23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Duni amaliza utata wa mgombea ubunge Ukawa Mtwara

duniNa Elias Msuya, Mtwara

MGOMBEA mwenza wa urais wa Chadema kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Juma Haji Duni, amemaliza utata wa mgombea ubunge wa umoja huo jimbo la Mtwara baada ya kumtangaza Maftah Hanachuma Mchumo kuwa ndiye atakayepeperusha bendera za vyama vinavyounda umoja huo.

Utata wa mgombea wa Ukawa katika jimbo hilo ulitokana na   Chadema kumsimamisha Joel Nanauka, NCCR Mageuzi, Uled Hassan Abdallah na CUF, Maftah Machumo.
Kabla ya Duni kumtangza Maftah, Makamu mwenyekiti wa Chadema (Zanzibar), Ali Said Mohamed, alisema hawatatangaza mgombea jambo lililozua vurugu kwenye mkutano huo uliofanyika katika uwanja wa Mashujaa mjini Mtwara jana.
Baada ya kuona vurugu hizo, Duni aliyekuwa amemaliza kuhutubia, alisimama jukwaani na kumtangaza Maftah na kusababisha shangwe kubwa kutoka kwa wananchi waliokuwa wamefurika katika uwanja huo.
“Namtangaza Maftah kuwa mgombea ubunge…,” alisema Duni.

Mbali na suala hilo, Duni alisema serikali ya Ukawa itapambana na kero za stakabadhi ghalani kwa wakulima wa korosho, ukosefu wa elimu na wananchi kutonufaika na gesi inayopatikana mkoani humo.

Akiwa akiwa wilayani Newala, alisema haiwezekani wakulima wa korosho wahangaike kutunza mazao yao halafu Serikali iwaingilie wakati wa kuvuna.
“Haiwezekani bibi mkubwa na mtoto wake mgongoni walime, wapalilie halafu ukifika wakati wa mavuno Serikali ije kuwakopa. Hakuna kuwakopa masikini, Ukawa tukiingia madarakani tutaweka bei inayostahili na tutafuta stakabadhi ghalani,” alisema Duni.

Kuhusu gesi, Duni alisema kinachotakiwa ni rasilimali hiyo kuwanufaisha wananchi wa mkoa huo inapotoka hata kama inasafirishwa kwenda Dar es Salaam.

“Haiwezekani gesi iende Dar es Salaam wakati hapa hamna umeme. Akija Magufuli (Dk. John) hapa ambaye sisi ndiyo funguo zake na kuwapa ahadi mpya, muulizeni zile alizoahidi Kikwete (Rais Jakaya) mbona hazijatatuliwa?”  alisema.
Akizungumza katika uwanja wa mashujaa mjini Mtwara,  Duni alisema Ukawa wakiingia madarakani watatoa elimu bure kutoka shule ya msingi hadi chuo kikuu.
“Naweza kujitolea mfano mwenyewe. Mimi nimezaliwa peke yangu kwa wazazi wangu, nilisoma elimu ya msingi bure, darasa la 13 hadi 14 bure, nimeenda chuo kikuu bure na ninaenda Ulaya kusoma kwa gharama ya serikali hadi leo nimekuwa mtaalam. Kwa nini nyie msisome bure,” alihoji Duni.
Akiwa wilayani Newala, Duni alimtambulisha Juma Manguya kuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CUF.
Awali akimkaribisha Duni kuhutubia, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Zanzibar Ali Said Mohamed alisema katika wilaya ya Newala vyama vya CUF na Chadema vimegawana kata ambako CUF imepata kata 12 na Chadema nne Newala mjini huku vijijini CUF ikipata kata 17 na Chadema tano kwa ajili ya wagombea udiwani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles