24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Zitoto asisitiza mabadiliko nchini

IMG_5219NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM

KIONGOZI wa Chama Cha ACT-Wazelendo, Zitto Kabwe, amesema ni vigumu Watanzania kupata mabadiliko kwa viongozi walewale waliowahi kushiriki kuinyonya wakiwa mawaziri wakuu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alisema Tanzania inapoteza Sh bilioni 900 kwa kila mwaka kwa wafanyabiashara wakubwa wachache wanaotumia ulaghai kukwepa kodi.

Zitto alikuwa akuzungumza kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni ya uchaguzi ya chama hicho uliofanyika kwenye viwanja vya Zakhem, Mbagala, Dar es Salaam jana.

Alidai  siyo CCM wala Ukawa wanaoweza kuzungumzia jambo hilo kwa sababu wanafadhiliwa kwenye kampeni zao na matajiri hao.

“Chama pekee kitakachowashukia wakwepa kodi wote ni ACT Wazalendo ambacho kitasaidia kuokoa Sh bilioni 900 ambazo zitaingizwa kwenye sekta ya elimu na afya kwa kutumia mifuko ya jamii,” alisema.

Zitto alisema chama cha ACT-Wazalendo kitasimamia ufisadi wa aina yoyote kwa kuhakikisha kinasimamia na kuendeleza uadilifu kwa kuwataka viongozi wake wanaotaka kuwania madaraka   watangaze mali zao kabla ya kuingia madarakani.

Alisema ingawa kila chama kimekuwa kikijinadi kwamba kitapambana na rushwa kwa kutumia miiko ya uongozi,   vyama vingine vinaeleza namna ya kuiondoa rushwa huku vikishindwa kueleza namna vitakavyopambana.

“Hiyo imechangiwa na nchi hii kuwa na mawaziri wakuu wanaofikia 10 tangu kuasisiwa kwake ambako watatu wamekwisha kufariki dunia.

Wanne waliohai wanaisaidia CCM na wawili wanakiunga mkono Ukawa wakihubiri mabadiliko.  Swali ni je, unawezaje kuhubiri mabadiliko kwa mawaziri wakuu waliokuwa kwenye serikali iliyowanyanyasa wananchi wanyonge?” alihoji Zitto na kuongeza:

“Tumesikia mmoja wa wagombea akisema watarejesha shirika la ndege hivi tujiulize mwaka 1996 -2002 wakati linauzwa shirika hilo Waziri Mkuu alikuwa nani?  Watu wakajibu (Lowassa)…hatuwezi kutumia watu walewale kuleta mabadiliko kwa watu waliotuletea matatizo.

“Mgombea wa CCM anasema ataleta mahakama maalum ya kushtaki mafisadi… wakati tukiwa kwenye bunge la katiba tulitaka Takukuru ipewe meno mgombea wa CCM alikataa leo ameona kuna nini cha muhimu.  Hivyo tunatakiwa kutambua kwamba chama chenye kufanya mabadiliko ni ACT chini ya mgombea wetu Anna,” alisema Zitto.

Kiongozi huyo wa ACT alibeza ahadi iliyotolewa na  CCM kutoa Sh milioni 50 kwa kila kijiji.  Alisema kwa vijiji vyote Tanzania nzima itagharimu Sh bilioni 600 ambazo ni sawa na bajeti ya wizara nzima ya kilimo, bila ya kueleza mahali watakapozipata.

Mgombea Urais

Mgombea urais wa chama hicho, Anna Mghwira alisema iwapo atapata nafasi hiyo atahakikisha anamteua kiongozi mkuu wa chama hicho na kuwa waziri wake mkuu   waweze kushirikiana katika kuleta mabadiliko ya fikra na sera.

Alisema akichaguliwa kuwa rais wa tano atahakikisha analinda utu, uzalendo na uadilifu ambao uliasisiwa na Mwalimu Nyerere lakini sasa   umeporomoka kwa kiasi kikubwa.

Mgombea huyo ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alisema akipewa nafasi atatengeneza serikali itakayolinda Muungano, itakayojumuisha mashirika ya dini na asasi za raia kwa sababu anaamini   taifa halina dini.

Alisema  na serikali yake itaapishwa Dodoma kama alivyofikiri Mwalimu Nyerere kwa kuwa mkoa huo ndiyo makao makuu ya Serikali.

Mabango yaliyokuwapo

Wakati huo huo, mkutano huo ulipambwa na mabango mbalimbali   baadhi yakisomeka:   ‘Kuzikwa na wengi siyo kwenda peponi’, ‘ACT chama kitakachong’oa wezi’, ‘Anna ni mpambanaji wa kweli’, ‘ACT ndicho chama mbadala wa CCM’, ‘ACT chama kinachojali akina mama’.

‘Hakuna kama ACT’, ‘Mwisho wa CCM Oktoba 25’, ‘Wazalendo wa kweli ACT’, ‘Zitto mbabe wao’, ‘hatulei mafisadi’, ‘waadilifu wapo ACT’, ‘CCM majizi hayana uzalendo’, ‘ACT mkombozi wa taifa letu’, ‘Watanzania wanataka fikra pevu’ na ‘wazendo wasiotumia fedha’. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles