24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Vigogo wajisalimisha kwa Rais Magufuli

magufuli1_55a2dfc75cd8d*Ni wa makampuni yaliyochota Sh bil 300 za CIS

*Zitto kabwe aibuka, aanika madudu ya Hazina

SHABANI MATUTU NA FLORIAN MASINDE

SIKU moja baada ya Serikali kuzitaka kampuni 980 zinazodaiwa fedha zilizotolewa na wahisani chini ya Mpango Maalumu wa Kuagiza Bidhaa na Malighafi kutoka Nje (CIS), baadhi ya vigogo wameanza kujisalimisha kwa Serikali ya Rais John Magufuli.

Hatua hiyo imetokana na mpango wa Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, kuwataka wafanyabiashara  wakubwa waliochota mabilioni hayo kuyarudisha kwa mujibu wa sheria.

Inaelezwa kupitia mpango huo, zaidi ya makampuni 900 yaliyokopeshwa fedha hizo zinazofikia Sh bilioni 349, yalishindwa kuzirudisha fedha hizo, huku wengine kuona kama zawadi kwao.

Kampuni hizo zilizokopeshwa fedha hizo chini ya mpango huo, zimekuwa zikirudisha kwa kusuasua na nyingine zikionyesha nia ya kutorejesha mikopo hiyo, huku Serikali ikilazimika kutoa miezi sita kwa kampuni zote kutakiwa kulipa madeni hayo.

HISTORIA YA FEDHA ZA CIS

 Fedha hizo za kigeni zilitoka kwa wahisani kuanzia mwaka 1980 -1992/93 kwa lengo la kuipa serikali uwezo wa kuimarisha uchumi wake.

Fedha hizo zililengwa kwa taasisi, kampuni, viwanda na biashara mbalimbali ili kuzipa uwezo wa kuagiza bidhaa na malighafi kutoka nje, kwa kuwa wakati ule nchi ilikuwa na upungufu mkubwa wa fedha za kigeni.

Fedha za CIS zilitolewa kama mikopo yenye masharti nafuu, ambapo wakopaji walitakiwa kulipa deni bila kutozwa riba, lakini mkopaji akichelewa kulipa katika kipindi cha miezi 18, mkopo huo huwa na riba ya asilimia 17.

Fedha zilizokusanywa kutokana na malipo ya deni zilikuwa zinachangia mapato ya Serikali (bajeti) pamoja na miradi maalumu ya maendeleo, baada ya makubaliano na wahisani husika.

ZITTO AIBUA MADUDU

 MTANZANIA ilimtafuta aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe ambaye alionesha wasiwasi wa kufanikiwa kwa kazi hiyo chini ya Kampuni ya Msolopa Investment Ltd,  iliyopewa  kazi ya kukusanya madeni hayo .

Alisema mwaka 2013, PAC ilipowaita viongozi wa Hazina kuelezea kuhusu makusanyo hayo ya madeni walieleza kuwa makampuni mengi yamekufa hali iliyowafanya wapate ugumu katika kukusanya fedha zote.

“Kati ya madeni yaliyokuwa yakidaiwa ni Sh bilioni 379  na zilizokusanywa ni Sh bilioni 142 pekee na Kampuni ya Msolopa na kiasi kilichobaki jibu lao Hazina walisema makampuni yaliyokuwa yanadaiwa yalikuwa feki,” alisema Zitto.

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo),  alisema kampuni nyingi ambazo hazijalipa fedha hizo za CIS zimeshafungwa.

“Baada ya kubainika kwa hayo ilibidi Kamati ya PAC, kuagiza Hazina waunde kikosi kazi kufuatilia suala hilo, lakini tangu mwaka huo 2013 sikusikia chochote hadi juzi niliposikia Serikali imetangaza kumpatia kazi ya ukusanyaji madeni Kampuni ya Msolopa ambayo mwaka 2013 tulielezwa kuwa ilishindwa kazi hiyo,” alisema Zitto.

Ametaka jambo hilo kufanyiwa kazi hadi mwisho kwa sababu imekuwa ni kawaida kuibuka na kuzama kila wakati  ambapo kwa upande wa PAC ilifanya kazi kwa kiwango chake, hivyo kwa sasa Serikali inatakiwa kufanyia kazi kwa uwazi na kuzingatia haki.

“Orodha ya wadaiwa iko wazi na Kamati ya PAC ilipewa na Kampuni ya Msolopa ilipewa orodha hiyo na inapaswa kuwekwa wazi na wapo wafanyabiashara na mashirika ya umma yaliyobinafsishwa,” alisema Zitto.

KAULI YA WIZARA YA FEDHA

 Kutokana na tangazo la Wizara ya Fedha na Mipango, ambalo lililosaini na Katibu Mkuu, Dk. Servacius Likwelile, MTANZANIA ilifika wizarani hapo na kuzungumza na Msemaji wa wizara hiyo, Ingiahedi Mduma, ambaye aliwataka Watanzania kuwa wavumilivu katika kipindi  cha miezi sita kilichotolewa na Serikali kwa wadaiwa hao.

Alisema kutokana na agizo hilo la kutakiwa kulipa ni vema wadaiwa wa makampuni hayo kutumia muda huo kurejesha fedha hizo kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo majina yao kutangazwa hadharani.

Alisema ili kuhakikisha madeni hayo yanalipwa, Serikali imeingia mkataba na Kampuni ya Msolopa Investment ya jijini Dar es Salaam kuwafuatilia wadaiwa wote na kuhakikisha wanalipa ndani ya kipindi hicho.

Mduma  alisema katika juhudi hizo mpya wadaiwa waliokuwa wanafuatiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wanapaswa kuwasiliana na mamlaka hiyo waweze kupata kumbukumbu za madeni yao, vivyo hivyo kwa wadaiwa waliopata mikopo yao kupitia Benki ya Rasilimali (TIB), wanatakiwa kuwasiliana na benki hiyo kuwasilisha madeni yao haraka.

Pamoja na hali hiyo mmoja wa maofisa wa juu wizarani hapo aliiambia MTANZANIA kwamba tangu lilipotolewa tangazo hilo na Wizara ya Fedha baadhi ya viongozi wa makampuni kadhaa yanayodaiwa walikweda kujisalimisha kwa Rais Magufuli na wengine kuahidi kuzilipa ndani ya kipindi kilichopangwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles