25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Haikuwa bahati: Simba yatupwa nje Ligi ya Mabingwa ikionyesha kiwango bora

ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM

TIMU ya Simba imeaga michuano ya kimataifa baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani na UD Songo ya Msumbiji katika mchezo wa marudiano wa  mzunguko wa kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba imetupwa nje ya michuano hiyo kutokana na faida ya bao la ugenini walilopata UD Songo baada ya mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa mjini Beira, Msumbiji Agosti 11 kumalizika kwa suluhu.

Hata hivyo, wachezaji wa Simba wanatakiwa kujilaumu wenyewe kutokana na kushindwa kutumia nafasi nyingi walizotengeneza, hasa kipindi cha pili.

Wageni walionekana kuanza kwa kasi na kulisakama lango la Simba.

Dakika ya tatu, makosa ya kiungo wa Simba, Jonas Mkude nusura yaigharimu timu yake baada ya kuporwa mpira na Luis Miquissone ambaye alipiga mkwaju uliopanguliwa na kipa Aishi Manula na kuzaa kona ambayo hata hivyo haikuwa na madhara.

UD Songo iliendelea kupeleka mashambulizi lango la Simba, lakini Manula alisimama imara kuokoa hatari zote.

Dakika ya 13, Miquissone aliiandikia UD Songo bao la kuongoza kwa mkwaju wa adhabu ndogo nje kidogo ya eneo la hatari la Simba, uliokwenda moja kwa moja wavuni na kumwacha Manula akiwa hana la kufanya.

Bao hilo liliifanya UD Songo kuzidi kujiamini na kumiliki mpira, lakini hata hivyo washambualiaji wake, Pachoio King na Stelio Ernest walikosa maarifa ya kumalizia nafasi kadhaa walizopata.

Dakika ya 31, Clatous Chama alipoteza nafasi ya wazi ya kuiandikia timu yake bao baada ya kupokea pande safi kutoka kwa Deo Kanda na mkwaju wake kushindwa kulenga lango.

Miquissone ambaye ni nahodha wa UD Songo, alilimwa kadi ya njano dakika ya 32, baada ya kupingana na uamuzi wa refa.

Dakika ya 41, kocha wa Simba, Patrick Aussems alifanya mabadiliko katika kikosi chake kwa kumtoa Francis Kahata na kumwingiza Hassan Dilunga.

Mabadiliko hayo yaliimarisha Simba eneo la katikati ya uwanja, ingawa hayakuweza kubadili matokeo kwani hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinakamilika ilikuwa nyuma kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili Simba ilirudi kwa kishindo, ikionekana wazi kuwa na dhamira ya kusawazisha bao hilo na kusaka mabao zaidi, kuhakikisha wanasonga mbele katika michuano hiyo.

Dakika ya 47, Gadiel Michael alilimwa kadi ya njano baada ya kumchezea rafu Miquisson.

Dakika ya 49, UD Songo ilifanya mabadiliko ya kumtoa Frank Banda na kumwingiza Cremildo Ernesto.

Dakika 63, Simba ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Sharaf Eldin Shiboub na kumwingiza Miraji Athumani.

Mshambuliaji wa UD Songo, King alilimwa kadi ya njano dakika ya 64  baada ya kumchezea madhambi Manula.

Dakika ya 77, Aussems alifanya mabadiliko mengine akimtoa Gadiel na kumwingiza Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

Dakika ya 85, Simba ilipata penalti baada ya Miraji Athumani kukwatuliwa ndani ya eneo la hatari la UD Songo wakati akiwa katika harakati za kutaka kufunga.

Erasto Nyoni aliiandikia Simba bao kwa mkwaju huo wa penalti.

Dakika ya 87, mlinda mlango wa UD Songo, Leonel Pendula alilimwa kadi ya njano baada ya kuchelewesha muda.

Licha ya Simba kuchachamaa na kulisakama lango la UD Songo kipindi cha pili, lakini washambulaji wake, Chama, Kanda na Meddie Kagere walikosa maarifa ya kuukwamisha mpira wavuni.

Hata hivyo, UD Songo inabidi kumshukuru kipa wao kutokana na kazi nzito ya kupangua michomo hatari aliyoifanya.

Hadi dakika 90 za mtanange huo zinakamilika, timu hizo zilifungana bao 1-1.

Simba:  Aishi Manula, Shomari Kapombe, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Deo Kanda, Sharaf Shiboub, Meddie Kagere, Clatous Chama na Francis Kahata

UD Songo: Leonel Pendula, Antonio Chirinda, Hermenegildo Mutambe, Pascal Carlos, Infren Matola, Amade Momade, John Banda, Luis Miquissone, Pachoio King, Stelio Ernest na Frank Banda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles