Imechapishwa: Sat, Oct 7th, 2017

KAPO HIZI MAJUU SOMO KWA MASTAA BONGO

Na BADI MCHOMOLO

WATAALAMU wa uhusiano wanadai kwamba hakuna kitu kigumu kama watu walio kwenye uhusiano kudumu kwa muda mrefu bila kuachana.

Kudumu kwenye uhusiano ni moja ya mitihani mikubwa  katika maisha ya binadamu; wapo wanaofaulu japokuwa hupitia changamoto mbalimbali za maisha.

Kwa upande wa mastaa wa Bongo, wengi wameonekana kukabiliwa na changamoto hiyo na kujikuta wakibadilisha wapenzi kila kukicha.

Hapa mastaa wetu wanaweza kujifunza kupitia mastaa wenye majina makubwa majuu ambao wamedumu kwa muda mrefu kwenye uhusiano wao bila mizengwe.

JAY Z, BEYONCE

Hii ni miongoni mwa kapo ambayo ina mvuto wa hali ya juu katika mastaa barani Ulaya, mbali na kufika hapo walipo na kupata watoto watatu lakini wamepitia mambo mengi ambayo yangeweza kuwatenganisha.

Beyonce aliweka wazi kuwa walianza uhusiano akiwa na umri wa miaka 19, lakini alianza kumjua Jay Z akiwa na umri wa miaka 18 na sasa ana umri wa miaka 36 na Jay Z sasa ana umri wa miaka 47.

Beyonce amedai haikuwa kazi rahisi kuwa na uhusiano na mtu ambaye amemzidi umri kwa miaka 11, lakini walikuwa na mapenzi ya kweli ndiyo maana wameweza kudumu.

Mwaka 2005, Beyonce na Jay Z, waliripotiwa kuwa wamemwagana kutokana na Jay Z kuhusishwa kutoka na Rihanna, lakini ilidaiwa kuwa hiyo ilikuwa ni mipango ya kuwafanya wawili hao waachane, lakini hawakuweza kuachana na wapo hadi sasa wakiwa na familia ya watoto watatu.

VICTORIA, DAVID BECKHAM

Mapenzi ni kama upofu, ndivyo unavyoweza kusema kwa msanii wa muziki na mwanamitindo maarufu nchini England, Victoria Beckham ambaye amefunga ndoa na nyota wa soka wa zamani wa timu ya Taifa ya England na klabu ya Manchester United na Real Madrid, David Beckham.

Victoria mwenye umri wa miaka 43, aliwahi kusema kuwa uhusiano wake na Beckham ulianza akiwa na miaka 19 na sasa wamefanikiwa kuwa na watoto wanne.

Victoria alisema hakuamini kukutana na mchezaji huyo na kuanza uhusiano kwa kuwa mrembo huyo alikutwa anakunywa pombe, lakini Beckham alishindwa kuzuia hisia zake na kuanza kufanya mazungumzo naye.

Hatimaye baada ya hapo waliweza kupeana mawasiliano na kisha kuanza kuonekana kwenye viwanja mbalimbali vya starehe, lakini Beckham aliweka wazi kuwa kitu ambacho kilimfanya aendelee kuwa na mrembo huyo ni kutokana na kuwa anamkumbusha mara kwa mara mambo ya soka lake.

WILL SMITH, JADA PINKETT

Uhusiano wa wawili hao unaonekana kuwa imara zaidi kwa kuwa hadi sasa wamefikia miaka 20 ya uhusiano wao.

Smith ambaye anafanya vizuri katika filamu na muziki, alifunga ndoa na Jada Pinkett mwaka 1997 na kufanikiwa kupata watoto wawili Jaden na Willow Smith.

Katika kipindi cha miaka 20 wamekutana na changamoto mbalimbali, lakini uvumilivu na mapenzi ya dhati yamewafanya hadi leo hii wawe pamoja.

SNOOP DOGG, SHANTE

Rapa Snoop Dogg alianza kuwa kwenye uhusiano na Shante Broadus tangu wakiwa shule huku wakisoma darasa moja.

Uhusiano wao haukuwa wa siri na waliamua kuuweka wazi mara baada ya kumaliza shule, baada ya hapo wakaamua kufunga ndoa mwaka 1997 na hadi sasa bado wapo kwenye ndoa.

DR DRE

Ni mkongwe wa muziki wa Hip Hop nchini Marekani, amekuwa akifanya vizuri kutokana na kazi yake ya kuandaa midundo ya nyimbo mbalimbali.

Ni miongoni mwa mastaa waliopo kwenye ndoa kwa miaka mingi, alifanikiwa kufunga ndoa na mke wake Nicole Young tangu mwaka 1996, hadi leo hii bado wapo pamoja.

KANYE, KIM

Rapa Kanye West na mwanamitindo Kim Kardashian ni miongoni mwa mastaa ambao uhusiano wao unaonekana kuwa na mvuto mkubwa.

Kardashian amedai kuwa mara ya kwanza kukutana na rapa huyo ilikuwa 2002 au 2003 wakati anarekodi wimbo na rafiki yake Brandy, hivyo walianza uhusiano na baada ya muda aliweka wazi kuwa mapenzi anayoyapata kutoka kwa rapa huyo ni tofauti na anajuta kwa nini amechelewa kumjua.

Hata hivyo wawili hao wamepitia changamoto mbalimbali juu ya uhusiano wao, lakini wameweza kupambana nazo na wanaamini wanaweza kuendelea kuwa pamoja daima, sasa wanatarajia mtoto wa tatu.

Weka maoni yako

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>

YOUTUBE

KAPO HIZI MAJUU SOMO KWA MASTAA BONGO