25.9 C
Dar es Salaam
Friday, December 13, 2024

Contact us: [email protected]

Jumuiya za Kiislamu Zanzibar zapinga kurudiwa uchaguzi

jechaNa Mwandishi Wetu, Zanzibar

JUMUIYA ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) pamoja na Taasisi za Kiislam Zanzibar zimepinga kurudiwa kwa uchaguzi visiwani humo, kwa hoja kwamba hazioni busara yoyote ya kurejewa kwa Uchaguzi Mkuu Zanzibar kwa sababu ule wa awali ulifanyika kwa ufanisi na kukamilika vizuri.

Katika waraka wao walioutoa kwa vyombo vya habari jana, viongozi hao wa dini, walisema wanashangazwa na hatua ya kufuta uchaguzi huo iliyochukuliwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC),  Jecha Salim Jecha.

Wakati viongozi hao wa kiroho wakisema hivyo,  jana Ikulu ya Zanzibar ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikimnukuu Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (SMZ) Dk. Ali Mohamed Shein akisema yeye bado ni rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.

Waraka huo wa viongozi wa dini ya Kiislamu uliosainiwa na Katibu Mtendaji wa JUMAZA, Muhidin Z. Muhidini, ulisema katika Uchaguzi wa Oktoba 25, 2015, walikuwa na waangalizi katika majimbo yote ya Unguja na Pemba na kasoro zilizoripotiwa ni ndogo ndogo mno zikilinganishwa na chaguzi zote zilizopita tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.

“JUMAZA inashangazwa sana na hatua ya kufuta uchaguzi huu iliyochukuliwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jecha Salim Jecha. Tunauliza kwa nini wakati tulipokuwa na kasoro kubwa zaidi katika chaguzi za mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010 uchaguzi haukufutwa na kutakiwa kurejewa tena?

“Kwa nini iwe huu wa 2015 tu? Na je kama uchaguzi utakaorejewa nao ukawa na kasoro zitakazolalamikiwa, utafutwa tena? tutafanya chaguzi ngapi kwa mtindo huu?,” iliuliza sehemu ya waraka huo na kuendelea.

“Kitendo cha kuufuta uchaguzi huo kimesababisha nchi yetu kuingia katika mgogoro mkubwa wa kikatiba na kisiasa, kwani wananchi wa kawaida ambao ndio wapiga kura wanaathirika kisaikolojia kwa kushindwa kujua hatima ya kura walizozipiga.

“Kwa upande mwingine kumekuwa na ongezeko la ugumu wa maisha visiwani Zanzibar unaotokana na mfumuko wa bei kwa bidhaa muhimu na mzunguko wa pesa kuwa mdogo, kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kuwa na hofu ya kuendelea na shughuli za uzalishaji kwa hofu ya kutokea vurugu” ilisema sehemu ya waraka huo.

Waraka wa taasisi hizo zinazoheshimika huko Zanzibar umeeleza mambo mengi huku ukimsihi Rais Dk. John Magufuli kutumia busara kuinusuru Zanzibar isiingie kwenye machafuko.

Katika waraka huo viongozi hao wa dini walisema  walikwishamwandikia barua Rais Magufuli ambaye ameonesha dalili njema za uadilifu na uwajibikaji mkubwa ili achukue hatua za wazi na za haraka katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo kabla nchi haijatumbukia pahala pabaya.

“Aidha, tunamuomba Rais Dk. Magufuli kusimamia kwa udhati na ujasiri kuona haki inachukua mkondo wake na uamuzi wa Wazanzibari walio wengi uheshimiwe.

“Tuliwaandikia barua za nasaha viongozi wote wakuu wa kisiasa wanaoshiriki katika mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa mkwamo huo wa kisiasa.

“Tuliwaandikia barua mabalozi wa nchi sita waliopo Tanzania kuomba wasaidie katika kuutafutia ufumbuzi mgogoro huu katika kuhakikisha demokrasia inachukua mkondo wake. Mabalozi wahusika ni kutoka nchi za Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Norway na Sweeden” unasema waraka huo wa viongozi wa dini ya Kiislam.

Dk. Shein akaza buti

Wakati huo huo, Rais wa SMZ na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema yeye bado ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.

Dk. Shein alisema yeye anaongoza nchi kwa mujibu wa Katiba na sheria na kama si uwezo huo aliopewa kikatiba hana sababu ya kuendelea kukaa madarakani pamoja na serikali anayoingoza.

Dk. Shein alitoa kauli hiyo jana kwa nyakati tofauti wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba katika siku yake ya kwanza ya ziara yake ya siku tatu kisiwani humo kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi.

“Tuko madarakani na uongozi wote wa serikali… yupo Makamu wa Kwanza wa Rais, Makamu wa Pili wa Rais na mawaziri” alisisitiza Dk. Shein na kuongeza kuwa hao wanaodai kujiondoa serikalini ni uamuzi wao wenyewe.

Alibainisha kuwa yeye na serikali anayoingoza kuendelea kuwepo madarakani “si uamuzi wake” na wala yeye hana ubavu wa kujiweka madarakani bali ni Katiba ambayo inajieleza wazi” alisema Dk Shein.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles