24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

BENKI YA FNB  YAFUNGUA TAWI JIPYA ARUSHA

Na ESTHER LEMA (OUT)-ARUSHA


FIRST National Bank (FNB) Tanzania imeendelea kupanua wigo wake kitaifa kwa kufungua tawi jipya Jijini Arusha kwa lengo la kuhudumia ongezeko la idadi ya wateja katika mkoa huo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi, Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Dave Aitken, alisema uzinduzi  wa tawi  hilo umelenga kukidhi ongezeko kubwa la wateja na mahitaji ya huduma za benki na fedha katika Kanda ya Kaskazini.

“Uzinduzi wa tawi la Arusha ni sehemu ya mkakati wa uwekezaji endelevu uliolenga kuhakikisha maeneo mengi ya nchi yanapata huduma bora za fedha. Pia ukuaji wa haraka wa Mkoa wa Arusha ambao una mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Tanzania,” alisema.

Aitken alisema tawi la Arusha ni la 10 miongoni mwa mtandao wa matawi ya FNB Tanzania, ikiwa ni sehemu ya mpango mkakati wa kupanua mitandao ya matawi kwa kusudi la kuyafikia maeneo mengi ya nchi.

 “First National Bank (FNB), daima tunafikiria njia ambazo zinaweza kutoa huduma za kibenki kwa urahisi kwa wateja wetu. Tawi letu la Arusha litasaidia kuwapatia huduma zote za kibenki wananchi wa Mkoa wa Arusha na wanaoishi maeneo jirani,” alisema Aitken.

Akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi rasmi wa tawi hilo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alisema Arusha ina uwezo wa ukuaji katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kudhihirisha kuwa jiji hilo linakua kwa kasi.

 “Tunakaribisha uwepo wa FNB Tanzania Arusha na tunatazamia kuwasaidia kuimarisha huduma zenu hapa na mikoa mingine,” alisema.

Aliongeza kuwa, pamoja na utajiri mkubwa wa maliasili na utalii, Mkoa wa Arusha umechangia sana katika kukuza uchumi wa Tanzania kupitia sekta nyingine za uzalishaji mali na biashara.

 “Arusha ina fursa na hazina kubwa ya rasilimali, jambo ambalo limechangia ukuaji wa haraka wa biashara katika sekta zote muhimu za kiuchumi. Ni matumaini yetu uwepo wa FNB katika mji huu utachangia katika kuleta maendeleo ya biashara kupitia ubunifu wa huduma za kibenki,” alisema Kijaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles