ZAINAB IDDY, DAR ES SALAAM
KOCHA msaidizi wa Azam, Idd Nassoro ‘Cheche’, amesema hawajakata tamaa katika harakati ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza na BINGWA jana, Cheche alisema licha ya Simba kuonekana kutangulia mguu mmoja katika mbio za kutetea ubingwa wao wanaendelea na mapambano ya kuwania taji hilo.
Cheche alisema pamoja na kuzidiwa alama nyingi na Simba walio juu yao katika msimamo lakini wanaamini wana nafasi ya kutwaa ubingwa.
“Simba wmaetuzidi alama 14 ambazo ni sawa kama na michezo mitano, hatujakata tama tunanafasi ya kutwaa ubingwa wa msimu huu kwa sababu waliojuu yetu wanaweza kupoteza mechi.
“Ligi ni ngumu kila mtu anapambana sitaki kuamini kuwa mechi walizobaki nazo Simba watashinda zote, kwa sababu timu nyingi wanazokutana nazo zipo katika hatari ya kushuka daraja najua haziwezi kukubali kupoteza kirahisi na hiyo ndio nafasi yetu ya kuchukua kombe.”
Azam ambayo ipo nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na pointi 45, baada ya kucheza mechi 23 sawa na Simba, lakini wakizidiwa kwa alama 14 baada ya Wekundu wa Msimbazi kujikusanyia 62.