24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Corona yang’oa vigogo Maabara Kuu

Na ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ameagiza kusimamishwa kazi kwa Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, Dk. Nyambura Moremi na Meneja Udhibiti na Ubora wa maabara hiyo, Jacob Lusekelo ili kupisha uchunguzi kuhusu upimaji wa sampuli za virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.

Ummy amechukua hatua hiyo jana na taarifa kutolewa kwa umma ikiwa ni siku moja baada ya hotuba ya Rais Dk. John Magufuli ambaye aliagiza hatua zichukuliwe ili kubaini tatizo linalosababisha maabara hiyo kutoa majibu yasiyo sahihi kwa sampuli za vipimo vya corona.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo wakati akimwapisha Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Mwigulu Nchemba ambapo alibainisha changamoto za utendaji wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii.

Katika taarifa hiyo ya wizara iliyotolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Idara Kuu-Afya, Catherine Sungura, Waziri Ummy alieleza kuwa amemwelekeza Katiba Mkuu (Afya) kuwasimamisha kazi mara moja Dk. Moremi na Lusekelo ili kupisha uchunguzi. 

“Waziri Ummy pia ameunda kamati ya wataalamu wabobezi tisa kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa mwenendo wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii ikiwemo mfumo mzima wa ukusanyaji na upimaji wa sampuli za Covid-19,” alieleza katika taarifa yake. 

Ummy alisema kamati hiyo itaongozwa na Profesa Eligius Lyarnuya kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) na wajumbe watakuwa ni Profesa Said Aboud – Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili (Muhas), Profesa Gabriel Shirima – Chuo Kikuu cha Nelson Mandela (NMIST), Profesa Steven Mshana – Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Buganda (Cuhas) na Profesa Rudovick Kazwala – Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua).

Alisema wajumbe wengine ni Dk. Thomas Marandu – Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),  Dk. Mabula Kasubi – Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Danstan Hipolite – Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Viola Msangi – Mtaalamu wa maabara mstaafu na Jaffer Sufi – Mtaalamu wa maabara mstaafu. 

Ummy alisema kamati hiyo itaanza kazi mara moja na itatakiwa kuwasilisha taarifa yao kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kabla ya Mei 13.

Alisema sambamba na uchunguzi wa kamati hii, shughuli za upimaji wa sampuli katika maabara hiyo zinaendelea. 

Hatua hiyo ya Ummy ni utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli ambaye baada ya kumwapisha Waziri Nchemba juzi, alisema wakati Serikali ikiendelea kupambana na maambukizi ya virusi hivyo, tayari wamebaini hitilafu katika mfumo wa upimaji katika Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, hivyo hatua zaidi zinatakiwa kuchukuliwa ili kuwa na uhakika wa matokeo ya vipimo vya corona katika maabara hiyo.

“Pale National Referral Laboratory inayohusika kupima corona kuna controversial (utata) nyingi za ajabu, hasa baada ya kufuatilia na kutaka kujua uhakika wa vipimo.

“Katika kufuatilia uhakika wa vipimo, Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Afya, Profesa Mabele Mchembe alikwenda na kuchukua sampuli za mbuzi, kondoo, papai, oil ya gari na vitu vingine na kupeleka maabara bila wahusika kujua.

“Sampuli ya oil ilipewa jina la Jabir Hamza (30) ilileta majibu negative (haina maambukizi), sampuli ya fenesi iliyopewa jina la Sarah Samwel (45) matokeo yalikuwa unconclusive (haikuonyesha majibu), sampuli ya papai iliyopewa jina la Elizabeth Anne (26) ilileta majibu positive (imeambukizwa).

“Pia sampuli ya ndege kware positive (imeambukizwa), sungura undeterminant (haikubainika), mbuzi akawa positive (imeambukizwa), kondoo akawa negative (haijaambukizwa). 

“Sasa tukishaona umepeleka sampuli ukamwambia huyu ni binadamu ikawa positive (imeambukizwa) basi ile jamii yote inatakiwa kuwekwa isolation, kwa hiyo yale mapapai, kware, mbuzi wote walitakiwa watengwe,” alisema Rais Magufuli.

Pamoja na hili, mkuu huyo wa nchi alisema alitoa nafasi pia kwa wanasayansi wengine kufanya uchunguzi huo kwa kuchukua sampuli mbalimbali na watakuja kubaini kwamba kile anachokizungumza kina ukweli.

“Kwa hiyo narudia kuwaeleza Watanzania, bado tuko kwenye elementary stage (hatua za awali), tusitaharuki na watu waendelee kuchapa kazi, tusitishane, na wanasiasa waache kuitumia hii kama agenda kwa sababu haitawasaidia,” alisema Rais Magufuli. 

Alieleza kuwa uzoefu unaonyesha ni kawaida kuwa kila gonjwa jipya linapotokea watu hupata wasiwasi kama ilivyotokea kwa ugonjwa wa Ukimwi, lakini hata watu wanaobainika kuambukizwa virusi vya Ukimwi wanakwenda kuposa na kuoa.

Alisema wakati wa ugonjwa wa surua ilikuwa marufuku hata kwenda kutembelea eneo hilo na imekuwa hivyo hivyo kwa magonjwa kama ukoma na kifua kikuu (TB), ebola, zika, hofu zimekuwa zikijengeka, lakini matatizo hayo hatimaye yalipatiwa ufumbuzi.

Alimwagiza Waziri Dk. Nchemba akashirikiane na Wizara ya Afya wakaangalie upya kwenye Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii kuna nini ndani na kama kuna kitu kama jinai ishugulikiwe kisheria na kama kuna watu walijihusisha kwenye jinai kwa kutumia hivyo vifaa, basi sheria ichukue mkondo wake, lakini pia kama vifaa vina matatizo ya kiufundi lazima pia viangaliwe.

“Nilishasema tusikubali kila msaada tukafikiri ni kwa faida ya nchi hii. Mnaweza mkaambiwa kuwa wote mna corona na ndiyo maana utakuta wengi walioambiwa kuwa wana corona mpaka sasa bado ni wazima,” alisema Rais Magufuli.

Alimpongeza Katibu Mkuu Mpya wa Wizara ya Afya, Profesa Mchembe kwa hilo la kufanyia vipimo sampuli za mapapai na mafenesi kwa kuwa katika hilo wamekwenda na mabadiliko na kumtaka aendelee hivyo hivyo pamoja na watendaji wake walioko katika Wizara ya Afya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles