23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

KWANINI NI MUHIMU WARUDI SHULE BAADA YA KUJIFUNGUA?

mwanafunzi-mjamzito

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

 TEKLA (si jina lake halisi), ni mwalimu katika shule moja ya msingi jijini Dar es Salaam.

Katika harakati za kutafuta maisha amekumbana na changamoto nyingi ambazo kama si mama yake kupambana huenda leo angekuwa na maisha mabaya zaidi.

Tekla anasema alikuwa akiishi na mama na baba yake wa kambo na kwamba mara nyingi mama yake alikuwa akiingia kazini usiku na kurudi asubuhi.

“Wakati nikiwa kidato cha tatu, siku moja wakati nimelala baba alinifuata na kunitongoza. Nilikataa na kukimbia kwenda kukaa nje hadi asubuhi alipoondoka kwenda kazini ndio nikarudi ndani kujiandaa na kwenda shule.

“Tulikuwa tumepanga vyumba viwili hivyo mimi nilikuwa nalala sebuleni halafu wazazi wangu chumbani, siku nyingine baba akaja tena akiwa ameshika panga. Niliogopa sana nilijua ataniua hivyo nikajikuta nimefanya naye mapenzi,” anasema Tekla.

Anasema baba yake huyo aliendelea kumfanyia vitendo hivyo huku akimpa vitisho na kwamba hakuwahi kumwambia mama yake.

“Wakati naendelea na masomo nikashtukia nimepata ujauzito, sikumwambia mtu niliendelea kwenda shule hadi mimba ilipofikisha miezi saba. Niliongeza kipimo cha sketi nikawa navaa na sweta kila siku ili kuficha tumbo,” anasema.

Anasema wakati mimba ilipofikisha umri wa miezi saba ilikuwa ni Desemba na baada ya kufunga shule alimuomba mama yake amruhusu asafiri kwa ajili ya likizo.

Anasema alikwenda kwa bibi yake mkoani Dodoma na alipofika aliamua kumweleza ukweli bibi yake huyo.

“Mama alitaarifiwa na kuja Dodoma, sikuwahi kusema kama baba ndiye aliyenipa ujauzito ule nilikuwa naogopa sana. Nilikaa Dodoma hadi Februari nilipojifungua…nilijifungua mtoto wa kiume lakini alifariki dunia baada ya siku mbili,” anasema.

Mwalimu huyo anasema alipumzika kwa bibi yake na baada ya likizo ya Aprili aliamua kurudi shule lakini akamuomba mama yake asomee huko huko mkoani Dodoma ambapo aliamua kurudia kidato cha tatu.

“Niliumia sana kwa sababu mama yangu ndiye alikuwa anahangaika kwa kila kitu na kunitafutia ada halafu baba akaja kunibaka…sitaki kukumbuka, namshukuru sana mama yangu hakunifukuza wala kunichukulia hatua yoyote ile na hata nilipotaka kurudi tena shule alikubali.

“Nilisoma kwa bidii na nilipomaliza kidato cha nne nilifaulu vizuri kwa kupata daraja la nne na alama 27, nilienda kusomea ualimu na baada ya kumaliza nikaajiriwa kuja kufundisha hapa Dar es Salaam.

 Kisa cha Tekla ni mfano wa matukio mengi yanayowakumba wasichana nchini, wako wanaobakwa bila kutaka na kulazimika kuacha shule kutokana na sheria kutoruhusu kuendelea na masomo.

Kitendo cha ukatili kama alichofanyiwa Tekla kinamnyima fursa ya kupata haki zake kama vile ya elimu.

Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto uliozinduliwa Jumanne wiki hiii, jijini Dar es Salaam unasisitiza juu ya kupunguza vitendo vya ukatili wa kimwili kwa wanawake na watoto kwani vinaleta kikwazo katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2015.

Tafiti zinaonyesha sababu nyingi zilizochangia wasichana kupata mimba na kukatisha masomo yao zinahusishwa pia na vitendo vya ukatili.

SABABU ZA KUPATA MIMBA

 Faustin Mroso ni Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kwamatuku iliyoko Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, anasema wazazi wengi pia wamekosa mwamko wa elimu na hata shule ikipeleka taarifa

za kutooneka kwa mwanafunzi wazazi huwa hawatoi ushirikiano.

Pia wazazi wanalaumiwa kwa kushindwa kuwatimizia watoto wa kike mahitaji yao ya msingi ya kimasomo.

Mmoja wa wanafunzi katika shule moja ya sekondari mkoani Dar es Salaam, anasema amejikuta akianza uhusiano wa kimapenzi ili kupata fedha za kujikimu.

“Mama yangu ni mfanyabiashara ndogondogo na baba yangu ni mtumishi wa umma, kila mwezi baba hunipa Sh 50,000 kwa ajili ya nauli na mahitaji mengine ya shule. Lakini baba akishanipa mama hunifuata na kuniomba zile fedha ili aongezee katika mtaji wake.

“Huwa naingiwa na huruma na kumpa kwa jinsi ninavyoona anavyohangaika kwa sababu aliwahi kuniambia baba huwa hatoi fedha za matumizi ya nyumbani, anachojua ni kulipa ada na mahitaji mengine ya shuleni,” anasema mwanafunzi huyo ambaye ni mtoto wa pili kuzaliwa kati ya watoto sita wa familia hiyo.

Anasema alilazimika kuanza uhusiano wa kimapenzi na kwamba mwanamume aliyekuwa naye alikuwa akimpa Sh 3,000 kila alipokuwa akikutana naye kimwili.

Naye Mwalimu…ansema kukosekana kwa elimu ya afya ya uzazi kumechangia wanafunzi wengi kushindwa kupokea mabadiliko ya makuzi kwa umakini.

HALI ILIVYO

Kila mwaka zaidi ya wasichana 8,000 huacha shule kutokana na mimba.

Takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi za mwaka 2010 zinaonesha katika shule za sekondari wanafunzi waliokatisha masomo walikuwa 66,069.

Katika shule za msingi waliokatisha masomo kwa sababu ya utoro (baadhi ni watoro kwa sababu ya mimba) walikuwa wanafunzi 76,246 na waliofukuzwa kwa sababu ya mimba ni 1,056.

Shule ya Sekondari Nanyamba iliyoko mkoani Mtwara ni miongoni mwa shule zilizokumbwa na tatizo hilo ambapo kwa mwaka huu wanafunzi wanane wa kidato cha pili na nne wamepata mimba.

Pia katika Shule ya Sekondari ya Kwamatuku iliyoko Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, kati ya Januari hadi Juni mwaka huu, wanafunzi sita wamepata mimba.

Mkoani Kilimanjaro wanafunzi 238 wa shule za msingi na sekondari wamepata ujauzito katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Agosti mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki, anasema Wilaya ya Rombo ndiyo inaongoza ambapo wanafunzi waliopata ujauzito ni zaidi ya 60.

Kulingana na Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978 kifungu 35 na kanuni zake za mwaka 1978 na marekebisho ya 1995 na 2002, mtoto wa kike akipata mimba ni ushahidi tosha kuwa amefanya vitendo vya ngono vilivyo kinyume na sheria za shule hivyo anafukuzwa shule.

 MJADALA WARUDI SHULE, WASIRUDI

 Kumekuwapo na malumbano ya muda mrefu kuhusu wanafunzi wanaoapata mimba kama waendelee na masomo baada ya kujifungua au la.

Kumekuwa na hoja zinazopingana na kukinzana juu ya suala hilo huku nyingi zikitawaliwa na hisia, mitazamo na imani bila kuwapo na ushahidi wa kisayansi.

Watoto wanaendelea kuteseka, wanapata mimba na kukatisha masomo, wanaathirika kisaikolojia, wanajikuta wakianza majukumu ya ulezi wangali bado wadogo na kubaki wajinga.

Shirika lisilokuwa la kiserikali linalojihusisha na masuala ya elimu (Hakielimu), mwaka 2011 lilifanya utafiti juu ya suala hilo na kupendekeza njia za kufuatwa ili kufikia mwafaka wa jambo hilo.

Chapisho la Hakielimu la mwaka 2011 linaonyesha hakuna ushahidi wa wazi ndani ya jamii unaoonesha kuwapo kwa faida za kuwafukuza shule wasichana waliopata mimba.

Kulingana na chapisho hilo, maamuzi ya kuwafukuza shule wasichana yanawasukumia kwenye umasikini wa kudumu watoto wanaozaliwa na wasichana hao na hivyo kuendeleza duara la umaskini kwenye familia zao na taifa kwa ujumla.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bunge, Hadija Telela, anasema kuruhusiwa kwa jambo hilo kutasababisha mmomonyoko wa maadili na hivyo kushusha ubora wa elimu nchini.

“Mimi naona wasirudi shule kwa sababu wakiruhusiwa vitendo vya ngono vitaongezeka na kutakuwa na upotovu mkubwa wa nidhamu,” anasema Mwalimu Telela.

Naye Sheikh Khalifa Khamis anapinga hoja hiyo kwa sababu mafundisho ya dini hayaruhusu ngono kabla ya ndoa.

“Dini zote haziruhusu ngono kabla ya ndoa hivyo, ukiruhusu watoto waendelee na masomo maana yake unahalalisha ngono kabla ya ndoa,” anasema Sheikh Khamis.

Naye mkazi wa Temeke, Dar es Salaam, Zawadi Fundiyaya, anashauri watoto wanaopata mimba wakiwa shuleni wasamehewe na kuruhusiwa kuendelea na masomo kwa sababu wengi wanakuwa bado hawajapevuka kiakili.

WAZIRI WA AFYA, ELIMU

 Waziri Ummy Mwalimu wakati anazindua Mpango kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto, alipaza sauti na kutaka wanafunzi wanaopata mimba wafikiriwe kurudi kuendelea na masomo.

“Tufikirie watoto wa maskini wanaopata mimba shuleni waendelee na masomo kwa sababu wa kwangu mimi na wewe tutampeleka private (shule binafsi) wataendelea na masomo.

“Elimu kwa watoto wa kike ndiyo mwarobaini wa kutokomeza vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto,” anasema Mwalimu.

Anasema wataanzisha sehemu rafiki katika shule za msingi na sekondari ili mtoto atakapofanyiwa jambo baya la ukatili aweze kupata msaada wa haraka.

“Kutakuwa na kamati za ulinzi na usalama wa mtoto wa kike katika kila mtaa na kijiji na pia utaanzishwa mtandao wa wanaume katika kila kata ili kulinda vitendo vya ukatili,” anasema.

Naye Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya, anasema “Suala la mwanafunzi kupata ujauzito akiwa shuleni ni jambo zito tunaliangalia kwa umakini na kipekee. Tutalifanyia kazi liweze kupata ufumbuzi, liangaliwe kwa mapana utekelezaji wake usiwe na athari kwa maeneo mengine.

Pia baadhi ya wadau mbalimbali wa maendeleo wanapendekeza ziwepo shule maalumu za ufundi stadi ambazo watapelekwa wasichana waliojifungua kuendelea na masomo na kupata ujuzi wa kimaisha.

Mwalimu mlezi wa wanafunzi wa kike katika Shule ya Sekondari ya Kwamatuku, Christina Kavishe, anashauri kuwekeza kwenye elimu ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango kwani pia kutasaidia kunapunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

“Changamoto zingine zinazoathiri makuzi ya kimaadili kwa vijana ni kutopewa maarifa na taarifa sahihi jinsi ya kutumia miili yao bila kuathiri ndoto zao,” anasema Mwalimu Kavishe.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiq, anasema “Kuna mila ya kupeana jani linaloitwa Mashale na kusuluhishana, mila hii ni potofu na inawakandamiza watoto wa kike wanaopewa mimba na wale wa kiume ambao hulawitiwa. Jambo hili linasababisha Jeshi la Polisi kufanya kazi katika mazingira magumu sana.

Elimu inabaki kuwa kitovu cha maendeleo ya binadamu popote alipo hivyo cha msingi ni kufanya utafiti kubaini ukweli na uhalisia wa jambo hilo ili tuwe na mtazamo wa kujenga na wala si kubomoa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles