24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

KING CLASS AANIKA SIRI YA UBINGWA WA DUNIA

Bondia wa Dunia ubingwa wa Global Boxing, Ibrahim Class ‘Kingi Class Mawe’ (katikati) akiwa na Mhariri wa Michezo wa Gazeti la Mtanzania, Mwani Nyangasa (kushoto). Kulia ni Kocha wa Viungo wa Bondia huyo, Joe Anea, alipotembelea ofisi za New Habari (2006) Ltd., jijini Dar es Salaam jana. Picha na John Dande

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

BONDIA Mtanzania aliyetwaa ubingwa wa dunia wa ‘Global Boxing Council ’ (GBC), uzito mwepesi wa Kilogram  61, nchini Ujerumani, Ibrahim Class ‘King Class Mawe’, ameanika siri ya kufanya vizuri Kimataifa kuwa ni kutokana na uongozi mzuri unaomsimamia pamoja kupanga vizuri ratiba zake.

Hivi karibuni King Class alifanikiwa kumkalisha chini bondia Jose Forero, kutoka Panama, baada ya kumzidi kwa pointi katika pambano lililofanyika nchini Ujerumani.

Bondia huyo anakuwa wa kwanza nchini Tanzania, kuandika historia ya kutwaa ubingwa huo wa mkanda wa GBC, pia aliwahi kutwaa ubingwa wa WPBF Afrika mwaka 2014 nchini Zambia.

King Class aliyasema hayo jana alipotembelea Ofisi za New Habari (2006) LTD, zinazochapisha magazeti ya MTANZANIA, BINGWA, DIMBA na RAI.

Alisema mara nyingi huwa anapanga vema ratiba zake kwa kufanya mazoezi, kula vizuri na kujiepusha na starehe zisizo za lazima ikiwa ni pamoja na ulevi.

“Unapokuwa una uongozi unaokusimamia vizuri kwa kila kitu  huku ukipanga vizuri ratiba zako na kujiepusha na mambo ambayo hayana faida, lazima utafanya vizuri kwani mchezo wetu hutakiwi kujichanganya na mambo mengi,” alisema.

Alisema baadhi ya mabondia wa hapa nchini wanajikuta wakishindwa kutamba hasa kimataifa, kwa sababu ya kujihusisha na ulevi, starehe na mambo ambayo yanawazidi kimajukumu.

Akizungumzia tofauti ya mabondia wa nje na hapa Tanzania, King Class alisema wa kimataifa wanakuwa na maandalizi mazuri tofauti na hapa, hali inayopelekea kufanya vizuri zaidi.

Aidha, King Class alieleza mipango yake ya baadaye, kuwa anaangalia zaidi kufanya vizuri kimataifa na si kuishia hapa, kwani anahitaji kuwa bingwa atakayejuliakana dunia nzima.

“Malengo yangu ni kuona nazidi kuitangaza vema Tanzania kimataifa, si kuishia hapa nyumbani na ndio maana nakuwa makini kwa kila pambano nitakalocheza kwani nahitahi kujitengenezea heshima kupitia ngumi,” alisema.

Upande wake msimamizi wa bondia huyo, Joe Anea, alivitaka baadhi ya vyama vya ngumi nchini visitafute umaarufu kupitia kwa King Class, kwani ana usimamizi wake na endapo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe, akihitaji kuonana na bondia huyo watampeleka wao kama wasimamizi wa na si chama.

“Hivi karibuni nilisikia kuwa vyama hivyo vikisema kuwa wanaangalia utaratibu wa kumpeleka King Class kwa Waziri, wakati wao hawajahusika kwa kitu chochote kwa bondia wetu ukizingatia wakati tunataka kuelekea nchini Ujerumani, tuliwaita na hawakuja hivyo kila kitu kinachomhusu King Class tunakisimamia sisi,” alisema.

Hivi karibuni Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa (TPBC), walikaririwa wakisema wanataka kumpeleka bondia huyo kwa Waziri anayehusika na michezo ili atambulike.

Kufuatia kauli hiyo, waliibuka pia Chama cha Ngumi za kulipwa nchini (PST) kupitia rais wake, Emmanuel Mlundwa aliyesema TPBC hawana haki ya kufanya hivyo kwa kuwa hawajachangia chochote labda wao PST kwa kuwa waliwahi kumwandalia pambano na ndio waliomtambulisha Panama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles