27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

SAA 17 ZA KUMUOKOA LISSU

AGATHA CHARLES Na MAREGESI PAUL -DAR/DODOMA

HATIMAYE, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, amefanyiwa upasuaji wa mara ya pili uliochukua saa saba katika Hospitali ya Nairobi, nchini Kenya, ili kuondoa risasi mwilini mwake zilizokuwa zimemjeruhi eneo la tumbo, miguu na mkono.

Upasuaji huo unatanguliwa na ule uliofanyika hapa nchini juzi, katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, ambao ulichukua takribani saa 10.

Taarifa iliyotumwa jana jioni na  Mkuu wa Idara ya Uenezi Chadema, Hemed Ali, ambaye ameambatana na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa kumsindikiza Lissu kwenye matibabu nchini Kenya, ilieleza kuwa, upasuaji huo ulianza saa nne jana asubuhi na kukamilika saa 11 jioni.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, madaktari walieleza upasuaji huo kukamilika kwa mafanikio.

Ilielezwa kuwa Lissu, ambaye alinusurika kifo kutokana na watu wasiofahamika kummiminia risasi kwenye gari wakati akijiandaa kushuka nyumbani kwake mjini Dodoma, alifanikiwa kutolewa chumba cha upasuaji na kuwekwa chumba maalumu cha uangalizi wa karibu zaidi (Executive ICU).

Hemed alisema madaktari waliwaeleza kuwa, hakukuwa na tishio lolote la kiafya, kwani Lissu alikuwa macho akiwa na fahamu zote.

“Na hii ndio ilikuwa hatua ngumu na Mungu ametupitisha, hivyo tuendelee kumuombea apone haraka,” alisema.

Katika taarifa yake ya awali, Hemed alisema Lissu alisafirishwa usiku wa kuamkia jana kwa ndege ya kukodi ambapo aliwasili nchini Kenya saa saba usiku na kupokelewa na jopo la madaktari walioanza kumtibu kuanzia uwanja wa ndege hadi hospitali ya Nairobi.

“Tangu jana alipofika alifanyiwa stabilization ili aweze kukabiliana na surgery (upasuaji) na zoezi hilo lilifanikiwa vizuri na madaktari wametueleza kuwa hakuna hali yoyote ya hatari na matibabu yake yanaendelea kwa mafanikio,” alisema Ali.

Pamoja na hilo, Hemed alieleza kushangazwa na kitendo cha Ubalozi wa Tanzania  nchini humo kutowapa ushirikiano.

“Chakushangaza hadi sasa tangu tuwasili hatujapata ushirikiano wowote wa ubalozi wa Tanzania hapa Nairobi, si kwa balozi au maofisa wowote wale wa ubalozi. Freeman Mbowe amezungumza na vyombo mbalimbali vya habari pia taarifa yake itatoka punde,” alisema Hemed.

Akizungumza na Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, Mbowe alielezea shambulio lililompata Lissu kuwa ni kubwa na limemuumiza sana.

“Maisha yake yako stable (imara), timu ya madaktari pale Dodoma ilimsaidia sana. Risasi 21 na zaidi 25 za SMG kwenye mwili wa binadamu siyo kazi ndogo, madhara yake ni makubwa. Zipo risasi zimeingia kwenye miguu, mikono, tumboni zimesababisha madhara mbalimbali, sasa yote hayo tutayatolea ufafanuzi baadaye baada ya madaktari kumaliza kazi zao za uchunguzi,” alisema Mbowe.

Alisema madaktari wanapigana kuokoa maisha ya Lissu na hivyo kutoa matumaini kwamba hali yake itaimarika.

“Pamoja na majeraha aliyoyapata alipoteza damu nyingi sana. Hata Dodoma alilazimika kuongezewa damu zaidi ya pointi tisa, ni damu nyingi sana na hata kwenye ndege tulikuwa bado tunamuongezea damu hadi kufika hapa kwa sababu majeraha ya risasi yalikuwa mengi na yalimfanya apoteze damu nyingi sana. Lakini sasa anaendelea vyema na wanaendelea na uchunguzi wa kawaida,” alisema Mbowe.

Kuhusu swali la mwandishi kuwa ni nani wanamhisi kutekeleza shambulio hilo, Mbowe alisema haoni kuwa walikuwa ni wezi au wahalifu wa kawaida.

“Sioni uwezekano wowote wa kuwa wezi, hawa walipania kuteketeza maisha yake, siwezi nikasema ni wa serikali, siwezi nikasema ni watu wa ulinzi na usalama, lakini kwa vyovyote ni watu walikusudia kumuua Lissu, si kwasababu ya matukio ya kihalifu ama ya nia ya ujambazi,” alisema Mbowe.

Alisema nia ya ujambazi inaambatana na kuchukua kitu au nia ya kumuua kwa ugomvi fulani ambao Lissu si mgomvi na kwamba hajawahi kusikia hilo.

“Kwa vyovyote ni shambulio lina mkono wa kisiasa, nani amelifanya hatujui na kwasababu gani, kila mmoja ana uwezo wa kuchambua kupata ukweli uko wapi, sasa machine gun ya risasi 21 kwa kawaida si jambazi, jambazi anaua mtu kwa risasi moja au mbili, hana sababu ya kukumiminia risasi halafu asiondoke na chochote hata laptop,” alisema Mbowe.

“Ni lazima hofu yetu ya kwanza iende kwa wale ambao walikuwa ni mahasimu wakubwa wa chama chetu, wamekuwa mahasimu wakubwa wa Lissu, mahasimu wakubwa wa demokrasia katika nchi yetu, hatusemi moja kwa moja ni wao, lakini hofu ya kutuongoza kuwa ni wao lazima tuwe nayo,” alisema Mbowe.

Akijibu namna wanavyochukulia shambulio hilo, alisema: “Ni mwendelezo wa matukio mengi, si tukio la kwanza, lakini la kushambulia kwa risasi moja kwa moja ni tukio la kwanza.”

Mbowe alisema wanataka  jamii ya kimataifa ilione kwamba Tanzania si salama, demokrasia Tanzania si salama na kwamba jumuiya ya kimataifa iliangalie inawezaje kuisaidia Tanzania, nchi ambayo ilipata heshima kubwa huko nyuma kwa kuwa kisiwa cha amani.

Wakati huo huo, akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk. James Kiologwe, alielezea upasuaji waliomfanyia Lissu hospitalini hapo juzi kabla ya kupelekwa Kenya, akisema ulikuwa mgumu na walijitahidi kuhakikisha wanaokoa maisha yake.

“Lissu alikuwa amepoteza damu nyingi na walimwongezea ndipo wakaanza kufanya upasuaji,” alisema Kiologwe.

Alipoulizwa iwapo walizitoa risasi zilizokuwa mwilini, Kiologwe alisema hawezi kulizungumzia hilo.

“Unaponiuliza ugumu ulikuwa wapi sina jibu pia na hilo tulizitoa au hatujazitoa, sina majibu kwa sababu mimi sina mamlaka ya kuyazungumzia hayo,” alisema Kiologwe.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alitoa taarifa ya shambulizi dhidi ya Lissu jana bungeni akisema gari alilokuwa amepanda mwanasiasa huyo, lilishambuliwa kwa risasi kati ya 28 na 32.

Ndugai alisema, kati ya hizo, risasi zilizofanikiwa kumpata zilikuwa tano, ambapo moja ilimpiga mkononi, mbili miguuni na mbili tumboni.

Kwa mujibu wa Ndugai, tukio hilo lilimfika Lissu saa saba mchana alipokwenda nyumbani kwake kwa ajili ya kupumzika baada ya Bunge kusitisha shughuli zake.

“Alipofika nyumbani kwake Area D, site III na kabla hajashuka kwenye gari lake, watu wasiojulikana wakiwa kwenye gari jeupe aina ya Nissan ambalo namba zake hazikutambulika, walianza kushambulia gari la Mheshimiwa Lissu kwa risasi”.

Ndugai alisema baada ya shambulizi hilo, Lissu alichukuliwa kwa kutumia gari la familia ya Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson ambaye ni jirani yake na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

“Alipofikishwa hospitalini hapo, alipelekwa moja kwa moja kwenye chumba cha upasuaji na kufanyiwa upasuaji ili kuzuia damu isiendelee kuvuja. Upasuaji huo uliongozwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Dk. Mpoki Ulisubisya, akisaidiwa na madaktari bingwa wa Mkoa wa Dodoma.

“Baada ya upasuaji, ilielezwa hali yake ilionyesha kutengemaa na kuweza kusafirishwa kwa matibabu zaidi. Hivyo basi, ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), uliagiza ndege ambayo ilifika Dodoma saa 10.30 jioni kwa ajili ya kumchukua mgonjwa ili kumpeleka Hospitali ya Rufaa Muhimbili kwa matibabu zaidi.

“Hata hivyo, baada ya mashauriano kati yetu, familia na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, wao walishauri ni vema mgonjwa akapelekwa Hospitali ya Aga Khan, Nairobi, Kenya.

“Kwa hiyo, ilipofika saa 4.30 usiku, ilifika ndege nyingine ya Kampuni ya Flying Doctors na kuondoka na mgonjwa jana saa sita usiku kuelekea Nairobi, Kenya.

Ndugai alisema katika safari hiyo, Lissu ameambatana na mkewe, Mbowe, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Msigwa, madaktari wawili kutoka Kampuni ya Flying Doctors na daktari bingwa mmoja wa upasuaji kutoka Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, ambaye ni kati ya waliomfanyia upasuaji kabla ya kusafirishwa.

Kwa mujibu wa Spika Ndugai, shambulizi hilo ni la kwanza nchini na kutokea mjini Dodoma tangu Bunge lilipohamia mkoani humo miaka kadhaa iliyopita.

Pamoja na hayo, Spika aliwataka wabunge wasiendelee kusambaza taarifa mbaya katika mitandao ya kijamii zikionyesha Serikali ilivyokataa kugharamia matibabu ya mbunge huyo kwenda Nairobi.

“Sisi hatukukataa kumtibu kama nilivyosema, bali tulitaka ahamishiwe Muhimbili na baadaye kama ingewezekana, asafirishwe kwenda India katika Hospitali ya Apollo kwa sababu ndiko Serikali inakopeleka wagonjwa wake.

“Lakini, baada ya familia na Mbowe kusema wanataka wamhamishie Nairobi, tukaona hatuna sababu za kukataa kwa sababu mara zote tulikuwa na mawasiliano mazuri kabisa.

“Hata Mheshimiwa Mbowe mwenyewe alisema siyo kwamba wana mashaka na umahiri na uwezo wa madaktari walioko Hospitali ya Dodoma au Muhimbili, bali alisema wangejisikia faraja kama mgonjwa angepelekwa Nairobi na ningeomba Watanzania walielewe hilo,” alisema Ndugai.

Wakati huo huo, wabunge walikubali kukatwa nusu ya posho yao ya kikao cha siku moja ambapo zilipatikana Sh milioni 43 kwa ajili ya kugharamia matibabu ya Lissu.

Kwa mujibu wa Spika, makato hayo yalikubaliwa baada ya Kamati ya Bunge ya Uongozi kukutana kwa dharura na wajumbe wa Tume ya Bunge.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles