24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

CUF Lipumba: Mkutano mkuu palepale

Na ASHA BANI

-DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Bara, Joran Bashange, kutoa matamshi makali ya kupinga kufanyika kwa  mkutano mkuu wa chama ulioandaliwa na viongozi upande wa Profesa Ibrahimu Lipumba, upande huo umedai mkutano upo palepale.

Juzi Bashange akizungumza na vyombo vya habari, alidai kuwa upande wa mwenyekiti anayetambuliwa Msajili wa vyama vya siasa, Profesa Lipumba unadaiwa kutaka kumwengua Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kupitia mkutano aliouita kuwa si wa halali kutokana na kuwapo zuio la mahakama.

Kutokana na maandalizi hayo ya mkutano, Bashange alitoa onyo kwa wajumbe kutoka eneo lolote Tanzania kutohudhuria na kwamba wanachama wapo tayari kukilinda chama hicho.

Hata hivyo, Msemaji wa upande wa Profesa Lipumba, Abdul Kambaya, alisema mkutano huo upo pale pale na kwamba hakuna zuio lolote la mahakama.

“Mkutano upo pale pale utafanyika Machi 14, mwaka huu katika Hoteli ya Lekam na waandishi tutawajulisha hakuna zuio lolote,” alieleza Kambaya.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema hilo ni suala la msajili lakini kama barua ikifika mezani kwao wakiomba ulinzi, itajadiliwa pia.

“Kwa sasa bado hatujapokea barua kutoka upande wowote, lakini kama imefika tutajadili, ila ni suala la msajili ndio anahusika zaidi siwezi kumuingilia hapo,” alisema Mambosasa.

Naye Naibu Msajili wa vyama vya siasa nchini, Sisty  Nyahoza, alisema hawezi kuzungumza kwa kuwa alikuwa safarini Dodoma hajui kama mwaliko wamepelekewa au la.

“Nimesema siwezi kuzungumza kwa kuwa nilikuwa safarini Dodoma, lakini kwa kutaka kufahamu zaidi fika ofisini kesho utajua kila kitu,” alieleza Nyahoza. 

Kwa muda mrefu CUF upande wa Maalim Seif, umekuwa ukimtuhumu Msajili wa vyama vya siasa kwamba amekuwa akiwabeba akina Profesa Lipumba kwa kuwapatia fedha za ruzuku bila kujali mgogoro uliopo ndani ya chama hicho.

Mgogoro huo wa CUF umesababisha kuwapo kesi kadhaa mahakamani, baadhi zikipinga Profesa Lipumba kuendelea kuwa mwenyekiti kutokana na awali kujiuzulu nafasi hiyo kabla ya kuomba kurejea tena.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles