25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Kura za maoni CCM zafutwa

*Dk. Bashiru atangaza uchaguzi kufutwa maeneo yenye malalamiko, vurugu nchi

* Mkoa wa Dar wawekwa chini ya ungalizi maalumu

ANDREW MSECHU –dar es salaam

KATIBU Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, amesema chama hicho kumeamuru kufutwa kwa kura ya maoni maeneo yote ambayo yalikuwa na ukiukwaji wa kanuni, kisha kurudiwa upya.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Dk. Bashiru alisema kura hizo zitarudiwa bila kujali kanuni kwa kuwa zilikiukwa katika maeneo yote yanayolalamikiwa.

Alisema wote waliokuwa wamechukua fomu sasa watapata fursa ya kuchujwa kupitia kura za wanachama na si kamati za uongozi.

Dk. Bashiru alisema kutokana na hitilafu hizo, katika maeneo yote ambayo uongozi wa chama umeorodhesha na unaendelea kuorodhesha hitilafu, upigaji kura utarudiwa tena bila kufuata utaratibu wa mchujo, kama ilivyokuwa awali.

Alisema kwa sasa wale wote waliokuwa wamechukua fomu awali watapigiwa kura na mchujo wao utafanywa kwa kura za wanachama, bila kujali idadi ya waliokuwa wamechukua fomu.

“Na kwa sasa tumeamua kufanya hivi si kwa nia ya kukiuka kanuni na taratibu, bali kwa kuwa hakuna muda wa kutosha kuanza mchakato huo upya.

“Wakati wote tumekuwa tukisisitiza utii wa katiba, kanuni na taratibu za chama. Tumekuwa tukisisitiza tusipuuze maelekezo ya chama na Serikali,” alisema.

Dk. Bashiru alifafanua kuwa ni katika utaratibu huo, uongozi umeamua kuongeza siku mbili zaidi katika mchakato wa ndani ya chama, kutoka Oktoba 29 hadi Oktoba 31 ili kukamilisha marudio hayo.

“Kwa kuwa utaratibu wa wagombea wa vyama kuchukua fomu kule serikalini unaanza Oktoba 29 hadi Novemba 4, ninaamini tutawahi kukamilisha na wagombea wetu watachukua fomu kwa wakati,” alisema.

Alisema yapo maeneo ambayo hayakuzingatia kanuni za chama katika kuteua, yapo ambayo hapakuwa na maelewano katika uteuzi na yapo ambayo hayakufuata utaratibu wa uteuzi.

“Kuna maeneo mengine hayakufuata utaratibu wa vituo, mengine yakaongeza vituo na hata mengine yakahamisha vituo bila taarifa. Lakini maeneo mengine wakachelewa kuanza kupiga kura, wakapiga muda ambao hatukukubaliana,” alisema.

Dk. Bashiru alisema maeneo mengine pia yalipuuza utaratibu wa utambuzi na uhakika wa wapigakura na kusababisha watu wasiostahili kupiga kura.

Alisema kuna maeneo mengine ambayo badala ya kufanya mchujo na kuwasilisha majina matatu kwa mujibu wa kanuni, waliwasilisha jina moja au mawili, hatua inayoonyesha kuwa kuna ujanja ujanja ulifanyika.

Dk. Bashiru alisema tatizo jingine lililoripotiwa ni kutozingatia jinsia baada ya baadhi ya wanawake waliojitokeza kuenguliwa wote na kubaki wanaume pekee.

Alisema katika baadhi ya maeneo pia siri za vikao zilivuja tofauti na taratibu za chama, hivyo kuwavuruga na kuwachanganya wanachama katika mambo yasiyo na ukweli.

Alisisitiza kuwa maeneo ambayo kura hiyo itarudiwa ni yale yatakayokuwa yamewasilisha taarifa na kutambuliwa na uongozi wa chama kuwa hitilafu hizo zimetokea.

Alisema marudio hayo yanahusisha pia maeneo yaliyofanya vizuri, lakini wasiamizi walichelewa matatizo yaliyoripotiwa zaidi Kawe na Kinondoni.

Dk. Bashiru alieleza kuwa katika Mkoa wa Dar es Salaam ndiko matatizo hayo yalipokithiri na ameagiza Kamati ya Maadili na Usalama chini ya Kanali mstaafu Ngemela Lubinga, pamoja na Katibu Mwenezi wa CCM, Humphrey Polepole kuzunguka maeneo mbalimbali ili kujua matatizo hayo na chanzo chake.

Alisema kwa kuwa Jiji la Dar es Salaam ndilo linaloongoza kwa malalakimo tofauti na mikoa mingine, kutakuwa na utaratibu mahususi wa kuyashughulikia ili kuyamaliza.

Dk. Bashiru alisema katika baadhi ya maeneo, viongozi waliokuwa wanatakiwa kusimamia mchakato wa uteuzi na kupitisha wagombea, wamejipenyeza na kuingia katika kinyang’anyiro kisha kuibuka wagombea, akiwataka wajue kuwa wana maswali ya kujibu.

Alisema katika hilo, wapo baadhi waliokuwa na uongozi lakini wakajiuzulu ili kuwania uenyekiti katika Serikali za Mitaa, hao pia wasidhani kuwa hata kama wamepita watapata uteuzi katika hatua za mwisho.

Alieleza kuwa katika suala la ukomo wa uongozi kwenye nafasi zote, chama hicho hakina ukomo tofauti na ule uliowekwa kwenye katiba, unaohusu ukomo katika nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

“Tofauti na ukomo huo wa kikatiba, chama hakina ukomo wa uongozi. Ukomo unaamuliwa na wapigakura, kama wakiona unawafaa hata kama umeongoza kwa muda gani utaongoza, wakiona haufai watakutoa.

“Kwa hiyo asitokee mtu akaanza kusema suala la ukomo, eti fulani kaongoza muda mrefu atupishe. Kuna watu ambao wana uwezo, katika uongozi siku zote wao ni vijana na watendaji wazuri, kwa hiyo ndani ya CCM hakuna suala la muhula au ukomo,” alisisitiza.

UTATA WA KURA

Katika upigaji wa kura za maoni uliofanyika juzi ili kuwapata wagombea wa nafasi za uenyekiti wa Serikali za Mitaa kupitia CCM, iliripotiwa kuibuka kwa vurugu katika baadhi ya maeneo, huku visasi vikitawala kwa baadhi ya wagombea, wengine wakitishia kutwangana ngumi.

Pia wagombea wengine walikataliwa na wanachama kuwapo katika orodha ya wagombea nafasi ya uenyekiti na uchaguzi kusimama kwa saa kadhaa.

Katika uchaguzi huo wa kura za maoni mkoani Dodoma hali ya sintofahamu  iliibuka katika Mtaa wa Mbuyuni, Kata ya Kizota, baada ya wakazi wa mtaa huo kugomea jina la mwenyekiti anayemaliza muda wake wa mtaa huo, Seleman Kaengela kuwepo kwenye orodha ya wagombea wa nafasi ya mwenyekiti kwa mara nyingine.

Pia utata ulijitokeza katika Mtaa wa Kimamba, Kwa Jongo na Kilimahewa, Kata ya Makurumla, Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam na kusababisha baadhi ya wanachama kuchapana makonde na wengine kususia uchaguzi kutokana na mizengwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles