24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

IGP SIRRO: SILAHA ILIYOTUMIKA KWA LISSU NI SMG

*Asema alikuwa hajui kama anafuatiliwa

Na PATRICIA KIMELEMETA

MKUU wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini, Simon Sirro, amesema risasi zilizomjeruhi Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, zilitoka katika bunduki aina ya SMG, zinazotumiwa na wahalifu wengi.

Kauli hiyo aliitoa jana Dar es Salaam, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo lililomkuta Lissu, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema).

Sirro alisema silaha hizo zimekuwa zikiingizwa nchini na wahalifu kwa njia mbalimbali, jambo ambalo ni rahisi kupatikana.

Alisema kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi limeunda timu ya wapelelezi waliobobea kutoka Makao Makuu ya Dar es Salaam na wamekwenda mkoani Dodoma ili kufuatilia tukio hilo na kusaidia kupatikana ukweli wake.

“Tumetuma wapelelezi waliobobea kwenda mkoani Dodoma kwa ajili ya kufuatilia suala hilo, hivyo basi tunaamini wahusika wa shambulizi hilo tutawapata na kuwachukulia hatua za kisheria,” alisema.

Sirro alisema timu hiyo imekwenda kuongeza nguvu kwa askari waliopo mkoani humo, ambao tayari wameanza kufuatilia suala hilo tangu lilipotokea.

Pia alisema jeshi hilo linafuatilia wananchi waliokuwa wakitoa taarifa kwenye mitandao ya kijamii ili waweze kuisaidia polisi katika tukio hilo.

Alisema kwa sasa wanafuatilia taarifa hizo wanazoamini zinaweza kuwasaidia kwenye uchunguzi wao.

“Tumeona taarifa nyingi zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii ambazo nyingine zilikuwa zinawataja watu mbalimbali wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo, tumetuma vijana wetu ili waweze kufuatilia kwa ajili ya kuwaita ili wahojiwe na kutusaidia katika uchunguzi wetu,” alisema.

Pamoja na hilo, IGP Sirro alisema Lissu hajawahi kutoa taarifa katika chombo chochote cha ulinzi na usalama kwamba anafuatiliwa na watu wasiojulikana na hatua hiyo imewafanya washindwe kujua kinachoendelea dhidi yake.

Hivi karibuni, Lissu, alitoa taarifa kwa waandishi wa habari kwamba alikuwa anafuatiliwa kwa wiki tatu na vijana wasiojulikana wanaotumia gari aina ya Toyota Premio, yenye namba za usajili T460 CQV na aliwazuia karibu na Kanisa la Mtakatifu Petro la Oysterbay, Dar es Salaam.

“Lissu hajawahi kutoa taarifa za kufuatiliwa na watu wasiojulikana, mambo haya ndio kwanza tunasikia leo (jana), yawezekana alikuwa akizungumza kisiasa, tunamuomba Mungu amponye ili aweze kutuambia suala hilo tutakaloweza kulifanyia kazi,” alisema.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles