28.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Eto’o awatabiria makubwa Samatta, Msuva  

NA BADI MCHOMOLO

NDOTO za wachezaji wengi Afrika kwa sasa ni kucheza soka la kulipwa Barani Ulaya, wapo ambao wamepata nafasi hiyo huku wengine wakiendelea kupambana kutafuta nafasi.

Kwa upande wa Tanzania, nahodha wa timu ya taifa (Taifa Stars), Mbwana Samatta tayari ameonesha kuwa kuna kitu anakitaka, kwa sasa anakipiga katika klabu ya Ligi Kuu nchini Ubelgiji, KRC Genk huku akitokea TP Mazembe ya DR Congo.

Tayari amepata nafasi ya kucheza soka la kulipwa Ulaya, lakini bado ana ndoto za kufanya hivyo kwa kucheza soka England, Hispania na Ujerumani.

Klabu mbalimbali nchini Uingereza kama vile Everton, West Ham, Bunley na Brighton zinadaiwa kuonesha nia ya kutaka kumsajili mchezaji huyo kutokana na kile anachokifanya ndani ya KRC Genk.

Kwa upande wa Tanzania kumekuwa na wachezaji wachache ambao wanaonesha nia ya kutaka kufika mbali kama vile Simon Msuva, Abdi Banda, Thomas Ulimwengu, Faridi Mussa, Shabani Chilunda na wengine.

Mshambuliaji wa zamani wa klabu ya Barcelona na timu ya taifa ya Cameroon, Samuel Eto’o anaamini Tanzania kuna wachezaji wazuri ambao wanaweza kucheza soka la kulipwa Ulaya, lakini wamejawa na woga.

Akizungumza na SPOTIKIKI mwishoni mwa wiki hii, Eto’o alisema, anaamini Tanzania kuna wachezaji wengi wenye ndoto za kucheza soka la kulipwa Ulaya, lakini wamejaa na woga.

“Wachezaji ninaowaona sasa Tanzania ni tofauti na kipindi cha nyumba, kuna Mbwana Samatta, Simon Msuva, wanaonekana kuwa na lengo la kufika mbali.

“Ninaamini wachezaji hao wanaweza kuibeba Taifa Stars katika michuano ya kuwania kufuzu Kombe la Afcon wakishirikiana vizuri na wachezaji wenzao. Tanzania ya sasa sio ya miaka 10 iliopita,” alisema Eto’o.

Mchezaji huyo aliongeza kwa kuwataka wachezaji mbalimbali barani Afrika kujitosa moja kwa moja kwa ajili ya kutimiza ndoto zao za kufika mbali na wapunguze woga.

“Kama wataamua kujituma na kujitoa kwa ajili ya maisha yao wanaweza kufika mbali, wanaweza kubadilisha maisha yao kwa muda mfupi,” alisema.

Mchezaji huyo aliweka historia ya kuwa mchezaji namba moja duniani kwa kulipwa fedha nyingi mwaka 2011 mara baada ya kujiunga na klabu ya Anzhi Makhachkala ya nchini Urusi.

Eto’o aliongeza kwa kusema wachezaji wengi Afrika wanashindwa kufika mbali kutokana na hali ya hewa, Academy, afya, chakula wanacho kula na mambo mengine madogo madogo.

“Kuna baadhi ya vitu ambavyo vinawafanya wachezaji wengi Afrika kushindwa kufika mbali kutokana na mazingira waliyotokea.

“Mchezaji anaweza kuonekana kuwa na uwezo mkubwa, lakini akashindwa kufika mbali kutokana na afya yake, mpangilio mbovu wa chakula na kushindwa kuendana na hali ya hewa ya huko Ulaya pale wanapopata nafasi ya kwenda kufanya majaribio.

“Kitu kikubwa ambacho kinaweza kuwasaidia soka la Afrika ni pamoja na kuwa na shule nyingi za soka kwa vijana wadogo, ili kuja kuwa na wachezaji wazuri walianzia soka utotoni,” aliongeza Eto,o.

Mchezaji huyo aliongeza kwa kusema, wachezaji wasiogope masuala ya ubaguzi wa rangi, kikubwa waangalie nini wanachokitafuta.

“Ubaguzi upo sana katika soka, nilikuwa napata tabu sana katika klabu mbalimbali nilizopitia, lakini kila siku nilikuwa napambana kuhakikisha natimiza malengo yangu, nashukuru niliweza kufanya hivyo bila ya kujali ubaguzi,” aliongeza.

Wiki iliopita mchezaji huyo alikuwa nchini Tanzania kwa ajili ya uzinduzi wa mradi wa uwanja wa mpira aina ya 5-A Side Soccer, maeneo ya Oysterbay.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles