25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

HUJUMA MCHANA KWEUPE

NORA DAMIAN Na RAMADHAN HASSAN-DAR/DODOMA


NI hujuma za wazi mchana kweupe. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Rais Dk. John Magufuli, kueleza kuwapo matumizi mabaya ya fedha ndani ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na kwenye taasisi za fedha kwa kuhusisha viongozi na wafanyakazi.

Hujuma hizo zilifichuliwa jana kwa nyakati tofauti na Rais Magufuli wakati wa uzinduzi wa nyumba 150 zilizojengwa na NHC katika eneo la Iyumbu na uzinduzi wa tawi la Benki ya CRDB mkoani Dodoma.

Rais Magufuli alisema licha ya kazi nzuri inayofanywa na NHC, lakini bado kuna dosari, hasa katika matumizi ya fedha.

“Mnafanya kazi nzuri, lakini matumizi yenu si mazuri, yako mengi ninayoyajua na tuhuma zipo.

“NHC mmeshakopa Sh bilioni 360, iko miradi inayoendelea vizuri, lakini kuna wakati matumizi ya fedha hayakuwa mazuri. Ndiyo maana tulizuia suala la kukopakopa kwa sababu baadaye mzigo huu utakuja kubebwa na Serikali.

“Serikali haitoi ‘guarantee’ mahali ambako bado kuna mashaka fedha yake inatumikaje.

“Asanteni sana kwa kulia mbele ya Watanzania na mimi nataka kuwaeleza kilio chenu sasa kiwafundishe namna ya kutumia vizuri fedha za Serikali, ni lazima mtu ujifunze kumeza kile kinachopita kwenye koo,” alisema Rais Magufuli.

Alilitaka shirika hilo kujitathmini kwa kuondoa dosari ndogondogo ilizonazo ili kwenda katika mlengo anaoutaka.

“Jengeni nyumba kila mahali, lakini angalieni matumizi yenu, nataka NHC itimize wajibu wake kwa manufaa ya Watanzania… mengine yote ni safi, tatizo ni matumizi ya fedha na maujanja ujanja fulani,” alisema.

 

TUHUMA KWA UONGOZI

Hujuma nyingine zilizotajwa na Rais Magufuli zinawahusu viongozi wa shirika hilo, akiwamo Mkurugenzi Nehemia Mchechu na Bodi ya Wakurugenzi.

“Visumu sumu ambavyo vinaleta mawazo vingi vipo, unakuwa na shirika la kujenga nyumba wakati wewe ni mkurugenzi na ni shirika lako.

“Umenunua viwanja kule na wewe unakwenda unanunua maeneo unayaandika kwa majina fulani, tukichunguza tunakuta vyako… mengine nimeyamezea kwa sababu ya kazi nzuri unayofanya.

“Hata katika majengo ya Kawe, pale kuna ‘share’ (hisa) ya 50/50 na mtu mwingine, mwenye hiyo ‘share’ ni nani… mimi nawajua.

“Mkurugenzi, mwenyekiti na waziri kakaeni mchambue mahali mlipokosea, mtakaporekebisha na mlete mapendekezo,” alisema Rais Magufuli.

Alimtaka Mchechu kuwa makini na watu anaofanya nao kazi.

“Ninafahamu kuna mgogoro, mnapigana vita humo humo, wako watu wanaotaka ukurugenzi wako na wanawatumia mpaka wajumbe wa bodi na wengine wanawatumia wanasiasa… wako wanaokupiga vita kwa wivu wao, lakini na wewe saa zingine matumizi yanakuwa ya ajabu,” alisema.

Rais Magufuli alishangazwa vikao vya bodi kufanyika Dubai wakati hapa nchini kuna maeneo ya kutosha.

“Bodi ilikuwa inakwenda kufanya vikao vyake Dubai, wamekosa maeneo ya kukaa Tanzania nzima?” alihoji Rais Magufuli.

 

AZIBANA HALMASHAURI

Rais Magufuli alizitaka halmashauri nchini kupunguza gharama za ardhi, hasa kwa miradi ya Serikali inayotekelezwa kwenye maeneo yao na ikibidi watoe bure.

“Ni kitu cha ajabu Serikali na Serikali kuuziana maeneo, ikibidi toeni bure kwa sababu mnajenga kwa ajili ya wafanyakazi na Watanzania masikini,” alisema.

Rais Magufuli aliagiza pia eneo la Iyumbu lililokuwa limetengwa kwa maziko ya viongozi ligawiwe kwa wananchi kwa sababu Serikali bado haijapata fedha za kulipa fidia.

Alitoa agizo hilo baada ya Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde (CCM), kumwomba aruhusu eneo hilo lenye ukubwa wa eka 129 litumiwe na wananchi hadi hapo Serikali itakapokuwa tayari kulipa fidia.

“Niliuliza marais wastaafu na hakuna aliyekuwa tayari kuzikwa Dodoma, sasa wakati tunasubiri sheria ibadilishwe, natamka ardhi irudishwe kwa wananchi na watakaotaka kuja kuichukua kama ni manispaa au shirika, muwalipe fidia wananchi.

“Mkitaka kulima anzeni hata kesho na pasitokee mtu wa kuja kuwatoa bila fidia,” alisema.

 

MKURUGENZI NHC

Awali Mkurugenzi wa NHC, Mchechu, alimwomba Rais Magufuli kibali cha kukopa Sh bilioni 232 kumalizia miradi ya ujenzi katika Jiji la Dar es Salaam.

Alifafanua kuwa fedha zinazohitajika katika miradi hiyo ni Sh bilioni 473, mikopo ni Sh bilioni 232 na faida itakayopatikana katika majengo hayo ni Sh bilioni 118.

“Tunaomba kibali cha kukopa fedha za kumalizia miradi yetu ya Dar es Salaam, hatuhitaji dhamana ya Serikali. Kila jengo tunalojenga ni biashara, hivyo ukitupatia kibali utatuwezesha tukimbie mbio na twende na kasi yako,” alisema Mchechu.

Mkurugenzi huyo alisema utendaji wa shirika hilo umekuwa ukiboreka kila mwaka na hivi sasa mapato yamefikia Sh bilioni 154 kwa mwaka………..

Kwa muendelezo wa habari hii jipatie nakala yako ya gazeti la MTANZANIA

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles