27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Kauli za Lowassa zaibua mjadala

Na ANDREW MSECHU – DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya aliyekuwa mgombea urais wa Ukawa kupitia Chadema kisha kurejea CCM, Edward Lowassa, kusema kuwa asiulizwe kwanini ‘amerudi nyumbani’ na kuwataka watu milioni sita waliompigia kura kuzielekeza kwa Rais Dk. John Magufuli, mjadala mpya umeibuka.

Katika mkutano wake wa juzi wakati akipokewa rasmi  mjini Monduli kujiunga na CCM, alisema hatua hiyo ya kurudi nyumbani, jibu lake ni rahisi, kwamba amerudi nyumbani, basi hajarudi kwa jirani wala kwa mtu, amerudi nyumbani kwake.

Kuhusu uongozi wa Chadema, Lowassa alisema anawashukuru sana, hana la ziada ila asiwekewe maneno mdomoni, ila anawashukuru sana.

Akizungumzia kauli hizo jana, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, alisema pamoja na yote yanayoendelea, kwa kuwa Lowassa ameshaondoka na amewashukuru viongozi wa Chadema, kwa sasa hakuna haja ya kuendeleza mjadala wowote.

“Kimsingi ni kwamba hawezi kuhamisha mwanachama yeyote wa Chadema. Lakini ameshaondoka na ametushukuru, kwa hiyo na sisi tunamshukuru, tunasonga mbele. Tusingependa kuendeleza mjadala wowote kwa sasa,” alisema.

Kwa upande wake Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Shaka Hamdu Shaka, aliwataka wapinzani wa chama hicho kutohoji Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa kurudi ndani ya chama hicho tawala.

Alisema hakuna asiyejua kuwa mwanachama huyo amekulia ndani ya chama hicho na kutoka kwake kwenda upinzani ilikuwa ni ajali mbaya ya kisiasa.

Alisema viongozi Chadema alipotoka walimlinganisha sawa na tembo kwani CCM inamtambua mwanasiasa huyo kati ya mibuyu minene inayotikisa katika uwanja wa siasa za Afrika Mashariki.

“Ni kweli huwezi kuushangaa mshale ambao chanzo chake ni mti na unaporudi porini kwani huko ndiko mahali ulikokuwa kabla ya kukatwa na kufanywa upinde ulikowekwa na kipande kidogo cha chuma na kuwa silaha. 

“Kama Chadema walimfananisha Lowasa na tembo wa siasa, kwetu ni hazina ya siasa kwa maendeleo yake ambayo haifilisiki na kurudi kwake hakupaswi kuhojiwa na mtu yeyote, aidha kutoka nje au miongoni mwa wana-CCM,” alisema Shaka.

Aidha, katibu huyo aliwataka wapinzani kuelewa na kutafakari msingi wa wanachama na viongozi wengi kurudi ndani ya CCM wakati huu ambapo chama kimekuwa na taswira pana ya kuleta mageuzi ya kiuchumi na utekekezaji endelevu wa dhana ya maendeleo ya pamoja. 

Alisema mtu kuendelea kupinga mambo yanayofanywa na utawala wa Rais Dk. Magufuli kunahitaji akili za kijuha na iwapo kweli akili zako zinafanya kazi kwa viwango.

Alipoulizwa ni kwa sababu ipi yeye alikuwa miongoni mwa viongozi waliokuwa wakimshambulia kwa maneno makali wakati akiwa upinzani, Shaka alisema watu hupopoa mti wenye mabungo ili wapate faida na hawezi kuangua matunda  ambayo huwezi kuyauza popote. 

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha (RUCU), Profesa Gaudence Mpangala, alisema si kweli kwamba Lowassa alikuwa na kura milioni sita alizoingia nazo katika upinzani, bali alichangia kwa kiasi kidogo kutoka kwa watu waliokuwa wakimpenda.

Alisema kabla ya uchaguzi wa 2015, tayari upinzani ulishapata nguvu sana kiasi kwamba ulikuwa tishio la kuiangusha CCM, hasa kutokana na CCM kuelelewa na kashfa za rushwa na ufisadi, hivyo Lowassa aliingia akikuta idadi kubwa ya kura za upinzani iko tayari.

Alieleza kuwa mambo yaliyoufanya upinzani upate nguvu na kuongeza idadi ya kura ni hatua ya Bunge kukataa kupitisha Rasimu ya Katiba ya Warioba ambayo wananchi walitoa maoni yao na kashfa za rushwa zilizokuwa zikiwakabili viongozi wa CCM.

Alisema historia inaonesha kuwa tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi, katika hatua ya awali CCM ilijivunia mfumo wa chama uliojengwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, kukifanya kuwa chama cha walio wengi, yaani wakulima na wafanyakazi, hivyo kushinda katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi.

Profesa Mpangala alisema suala la Lowassa kurejea CCM halikumshtua kwa kuwa alilitambua tangu awali kwamba, lazima lingetokea ila suala ilikuwa kwamba itakuwa lini.

“Ni wazi kwamba alihamia haraka upinzani baada tu ya CCM kukata jina lake katika waliokuwa wakiomba ridhaa ya kuteuliwa kuwa wagombea kupitia chama. Yeye si mtu wa upinzani na isingekuwa rahisi kwake kubeba itikadi ya upinzani, hakujiandaa kubeba mapambano ya upinzani ambayo ni magumu,” alisema.

Kwa upande wake, Dk. Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema kimsingi katika uchaguzi watu humfuata mtu wanayempenda kuliko wanavyofuata vyama, kwa hiyo upo uwezekano kuwa watu wengi walipigia kura upinzani kwa sababu ya Lowassa.

Alisema hatua ya upinzani kumpokea Lowassa katika Uchaguzi Mkuu uliopita inaweza kuwa ujumbe tosha kwamba unatakiwa kujenga vyama kuwa taasisi imara na kujenga watu wanaoweza kuaminika ndani ya vyama hivyo, kwa ajili ya kuwania nafasi ikiwemo ya urais.

“Huu ni ujumbe tosha kwa upinzani hasa Chadema, kuwa suala la kupokea mgombea ni sawa, kwa kuwa wapigakura pia huangalia mtu wanayempenda na si chama, kwa hiyo hawawezi kukwepa ukweli kwamba kura milioni sita ni za Lowassa kwa sababu alikuwa anapendwa,” alisema.

Aliongeza kuwa hatua ya Lowassa ambaye walimchukua kama lulu na tunu yao, kuondoka Chadema na kurejea CCM ina athari kubwa kwa chama hicho kwa kuwa anaondoka na kura zake, kwa hiyo wanachotakiwa kufanya kwa sasa ni kijenga chama kiwe taasisi imara ili kiweze kusimama bila kutegemea watu.

Alieleza kuwa kwa hatua hiyo ya Lowassa ambaye alikuwa tegemeo la mwisho, kuondoka Chadema

 imewaacha viongozi wa chama hicho wakiwa hawajui ni nani wanayeweza kumsimamisha katika uchaguzi ujao kwa kuwa hawana watu waliowaandaa, hivyo wanatakiwa kujifunza na kuandaa watu wanaoweza kuaminika.

Kutoka mitandaoni

Katika mtandao wa Twitter, muda mfupi badaa ya taarifa ya mkutano wa Lowassa mjini Arusha, baadhi ya wachangiaji waliendelea kuzungumzia hatua hiyo wakieleza mitazamo na hisia zao.

Aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya Awamu ya Nne, Hamis Kagasheki, aliandika akisema: “Aliwahi kusema kiongozi mmoja: Wakati mwingine si watu wanaobadilika bali huwa ni kubadilika kwa mazingira au vipaumbele.”

Mwanaharakati Maria Sarungi pia aliandika: “Ili kupata mabadiliko chanya na endelevu, ni muhimu kuleta mabadiliko kwa kutumia ufahamu, hatua kwa hatua na kwa uthabiti. Mabadiliko yanayoletwa kwa nguvu, kulazimisha hata iwe yenye kusudio njema huibua upinzani wa nguvu na hata ghasia.” 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles