha vituo vyote vya mafuta nchini vinatumia mashine hizo na kusisitiza kuwa wamiliki watakaokiuka agizo hilo, vituo vyao vifungwe na kufutiwa leseni.

Taarifa ya Ikulu iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa ilisema: “Na kwa hili natoa siku 14, wale wenye vituo vya mafuta wote,  uwe upo  Chato, uwe Biharamulo, uwe Kagera, uwe Dar es Salaam, hakikisha una hiyo mashine, ndani ya siku 14.”

Aidha Dk. Magufuli amewataka wafugaji waliovamia Hifadhi ya Taifa ya Burigi mkoani Kagera kuondoa mifugo yao mara moja na amemwagiza Mkuu wa Mkoa huo, Meja Jenerali mstaafu Salum Kijuu kuendelea na operesheni ya kuondoa mifugo yote iliyovamia hifadhi hiyo na maeneo mengine yasiyoruhusiwa kulishia mifugo.

Katika hatua hiyo, Dk. Magufuli aliwataka wafugaji kote nchini kuchunga mifugo yao katika maeneo waliyotengewa, huku akionya kuwa vitendo vya wafugaji kuingiza mifugo yao katika hifadhi na mashamba ya wakulima havikubaliki.

“Mkuu wa mkoa na wakuu wa wilaya simamieni hilo, ninajua bado kuna ng’ombe mle hifadhini, simamieni kwa kuzingatia sheria za hifadhi.

“Kwa hiyo wafugaji wajifunze namna ya kufuga, kama unaona una ng’ombe wengi na huwezi kuwatunza uza, hata mimi nimeuza ng’ombe wangu, niliona wamekuwa wengi siwezi kuwatunza, viwanda vipo,” alisisitiza.

Kuhusu kero ya uhaba wa maji inayowakabili wananchi wa Biharamulo, Dk. Magufuli alielezea kusikitishwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa mradi wa kupeleka maji katika mji huo na alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Bukoba (BUWASA), Alen Mwita kuhakikisha mashine zilizonunuliwa zinafungwa na kuanza kutoa maji ifikapo Julai 30.

Baada ya kuzungumza na wananchi wa Biharamulo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kituo cha mabasi, Dk. Magufuli alifungua barabara ya Kagoma – Biharamulo – Lusahunga ambayo inaunganisha barabara ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Kigoma, Shinyanga na nchi jirani za Burundi, Rwanda na Uganda.

Barabara hiyo ina urefu wa kilometa 154 na imejengwa kwa gharama ya Sh bilioni 190.4 zilizotolewa na Serikali ya Tanzania.

Mapema jana asubuhi, Dk. Magufuli alitembelea Seminari ya Mtakatifu Karoli Lwanga Katoke, alikosoma elimu ya sekondari, ambako aliendesha harambee iliyofanikisha kupatikana mifuko 1,000 ya saruji na mabati 150 kuchangia ujenzi wa Seminari hiyo.

Aidha Dk. Magufuli pia alitoa Sh milioni 1 za kutengeneza dirisha la bweni alilolivunja wakati akiwa kidato cha pili na madirisha mengine yanayohitaji matengenezo.

Akiwa njiani kuelekea Ngara, Dk. Magufuli alisimamishwa na wananchi wa Nyakahura ambao aliwahakikishia kuwa Serikali itaifanyia matengenezo barabara ya Nyakahura – Rusumo – Ngara akiahidi kumtuma Waziri wa Maji na Umwagiliaji kwenda kuangalia namna ya kutatua tatizo la maji na pia amechangia Sh milioni 10 katika ujenzi wa majengo ya shule.

Dk. Magufuli kesho ataendelea na ziara yake mkoani Kagera ambako atazungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika Ngara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here