27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

MTANDAO WA ELIMU, KAMATI YA BUNGE WATETA

Na Mwandishi Wetu -Dodoma

MTANDAO wa Elimu Tanzania (TEN/MET), umekutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii na kuwasilisha hoja mbalimbali za kufanyiwa kazi na Serikali kupitia sekta ya elimu, lengo likiwa ni kuhakikisha elimu bora inapatikana nchini.

Akiwasilisha hoja mahususi 14 mjini Dodoma mwishoni mwa wiki, Mwanachama wa TEN/MET kutoka Taasisi ya FAWETZ, Neema Katundu, alisema hii ni mara ya pili kuwasilisha hoja na lengo la msingi ni kuitaka Serikali kuingiza katika utekelezaji.

Katundu alisema wanaikumbusha Serikali kuhakikisha inatenga hadi asilimia 20 ya bajeti ya taifa kwenye sekta ya elimu na pia kuwekeza zaidi katika kuziba mianya ya upotevu wa mapato na matumizi mabaya ya fedha toka mapato ya ndani, ili yaweze kutumika kwenye uboreshaji elimu ya msingi nchini.

Alisema hoja nyingine walizowasilisha serikalini ni pamoja na kutaka utoaji wa ruzuku shuleni, hali halisi ya mahitaji ya sasa na kuhakikisha mchakato wa kuanzishwa kwa Bodi ya Taaluma ya Ualimu itakayoongeza tija na kulinda masilahi ya walimu.

Hoja nyingine walizowasilisha kwa kamati hiyo ni kutaka kuimarishwa kwa Idara ya Kudhibiti Ubora (Ukaguzi) na ipewe mamlaka na vitendea kazi kiuhalisia ili iweze kufanya kazi yake kiufasaha, uzingatiwaji wa haki za watoto na pia kuundwa kwa chombo maalumu cha usimamizi, utungaji na utekelezaji wa sera ya elimu,” alisema Katundu.

Waliishauri Serikali kutoa kipaumbele cha bajeti kwa sekta ya elimu kama ilivyofanywa kwa sekta ya miundombinu miaka miwili iliyopita, Serikali za mitaa kutunga na kusimamia sheria ndogondogo zitakazowabana wazazi wanaowanyima watoto haki ya elimu, huku wakiomba fedha za mikopo ya elimu ya juu kutenganishwa na fedha za maendeleo ya Wizara ya Elimu.

Kilio kingine kilichofikishwa katika kamati hiyo, ni pamoja na kutaka kuimarishwa kwa kamati za shule, kuhamasishwa kwa wazazi kuchangia maendeleo ya watoto wao kielimu, kuingiza kipengele cha elimu ya mlipakodi katika mitaala ya elimu na pia Serikali kupunguza vigezo katika upatikanaji wa mikopo ya elimu ya juu na kuongeza bajeti eneo hilo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, Peter Serukamba, aliwashukuru wanachama wa TEN/MET kwa kuwa wazalendo kuipigania elimu nchini, hivyo kuwataka watoe muda kwa kamati hiyo ili iweze kuzifanyia kazi hoja hizo kwa maendeleo ya taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles