25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Kiinua mgongo kwa vigogo kaa la moto

Hussein Bashe
Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM)

Arodia Peter na Kulwa Mzee, Dodoma

PENDEKEZO la Serikali kutaka kiinua mgongo cha wabunge kikatwe kodi limegeuka kaa la moto huku wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakishangazwa kutoguswa kwa baadhi ya viongozi wakiwamo Rais, makamu wake, Waziri Mkuu, majaji, wakuu wa mikoa na wilaya.

Pamoja na hali hiyo wameitaka Serikali kuacha kutoza kodi ya ongezeko la thamani (VAT) katika utalii kwani hatua hiyo inaweza kushusha uchumi wa nchi.

Kauli hiyo wameitoa jana bungeni walipokuwa wakichangia mjadala wa bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango wiki iliyopita.

BASHE

Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alisema suala la kukata kodi kiinua mgongo cha wabunge ni kuwachonganisha na wananchi.

“Kwanini Rais ameachwa, Waziri Mkuu, mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya? Wawekeni wote tulipe kodi, hata majaji, Spika na Naibu Spika, acheni kutugawa,” alisema Bashe.

Akizungumzia VAT katika utalii, Bashe aliwashauri wabunge wengine wasikubali kupitisha makato hayo kwani hayatasaidia kuinua uchumi.

Alisema utalii ni miongoni mwa sekta zinazokuza uchumi wa nchi, hivyo ni vema suala la kuweka kodi liangaliwe upya kwani watalii wanaweza kukimbia.

“Suala la kukusanya kodi ni suala jema, lakini kuna haja ya kuangalia kwani watalii wanaweza kwenda kule ambako wamefutiwa kodi,” alisema Bashe.

Aidha mbunge huyo alisema kuwa bajeti iliyotengwa kwa ajili ya Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ni ndogo na inamfunga miguu kufanya kazi zake.

“Unawezaje kumpeleka CAG kukagua miradi bila kumuwezesha?” alisema na kushauri ofisi hiyo iongezewe fedha.

Mbunge huyo pia aliitaka Serikali kuacha kutoza kodi kwenye mitumba akisema hatua hiyo ni sawa na kuua soko dogo na matokeo yake Serikali itajenga wezi.

Alishauri kujenga kwanza viwanda vya nguo kabla ya kufikiria kutoza kodi kwenye mitumba.

Bashe pia alishangazwa na hatua ya Serikali kupitia hazina kutaka kupeleka fedha kwa Mamlaka ya Kusimamia Mali za Shirika la Reli Tanzania (RAHACO) kwa ajili ya kununua mabehewa ya Sh bilioni 161 na kusema kuwa hakuna haja ya kufanya hivyo.

“Yapo maeneo ambayo hayana sababu ya kuchukua fedha hazina kuyahudumia, RAHACO ifutwe iwe chini ya TRL, RAHACO ni kichaka cha wizi, TRL ikope,” alisema.

 ZUNGU

Kwa upande wake Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu (CCM), aliiomba Serikali kuangalia upya suala la kodi kukatwa katika kiinua mgongo cha wabunge.

Alisema wabunge wanalipa kodi takribani Sh milioni 50 kwa miaka mitano, hivyo kuna haja ya suala hilo kuangaliwa upya.

Kuhusu kutoza kodi katika mitumba, Zungu alisema hayo yanafanyika katika nchi za Afrika Mashariki ambazo zina viwanda, lakini si kwa Tanzania ambako hatuna viwanda hivyo Serikali iliangalie upya suala hilo.

Akizungumzia kodi katika miamala ya simu, alisema kampuni za simu zinataka kuonyesha anayeumia katika utaratibu huo ni masikini.

Alisema watakaoumia ni kampuni za simu hivyo alipendekeza kodi ziendelee kukatwa na kwamba kuna haja ya kubadilika kwani bila kodi mambo hayaendi.

PROF. SIGALA

Naye Mbunge wa Makete, Profesa Norman Sigala (CCM),  alisema Serikali haijatenda haki katika ukusanyaji mapato kwani kuna migahawa mikubwa haitoi risiti.

Alipendekeza polisi wafundishwe  namna ya kufuatilia kodi ili waingie mtaani kukusanya kodi.

Akizungumzia kutoza kodi katika kuhamisha hisa, alisema  hiyo haipo mahali kokote na kwamba Waziri wa Fedha, Dk. Mpango anatakiwa kufahamu Soko la Hisa la Dar es Salaam lilianzishwa kwa ajili ya kuongeza wawekezaji, kuwatoza kodi ni kuwafukuza.

Aliishauri Serikali iache kufanya hivyo na kuongeza kwamba kodi katika miamala ya simu iendelee kukatwa.

 MSONGOZI

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Jackline Msongozi (CCM),  alisema kutoza kodi katika utalii ni sawa na kujikaba wenyewe.

Alisema Serikali ikubali kuondoa VAT katika utalii ili kipato kiongezeke kwani bila hivyo itakosa dola za Marekani bilioni 2.5.

 AESHI

Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilal (CCM),  aliomba CAG aongezewe fedha kwani bila kufanya hivyo atakuwa ombaomba na utafika wakati atashindwa kuwachunguza anaowaomba.

Akizungumzia kiinua mgongo cha wabunge, alisema akitokea mbunge wa Chadema, hasa David Silinde, akaandika barua ya kukubali kukatwa kodi, yeye atakuwa wa pili kufanya hivyo.

Mbunge huyo alipendekeza suala la kukata kodi katika kiinua mgongo lifutwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles