24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

‘Daktari mmoja huona wagonjwa 22,000 kwa mwaka’

TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM

RAIS wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Elisha Osati, amesema kwa sasa kuna idadi kubwa ya wahitimu wa masomo ya udaktari ambao hawana ajira, huku daktari mmoja aliyepo kwenye ajira huona wagonjwa 22,000 kwa mwaka.

Amesema hilo ni tofauti na mwongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ambao unataka daktari mmoja aone wagonjwa 10,000 kwa mwaka.

Hayo aliyasema jana Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa utoaji mikopo kwa wataalamu wa sekta ya afya wakiwamo madaktari na wafamasia ambao wametengewa Sh bilioni 5 na Benki ya NMB.

Dk. Osati alisema hadi sasa kuna madaktari wanaomaliza mafunzo kazini 1,470 na wengine 1,500 wanaingia katika mafunzo hayo, lakini hakuna ajira za madaktari zilizotangazwa na Serikali.

“Mikopo hii itakwenda kutatua changamoto ya ajira kwa watumishi wa sekta ya afya, wakiwamo madaktari ambao sasa wataweza kukopa na kuanzisha huduma za hospitali,” alisema.

 Dk. Osati aliwataka watumishi wa afya kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwa awali walikuwa hawakopesheki kutokana na kukosa dhamana.

“Tusiwe watu wa kulalamika kila mara kudai ajira tuwe sehemu ya suluhisho na kwa kupitia mikopo hii tutaweza kujiajiri na kuajiri wenzetu,” alisema.

Aliomba benki hiyo kuhakikisha riba wanazoweka katika mikopo hiyo inakuwa nafuu ili kurahisisha ulipaji. 

Kaimu Mkurugenzi wa NMB, Filbert Mponzi, alisema lengo ni kutoa mikopo ya gharama nafuu kwa hospitali binafsi, vituo vya afya na zahanati.

Mponzi alisema huduma hiyo ya mikopo ni matokeo ya ushirikiano kati ya NMB na Shirika la Medical Credit Fund (MCF).

Alisena NMB itatoa mikopo kuanzia Sh milioni 2 hadi bilioni 5 na MCF inatoa dhamana ya asilimia 50 katika mikopo yote.

“Wanufaika wa mkopo wa afya ni hospitali binafsi, vituo vya afya na zahanati, maduka ya dawa na wasambazaji dawa na vifaa tiba ili kuwezesha, kuiinua na kuboresha biashara za huduma za afya nchini,” alisema Mponzi.

Alisema ushirikiano huo na MCF una lengo la  kuijengea uwezo sekta ya afya ili waweze kutoa huduma hiyo kwa ufanisi na kuchangia kuongeza upatikanaji wa huduma nafuu za afya na kujenga mifumo endelevu kutokana na upatikanaji wa mitaji unakuwa rahisi zaidi.

“Huduma hii itawawezesha watoa huduma ya afya kupata fedha pamoja na kupata utaalamu wa kiufundi, ambao utasaidia  kutambua wauzaji na vifaa vya matibabu bora pamoja na upatikanaji wa vifaa vya tiba kwa ajili ya uboreshaji wa huduma zao,” alisema Mponzi.

Awali akizungumza katika uzinduzi huo, Mwakilishi Mkazi wa MCF Tanzania, Dk. Heri Marwa alisema kuanza utekelezaji wa huduma hiyo ni muhimu katika kutimiza malengo ya MCF ya kuhakikisha  Watanzania wengi wanapata huduma nafuu za afya na tiba.

“Upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya uwekezaji ni changamoto kubwa katika nchi nyingi za Kiafrika na inazuia utoaji huduma nafuu za afya, hususan tukiangalia mifumo endelevu ya afya,” alisema Dk. Marwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles