25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Mangula aonya makada wanaojipitisha majimboni

Nathaniel Limu -Manyoni 

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula, ametoa onyo kwamba ikibainika mwanachama anajipitisha pitisha kufanya kampeni za chini chini kabla ya wakati wake, kamati yote ya siasa ya ubalozi husika, itachukuliwa hatua stahiki.

Alisema adhabu zitakazochukuliwa, zitasababisha mhusika kukosa sifa za kushiriki Uchaguzi Mkuu mwaka huu.

Alitoa onyo hilo wakati akizungumza na  viongozi wa ngazi mbalimbali na baadhi ya wana CCM wa Wilaya ya Manyoni juzi.

Mangula alisema kipindi hiki hadi Juni 30, , nafasi za udiwani na ubunge bado zina wenyewe, hivyo kampeni za aina yoyote haziruhusiwi.

“Ikitokea mwanaCCM anakiuka sheria, kanuni na taratibu na kuanza kujipitisha pitisha anafanya kampeni, atakuwa anakwenda kinyume na sheria. Kamati ya siasa ya ubalozi husika, haichukui hatua yoyote, itaadhibiwa.

 “Adhabu zitakazochukuliwa ni onyo miezi sita. Adhabu nyingine ni onyo kali litakalodumu kwa miezi 18, adhabu ya tatu, ni karipio. Adhabu zote hizi zitasababisha mhusika kutokujishughulisha na siasa. Adhabu hizo zitatolewa kwa kila mjumbe wa kamati husika,” alisema Mangula.

Alisema adhabu hizo zitaangukia kwenye kipindi chote cha kuchukua na kurejesha fomu kuomba nafasi ya udiwani na ubunge.

Katika hatua nyingine, Mangula aliagiza wanaCCM wahakikishe wanashikamana  pamoja kipindi hiki cha kuelekea kufanyika Uchaguzi Mkuu.

“Kama zipo tofauti kipindi hiki tuzifute na tuhakikishe wote tunaimba wimbo mmoja. Hiki ni kipindi cha kupanga mikakati ya kukiimarisha chama chetu, kwa hiyo migongano kwa sasa izikwe kwa manufaa ya chama. 

“Kila wanaCCM tunapokutana, agenda yetu ihusu maandalizi ya Uchaguzi Mkuu. Tuhamasishane, ili kila mwanachama asikose kushiriki uchaguzi ujao,” alisema Mangula.

Aliwataka wahakikishe vitendo vya rushwa ya aina yoyote havitokei. Wakibaini  vinatendeka watoe taarifa mapema kwenye mamlaka husika na Takukuru ili hatua ziweze kuchukuliwa mapema.

Mlezi wa chama hicho Mkoa wa Singida, Munde Tambue alitumia fursa hiyo kumpongeza Mangula kwa usimamizi wake mzuri wa kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa zinafuatwa kikamilifu.

Kabla ya kufanya mikutano ya ndani na viongozi wa CCM Wilaya ya Manyoni, Mangula alitembelea shamba la kimkakati la korosho la ekari 12,000 katika Kijiji cha Mesigati.

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Manyoni, Charles Edward Fussi alitumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru Rais Dk. John Magufuli kwa kuwapatia pikipiki nne kwa usimamizi na ufuatiliaji wa mradi wa kilimo cha korosho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles