23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

TUUNGANE NA RAIS MAGUFULI KUKEMEA WANAOKAA UTUPU

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


HATUA ya Rais Dk. John Magufuli kukemea hadharani wasanii wanaocheza utupu
majukwaani na wanaporekodi video za muziki ni ya kupongezwa.
Ni suala linalopaswa kuungwa mkono na kila mwananchi anayependa
maendeleo ya jamii na nchi kwa ujumla.
Akihutubia katika mkutano wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi
juzi mjini Dodoma, Rais Magufuli alisema kila anapowasha televisheni
yake anashangaa kukutana na mabinti wakicheza utupu.
Alisema wakati mabinti wakicheza utupu, wanaume huwa wamevaa mavazi ya
staha na kusisitiza kwamba ni aibu kubwa kwa wazazi kuangalia mambo
hayo.
Pia aliitaka jamii kuamka na kuwakemea wale wanaofanya vitendo hivyo kwa kuwa
vinaashiria mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Tamko hilo la Rais Dk. Magufuli linapaswa kuungwa mkono na kila mtu
anayependa maadili mema kwa sababu suala hili
limekuwa kero kubwa katika jamii.
Unaweza kukaa sebuleni kwako na kuamua kufungulia televisheni ili
kutazama muziki lakini ukakutana na wasichana warembo waliovaa
nusu utupu huku wakinengua, ubaya unakuja pale ambapo unakuwa na watoto.
Ni aibu isiyoelezeka, vyombo vya habari navyo vinapaswa kujitathmini
katika hili, kwa sababu miziki mingi imekuwa ikipigwa mchana na
wanenguaji wake huwa wamevaa utupu.
Tunalalamika na kutupiana mpira kila siku juu ya mmomonyoko wa
maadili, kila mmoja akimtuhumu mwenzake kuwa ni chanzo.
Lakini tunasahau kuna mambo kama hayo ambayo huchangia kwa namna moja
au nyingine kuwaathiri watoto na hivyo kujikuta tukiwa na kizazi
kisichokuwa na maadili.
Dk. Magufuli anashauri: “Ifike mahali bila kujali vyama vyetu, tulinde
maadili yetu, ninyi kama wazazi, sifahamu kama enzi za akina Fatma
Karume au kina Maria Nyerere huo ndio ulikuwa mtindo, lakini nina
uhakika enzi zile haikuwa hivyo, lakini vyombo vyetu vya habari,
wasimamizi wa maadili haya wako wapi? Wizara inayosimamia haya wako
wapi je, TCRA wako wapi? Niwaombe ndugu zangu jumuiya ya wazazi
kuikosoa hata serikali katika kusimamia maadili ya Tanzania.”
Naamini kila mmoja wetu ana wajibu katika kusimamia suala hili,
vinginevyo jamii itazidi kuharibiwa na maadili yatazidi kuporomoka
kila siku.
Kwa kuwa Rais Magufuli ametoa rai hiyo ni vema kila mmoja kuhakikisha anasimama katika nafasi yake ili siku moja tujivunie kizazi chenye maadili mema
kinachojali utu, uzalengo, amani na upendo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles