22.1 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Profesa Lipumba abadili gia ardhini

Profesa Ibrahim Lipumba
Profesa Ibrahim Lipumba

CHRISTINA GAULUHANGA NA HARIETH MANDALI, DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amebadili gia ardhini na kulazimika kufuta uamuzi wake wa kujiuzulu uenyekiti wa CUF.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, alisema amekwisha kumwandikia barua Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, kuhusu uamuzi wake  wa kurejea katika nafasi  hiyo na kutengua barua ya awali ya kujiuzulu aliyoiandika Agosti 5, mwaka jana.

Profesa Lipumba   alisema   amechukua uamuzi huo baada ya kutafakari kwa kina hali ya siasa nchini yakiwamo yanayoendelea Visiwani Zanzibar na kuona inahitajika nguvu ya pamoja  kukabiliana na hali hiyo ndani ya chama.

Profesa Lipumba ambaye ni mtaalamu mbobezi wa uchumi duniani, alisema sababu kubwa iliyomfanya abadili uamuzi huo ni baada ya makundi ya wanachama   na viongozi wa dini kumtaka arejee katika nafasi yake ili kukijenga chama akiwa na viongozi wenzake.

Alisema ametafakari kwa kina maombi  hayo kwa kuzingatia hali halisi ya siasa Visiwani Zanzibar ambayo kwa sasa si shwari.

Profesa Lipumba  alisema   amezingatia Katiba ya chama hicho, Ibara ya 117 ambayo inaelezea kwa undani jinsi kiongozi anavyoweza kujiuzulu na  kurejea tena ndani ya chama hicho.

“Ibara ya 117 ya Katiba ya chama chetu inaelezea jinsi kiongozi anavyoweza kujiuzulu na kurejea kwenye chama.

“Hivyo tayari nimemuandikia barua Katibu Mkuu wa Maalim Seif Sharif Hamad kumueleza nia yangu ya kurejea katika wadhifa huo na barua hiyo   itapelekwa katika Mkutano Mkuu wa chama unaotarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu ambao ndiyo utatoa uamuzi wa mwisho.

“ Tayari wanasheria wa chama wameanza mchakato wa kuipitia barua hiyo kwa mujibu wa sheria na baadaye watatangaza uamuzi wao,” alisema Profesa Lipumba .

Alisema kwa sasa inahitajika nguvu ya pamoja  kwa ajili ya kukijenga chama kwa vile  hali ya siasa ni ngumu jambo ambalo linahitaji uwepo wa demokrasia ya kweli na ushirikiano wa dhati.

Profesa Lipumba alisema wakati Rais Dk. John Magufuli   akizindua Bunge la 11 alizungumzia mambo mbalimbali ambayo yaliungwa mkono lakini ili mambo yaende sawa ni jambo la muhimu kuwa na ushirikiano kwa kuwa kuna harufu ya uendeshaji nchi kwa ubabe.

“Tunataka wabunge wawe huru bungeni, watoe maoni yao pia yasikilizwe tofauti na hivi sasa ambavyo  Bunge linaendeshwa kibabe,”alisema Profesa Lipumba.

Alizungumzia Uchaguzi Mkuu uliopita,  alisema kuna mambo mengi yamejitokeza  ikiwamo kupokwa ushindi kwa Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye alishinda katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 25, 2015.

Hata hivyo hakuweza  kueleza kwa undani sababu zilizomfanya atake kurejea katika nafasi hiyo ingawa katika uamuzi wake  alioutoa Agosti 5, mwaka jana  alidai kutoridhishwa na hali ya mambo ikiwamo umoja ndani ya Ukawa.

Sababu nyingine aliyoitoa ni kupokewa kwa aliyekuwa mgombea urais aliyekuwa anaungwa mkono na vyama Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, Edward Lowassa.

Uchambuzi wa bajeti

Awali kabla ya kutangaza uamuzi huo, Profesa Lipumba aliichambua bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2016/17, akisema ni mzigo na haitekelezeki huku akiwataka vijana kusahau suala la kupata ajira.

Serikali ya Rais Dk. John Magufuli, imeonekana kutoa kipaumbele zaidi katika sekta ya viwanda na biashara lakini fedha zilizotengwa kwa ajili ya  kazi hiyo hazitoshelezi, alisema.

Alisema sekta ya viwanda nchini imeghubikwa na changamoto lukuki zikiwamo ubovu wa miundombinu kama ya barabara, tatizo la maji na umeme.

“Ukiangalia jinsi fedha zinavyoonyesha katika bajeti hiyo, inaonekana nzuri kwa maandishi   lakini kwa utekelezaji bado ni kitendawili hasa ukizingatia kuwa kwa sasa Serikali imejitoa kuwa tegemezi katika misaada kutoka nje,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema katika mwaka 2016/17, Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji  imetengewa Sh bilioni 81.9 kwa ajili ya kutekeleza  majukumu ya wizara.

Kati ya fedha hizo Sh bilioni  41.9 ni kwa ajili ya matumizi ya ya kawaida na Sh bilioni 40 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo, fedha ambazo ni asilimia 0.34 ya bajeti ya maendeleo, alisema.

“Hii ni kuwahadaa Watanzania  waiite bajeti hii kama ni ya kuongeza uzalishaji viwandani na kupanua fursa za ajira jambo ambalo lina kitendawili,” aliongeza.

Akichanganua kuhusu viwango vya riba na utata wake katika utekelezaji, Profesa Lipumba alisema   bajeti hiyo inategemea kuongeza ukopaji wa ndani kwa asilimia 50.

“Riba na mikopo kwa jumla iliongezeka kutoka  wastani wa asilimia 15.75 Desemba mwaka 2014 hadi asilimia 16.41 Desemba mwaka jana. Hata hivyo wafanyabiashara wadogo na wa kati wanatozwa riba za juu ya asilimia 20 na kuendelea,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema riba iko juu kwa sababu riba kwenye dhamana za Serikali ilikuwa wastani wa asilimia 18.25 mwaka jana ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.45.

Alisema deni la taifa hadi kufikia mwishoni mwa Machi mwaka huu, lilifikia Sh bilioni 45, 443.2 ikilinganisha na Sh bilioni 35,010.4  Machi mwaka jana, ambalo ni   ongezeko la asilimia 29.8.

“Ili kuonyesha kuwa deni la taifa halikui kwa kasi ya juu, alielezea kwa kutumia dola za Marekani kwa kuwa shilingi imeporomoka kwa kiasi kikubwa.

“Hadi kufikia Machi mwa huu, deni la taifa liliongezeka na kufikia Dola za Marekani bilioni 20.94 ikilinganishwa na Juni mwaka jana ambako deni lilikuwa Dola za Marekani  bilioni 19.69,” aliongeza.

Wanachama wapongeza

Wakati anazungumza na wanahabari ndani ya ukumbi wa Shaban Mloo Makao Makuu ya CUF jana wanachama walikuwa wamefurika nje ya ukumbi huo

Mwanachama wa CUF kutoka tawi la Cossovo, Manzese, Juma Yasir, alisema hatua ya kurejea ndani ya chama kwa kiongozi huyo itaongeza uimara wa chama hasa   upande wa bara.

Alisema kwa   miezi tisa ambayo Profesa Lipumba alijiuzulu limeonekana pengo kubwa  hivyo kurejea kwake kunaleta matumaini mapya ndani ya chama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles