24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Algeria yakumbwa na mlipuko wa virusi vya corona

Algiers, Algeria

WAZIRI wa Afya nchini Algeria amethibitisha nchi hiyo imepokea kisa cha kwanza cha virusi vya corona kupitia taarifa iliyotolewa na televisheni inayomilikuwa na serikali ya ENTV.

Waziri  huyo,  Abdel Rahman Ben Bouzid alisema mgonjwa huyo ni mwanaume raia wa Italia aliyewasili nchini humo Februari 17, kulingana na shirika la habari la Reuters.

Mgonjwa huyo ametengwa kwa sasa.

Algeria imekuwa nchi ya pili Afrika kuthibitisha kupata mgonjwa wa virusi vya Corona.

Misri ilikuwa ya kwanza kuthibitisha kupatika kwa kisa cha virusi vya Corona lakini baadae ikatangaza kwamba mgonjwa huyo hana tena maambukizi na anaendelea kupata nafuu.

Kutokana na kasi ya maambukizi hayo Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema dunia lazima ijiandae kwa janga.

Wakati huo huo, Naibu Waziri wa afya na mbunge mmoja nchini Iran wamethibitishwa kupata virusi vipya vya Corona, wakati nchi hiyo inapambana kukabiliana na virusi hivyo ambavyo vimesababisha vifo vya watu 15.

Watu wengi zaidi wamefariki nchini Iran kwasababu ya virusi hivyo kuliko nchi nyingine yoyote mbali na China.

Nchi hizo mbili zina uhusiano mkubwa wa kibiashara.

Hadi sasa Iran imeripoti visa 95 vya virusi vya Corona nchini Iran lakini idadi kamili inadhaniwa kuwa juu zaidi.

Nchi hiyo ni moja ya zile ambazo zimezua wasiwasi mkubwa kwamba virusi vya Corona huenda vikawa janga.

Naibu waziri, Iraj Harirchi, Jumatatu wiki hii alikanusha madai ya kwamba nchi hiyo inajaribu kuficha ukweli kuhusu mlipuko wa virusi hivyo.

Mkurugenzi wa Shirika la Afya Dunia (WHO) amesema kwamba kuongezeka ghafla kwa visa hivyo kwa nchi ambazo ziko nje ya China ni jambo la kutia wasiwasi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo, amesema, nchi yake ilikuwa na hofu kuwa Iran huenda imeficha taarifa muhimu kuhusiana na mlipuko wa ugonjwa huo na kusihi nchi zote kusema ukweli kuhusu virusi vya Corona.

Raia wa Kigeni waliopo China wakiwemo kutoka Afrika wamekua wakielezea hofu yao juu ya virusi vya Corona, mmojawao akiwa ni Mtanzania Dk. Khamis Hassan Bakari ambaye yupo jijini Wuhan ambako ni kitovu cha virusi hivyo.

Nchi zingine ambazo kwa sasa zimekumbwa na mlipuko wa virusi vya Corona kwa kiwango kikubwa ni Korea Kusini na Italia ambapo visa hivyo vimekuwa vikiongezeka katika siku za hivi karibuni.

MGONJWA WA UJERUMANI

Wizara ya afya ya jimbo la North Rhine Wesphalia nchini Ujerumani ilisema jana kwamba mtu aliyeambukizwa virusi vya Corona yuko katika hali mbaya na amepelekwa kwenye hospitali ya madaktari bingwa iliyoko kwenye mji wa Duesseldorf. 

Kulingana na wizara hiyo, mtu huyo anayetokea mji wa Erkelenz karibu na mpaka wa Uholanzi kwa mara ya kwanza alilazwa siku ya Jumatatu akiwa na homa kali ya mapafu. 

Lakini baadae aligundulika kuambukizwa virusi hivyo na kutengwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kabla ya kupelekwa Duesseldorf. 

Mke wake pia ametengwa kutokana na wasiwasi kwamba ameambukizwa virusi hivyo baada ya kuanza kuonyesha dalili. 

Tayari watu 80,000 wameambukizwa virusi hivyo kote duniani, huku Ujerumani ikiwa ni wagonjwa 17, idadi hii ikiwa ni kulingana na WHO. . 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles