30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Zitto atoa mazito kwa Magufuli

Zitto Kabwe
Zitto Kabwe

* AWATAKA CCM WAMDHIBITI, WAKISHINDWA WAPINZANI WATAFANYA KAZI HIYO

* AWAPIGA CHENGA POLISI KWA SAA 36, AHOJIWA NA VYOMBO VYA DOLA DAR

NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema anasikitishwa na Serikali ya Rais John Magufuli kuwakamata wapinzani, huku akikitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimdhibiti haraka.

Zitto ambaye amekuwa akisakwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam tangu Jumamosi, alisema kama CCM itashindwa kumdhibiti Rais Magufuli, basi wapinzani watatumia njia ya kikatiba kufanya kazi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho, Dar es Salaam jana, Zitto alisema Jeshi la Polisi limepokea maagizo kutoka ngazi za juu kuwakamata wapinzani akiwamo yeye.

Alisema anachokifanya Rais Magufuli ni kujenga mazingira ya kuwa na mtu mmoja anayezungumza, huku wengine wakidhibitiwa na vyombo vya dola.

“Sisi hatumwogopi Rais Magufuli kwa sababu yeye si Mungu, bali ni rais… leo anaweza akawa rais kesho akaondoka kwenye nafasi hii.

“Natoa salamu maalumu kwa CCM, lazima wawe na uwezo wa kumdhibiti rais anayetokana na chama chao, yeye si kiongozi wa chama bali ni mjumbe wa Kamati Kuu kutokana na nafasi yake ya urais.

“Viongozi wa chama wakae na kiongozi wao na wasimwogope kwa sababu kumejengeka tabia ya wabunge, viongozi wa CCM, viongozi wa Serikali kumwogopa,” alisema.

Zitto alisema endapo CCM itashindwa kumdhibiti Rais Magufuli, kuna hatari anaweza kusababisha wananchi wakakosa imani naye, jambo ambalo hawatakubali kuliruhusu.

Alisema Serikali imepiga marufuku watu wasifanye mikutano ya kisiasa wala makongamano, jambo ambalo kikatiba halikubaliki hata kidogo.

Zitto alisema wanashindwa kufahamu nini kinachofichwa na watawala katika bajeti ya mwaka 2016/17, hadi kufikia Serikali kuogopa kuzuia watu kutoa mawazo yao.

“Tunalaani vikali juhudi zinazofanywa na Serikali kuruhusu tabia za kubana wapinzani ambazo zinajengeka nchini… mambo haya tuliachana nayo miaka 20 iliyopita…

“Kama wapinzani tunadhibitiwa kiasi hiki, ipo siku nawaambia Serikali itafanikiwa kudhibiti vyama vya siasa, itahamia kwenye vyombo vya habari,” alisema.

Zitto alisema tangu kuanza mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, hakujawahi kutokea jaribio la kupindua Serikali tofauti na ilivyokuwa wakati wa chama kimoja.

Alisema kama Rais Magufuli ataendelea kuwabana watu wasitoe sauti zao, wanaweza kutumia njia nyingine kudai haki yao ya kikatiba.

“Endapo hali hiyo itaendelea kuna uwezekano mkubwa wa Rais Magufuli akaweka rekodi ya kutawala muhula mmoja, kwa sababu Watanzania hawatamkubalia kutokana na mwenendo wake.

“Rais anatumia Jeshi la Polisi kudhibiti upinzani, hatofanikiwa na wanasheria wetu wanajipanga ndani ya siku mbili kufungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ya kutaka kupata tafsiri ya haki ya kikatiba ya vyama vya siasa kukutana na kufanya siasa,” alisema Zitto.

Alisema kumekuwa na dhana miongoni mwa Watanzania kwamba hata ziara zake alizofanya nchi jirani huenda kuna mambo kadhaa alijifunza ikiwamo namna ya kudhibiti upinzani.

“Inawezekana ziara yake ya kwanza nje ya nchi aliyokwenda Rwanda, ajifunza namna ya kudhibiti upinzani.

“Tunamwambia Tanzania si Rwanda, bali ni huru na ya kidemokrasia na itaendelea kuwa hivyo,” alisema.

 KUWINDWA

Akizungumzia kuhusu kusakwa na polisi pamoja na kuzuiwa kongamano la chama chake kujadili mapendekezo ya bajeti ya Serikali, Zitto alisema hadi jana jeshi hilo halijatoa sababu zozote za kutaka kumkamata.

Alisema anasikitishwa na jeshi hilo kwa kushindwa kufuata taratibu za kumkamata, badala yake wamekuwa wakimvizia.

“Hadi sasa polisi hawajatoa sababu ya kunitafuta na kuzuia kongamano letu, wameendelea kunivizia tangu Jumamosi hawajafanikiwa.

“Nataka kuwaambia wananchi kuwa nipo salama kwa siku mbili ambazo natafutwa, vijana wetu wa usalama wamejitahidi  kuhakikisha sikamatwi, hii ni kuwaonyesha polisi hawawezi kunikamata wanavyotaka wao, bali kwa kufuata utaratibu uliopo,” alisema Zitto.

SAA 36 AWAKWEPA POLISI

Chanzo cha kuaminika kililiambia gazeti kuwa baada ya kupatikana kwa taarifa za kusakwa kwa mbunge huyo tangu lilipotangazwa kongamano la kujadili bajeti lililoandaliwa na chama chake, alikuwa akisakwa na polisi.

Kilisema kuwa tangu Jumamosi ya wiki iliyopita Zitto alijikuta akiwakwepa polisi kwa muda wa saa 36 huku akipita huku na kule kujinusuru na mkono wa askari hao.

“Zitto baada ya kupata taarifa za kusakwa kwake aliondoka kwake Jumamosi, na alikwenda hadi kwa jamaa yake mmoja anayeishi eneo la Makongo Juu.

“Baada ya dakika chache vijana wa ulinzi wa ACT-Wazalendo  ambao walikuwa wakifuatilia kila hatua, walimtaka ondoke katika eneo hilo na alitumia usafiri wa bajaji hadi eneo la Mlimani City ambako alichukua gari na kwenda Tabata nyumbani kwa marehemu mama yake.

“Alipofika katika hilo eneo akiwa katika gari maalumu, walinzi wa ACT-Wazalendo ambao pia walikuwa wamepiga kambi walimtaka aondoke kwani kulikuwa na askari waliovaa kiraia ambao walikuwa wakizunguka katika eneo hilo,” alisema mtoa habari wetu ambaye hakutaka kutajwa jina lake.

Kutokana na hali hiyo, Zitto aliondoka na kwenda Kinyerezi ambako alifuturu huko kwa mmoja wa rafiki zake na baadae usiku wa manane alikwenda maeneo ya Kinondoni alikojichimbia hadi jana alipojitokeza hadharani.

 KONGAMANO

Akizungumza jana kuhusu kongamano la kujadili katiba, Zitto alisema pamoja na kuwapo hali hiyo, wataendelea na msimamo wao wa kulifanya katika ofisi za chama chao.

Alisema kongamano hilo litafanyika leo saa 9 mchana na kuwataka wananchi wajitokeze ili kuijadili bajeti ya Serikali yao.

KAMANDA SIRO

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro alikiri jeshi hilo kumsaka Zitto.

Kamanda Sirro alisema Zitto alitakiwa kufika Kituo cha Kati jana, lakini alikiuka agizo hilo na kuamua kufanya mkutano na waandishi wa habari wakati aliagizwa asifanye.

Alisema mwendelezo wa mikutano hiyo, ni dalili ya kuleta uchochezi ndani yake.

“Zitto tulimkataza asifanye mkutano wowote na leo (jana) tutampata na tutamkamata tu, na huo mkutano anaotaka kufanya ofisini kwake ni marufuku kwa sababu lengo lake ni uchochezi.

“Bila amani hakuna siasa, na siasa inafanyika kwa sababu amani ipo, kuna makongamano mengi tunatoa vibali yanafanyika kwa amani, kwa kawaida polisi tunatoa ulinzi, kwa hili hatutampa nafasi mtu anayeichafua nchi,” alisema Kamanda Sirro.

ZITTO POLISI

Ilipofika saa 10:30 jioni jana, MTANZANIA ilipata taarifa ya kiongozi huyo kuitwa katika Kituo cha Polisi cha Kati, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Akizungumza na MTANZANIA, Ofisa Habari wa ACT-Wazalendo, Abdallah Khamisi, ilisema polisi walipiga simu ya kumwita Zitto kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi, Venance Msebo, wakimtaka ahakikishe kiongozi huyo anafika katika Kituo cha Polisi cha Kati.

Alisema kuwa Zitto alifika kituo cha polisi saa 11 jioni akiwa na viongozi wa chama chake pamoja na mwanasheria wake Stephen Mwakibola na kuhojiwa kwa saa moja.

Baada ya mahojiano hayo Zitto aliachiliwa ambapo alizungumza kwa ufupi kuwa polisi walikuwa wanamhoji kuhusu kongamano lililozuiwa na kwamba leo atatoa taarifa zaidi kuhusu wito huo baada ya kukutana na uongozi wa chama chake.

 WASOMI

Nao wasomi wa kada mbalimbali wamepinga kitendo cha Jeshi la Polisi kukamata wanasiasa na kuzuia mikutano ya hadhara kisiasa kwa kudai kuwa ni ukiukwaji wa katiba.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wasomi hao waliliambia MTANZANIA kuwa kitendo hicho si tu ni ukiukwaji wa demokrasia, bali pia ni kuishambulia katiba ya nchi ambayo inaruhusu demokrasia.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu, alisema kitendo hicho kinaonyesha Serikali imeamua kuishambulia katiba moja kwa moja.

Alisema katiba inaruhusu wananchi kukusanyika na kuwa na uhuru wa kushiriki katika mambo ya siasa kwa kuwa nchi inaendeshwa na mfumo wa demokrasia.

“Kuzuia mikutano ya siasa ya hadhara na kuwakamata baadhi ya wanachama wa vyama vya upinzani… jambo hili linaanza kuwatia wasiwasi wananchi,” alisema Profesa Baregu.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Kitila Mkumbo alisema kitendo kilichofanywa na jeshi hilo si sahihi kwa kuwa siasa ni sehemu ya shughuli za jamii.

“Kitendo cha kuwakamata wanasiasa wakati wanafanya shughuli zao za kila siku ni kwenda kinyume na katiba ya nchi… vyama hivi vimesajiliwa kisheria na kikatiba na Msajili wa Vyama vya Siasa anavitambua,” alisema.

Juzi Jeshi la Polisi mkoani Mwanza lilimkamata Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la chama hicho (BAVICHA), Patrobas Katambi, Katibu Mkuu wa Vijana, Julius Mwita, Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka na viongozi wengine wa chama hicho.

                               Imeandaliwa na Jonas Mushi, Asifiwe George, Herrieth Faustine na  Jamillah Shemni 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles