Imechapishwa: Mon, Sep 11th, 2017

ALBINO WAILILIA SERIKALI MAFUTA YA NGOZI

Na RAMADHAN HASSAN-MPWAPWA

SERIKALI kupitia Wizara ya  Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imeombwa kuboresha huduma za kliniki na upatikanaji wa mafuta ya kulainisha ngozi kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) wanaoishi vijijini.

Ombi hilo limetolewa jana wilayani hapa na Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) Mkoa wa Dodoma, Omary Lubuva, alipokuwa akiutambulisha mradi wa utetezi kwa watu wenye ulemavu katika kuongeza ushiriki kwenye michakato ya Serikali za ngazi za mitaa wilayani Mpwapwa.

Mradi huo umefadhiliwa na The Foundation Civil Society kwa kushirikiana na SHIVYAWATA Mkoa wa Dodoma.

Lubuva alisema watu wenye ulemavu wa ngozi vijijini hawana kliniki za kuangaliwa afya zao, ikiwa ni pamoja na madawa yao, hivyo wanapohitaji kupata huduma hizo hulazimika kusafiri umbali mrefu.

Kutokana na hali hiyo, Lubuva anaiomba wizara hiyo kujenga vituo vya afya katika maeneo ya vijijini na kuhakikisha mafuta kwa walemavu wa ngozi yanapatikana kwa urahisi.

Naye Seif Hatibu, mkazi wa Kijiji cha Chaludewa, akizungumza kwa niaba ya watu wenye ulemavu wa ngozi, alisema upatikanaji wa huduma zote kwa walemavu imekuwa ni changamoto kubwa kwao.

“Upatikanaji wa huduma hiyo kwa sasa kwa upande wetu tumetengewa siku maalumu huko mkoani, suala ambalo linatufanya tuzidi kuwa masikini zaidi kwa kuwa hali ya uchumi imekuwa ngumu huku vijijini,” alisema.

Weka maoni yako

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>

YOUTUBE

ALBINO WAILILIA SERIKALI MAFUTA YA NGOZI