24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

ATLANTROPA: Ndoto ya kuunganisha Afrika, Ulaya kuwa bara moja

namna-ambavyo-atlantropa-ingeonekana-kutokea-angani* Ni mpango wa kukausha bahari kuzaa Eurafrika

UKISOMA kichwa cha habari cha makala hii mawazo yako yatakuambia ni mpango wa kufikirika, lakini kwa mujibu ya wataalamu wa wakati ule ungewezekana iwapo kungekuwa na utashi na ushirikiano wa kutosha baina ya mataifa kuufanikisha.

Kwa wakati fulani, Afrika na Ulaya zilitenganishwa kwa umbali wa maili 8.7 tu sawa na kilomita 14, lakini bado Bahari ya Mediterranea ilizuia mabara hayo kuungana.

Lakini mwaka 1928, msanifu ramani mashuhuri wa Ujerumani Herman Sörgel aliwasilisha mpango aliouita Atlantropa, ambao pamoja na mambo mengine ungehusisha kukausha maji ya bahari hiyo na kuunda bara kubwa kabisa duniani la ‘Eurafrika’

Wakati wazo hilo likionekana kuwa ajabu na kioja au lisilowezekana, lilichukuliwa uzito mkubwa na wakuu wa mataifa na wakati fulani hata katika Umoja wa Mataifa (UN) kipindi kile.

Sörgel aliamini pamoja na mambo mengine kwamba mpango huo wa aina yake utakuwa jibu kwa tatizo la Ulaya la mgogoro wa wakimbizi waliotokana na Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia (WW1) na kusaidia kuleta amani duniani.

Alitaka iundwe kwa mabwawa ya nguvu za umeme katika ukanda wa Mlango Bahari wa Gibraltar, Dardanelles, na kati ya Sicily na Tunisia kila moja ikiwa na mitambo mikubwa ya nguvu za umeme.

Sörgel aliamini kuwa hilo litaibadili Mediterrania kuwa katika mabonde mawili makubwa, kwa sehemu ya magharibi likipunguzwa kwa mita 100 na mashariki kwa mita 200.

Hilo lingetoa jumla ya maili za mraba 254,900 sawa na kilomita mraba 660,200 za ardhi, yaani taifa au mataifa mapya yaliyotokana na bahari hiyo, likiwa ni eneo kubwa kuliko Taifa la Ufaransa.

Katika makala kwa jarida la The Conversation, Dk. Ricarda Vidal, mhadhiri wa Utamaduni wa Uoni na Historia katika Chuo cha King London nchini Uingereza alisema:

“Uzoefu wake wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, majanga ya kisiasa na kiuchumi ya mwaka 1920 na kuibuka kwa sera za Kinazi nchini Ujerumani kulimwaminisha Sörgel kuwa vita mpya ya dunia inaweza kuepukwa iwapo suluhu nzito itapatikana.

“Akiwa na imani ndogo katika siasa, Sörgel aligeukia teknolojia kama suluhu ya kuondokana na uwezekano wa kuzuia vita.”

Aliamini kuundwa kwa Bara Eurafrika kutakuwa jibu kwa Ulaya dhidi ya mgogoro wa ukimbizi uliosababishwa na WWI na kusaidia kuiletea dunia amani.

Dk. Vidal alisema: “mipango ya baadaye kwa Atlantropa pia ilihusisha mabwawa mawili katika Mto Congo na kuundwa kwa Bahari ya Chad katika ziwa na bonde kubwa la Chad na Congo.

Kwa mpango huo, Sörgel alitumaini kutachochea ushawishi wa hali ya hewa ya Afrika na kuifanya ifurahishe walowezi wa Ulaya.

Lengo la kufanya hivyo pia lilikuwa kutiririsha maji safi kwa ajili ya umwagiliaji kusini mwa Sahara Afrika na kutengeneza mfereji wa kupitisha meli ndani ya Afrika.

Wakati pendekezo hilo likionekana kama mzaha kwa sasa, wakati Sorgei alipolitoa kwa mara ya kwanza kipindi kile, lilichukuliwa kwa uzito mkubwa na wachora ramani, wahandisi,  wanasiasa na waandishi wa habari.

Kilichofanya wazo la Atlantropa livutie ni maono yake kwa amani ya dunia kuwa haiwezi kupatikana kwa siasa na diplomasia bali suluhu ya teknolojia.

Atlantropa ilikuwa idhibitiwe na chombo huru ambacho kingekuwa na nguvu ya kuzima usambazaji wa nishati kwa tafa lolote litakaloashiria kuwa tishio kwa amani.

Sörgel aliamini mradi huu kwa kugharimu mataifa fedha nyingi, kungewanyima uwezo na kiburi cha kugharimia vita na badala yake kujikita kwenye teknolojia kwa ajili ya ustawi na amani.

Aliuona mradi wake huo ambao ulipaswa kuchukua karne moja, kama njia ya amani Ulaya mbadala ya dhana ya ‘Lebensraum’ ambayo ilikuja kuwa moja ya sababu za uvamizi wa maeneo mapya uliofanywa na utawala wa Nazi wa dikteta Adolf Hitler wa Ujerumani.

Kwamba, Atlantropa itatoa ardhi na chakula, ajira, nguvu ya umeme na zaidi ya yote maono mapya kwa Ulaya na Afrika.

Aidha, ni njia ya kuiunganisha Ulaya iliyochakazwa kwa vita na kutengeneza bara moja kubwa ambalo litaifanya dunia kuwa na mabara makubwa matatu; Amerika, Asia na Atlantropa.

Ili kulitangaza wazo lake alitumia vipindi vya redio, filamu, mazungumzo na hata kutengeneza mfano wa Atlantropa.

“Haikushangaza, machoni mwa wenzake wakati ule, wazo lake kuhitaji ushirikiano wa mataifa, daima ilionekana hata kuwa kitu cha kufikirika kuliko teknolojia kubwa ya Atlantropa,” alisema Dk. Vidal.

Mwaka 1948, jarida la UN lenye makao mjini New York, liliandika: “Kutumia maporomoko ya maji Gibraltar kutengeneza umeme kwa ajili ya ustawi wa mwanadamu ilionekana kama ndoto, lakini hii ni karne ya 20 si ndoto, tatizo ni ushirikiano baina ya mataifa katika kuitimiza.”

Bahati mbaya kwa Sörgel, mipango yake haikundelea na Afrika na Ulaya zimebakia kuwa mabara mawili tofauti.

Naam, mradi huo wa aina yake ulipata sifa na kushabikiwa mwishoni mwa miaka ya 1920 na mapema miaka ya 1930, na kwa kipindi kifupi tena mwishoni mwa miaka ya 1940 na mapema miaka ya 1950, lakini ukatoweka muda si mrefu baada ya kifo kumchukua Sörgel.

Mipango yake ya dhati ikiwamo michoro ya miji mipya na maandishi kuunga mkono mawazo yake zinatunzwa katika makumbusho ya Deutsche mjini Munich.

 

Inakotoka Bahari ya Mediterania

Kwa mujibu ya wanasayansi Bahari ya Mediterranea iliyopo leo hii ilitokea miaka milioni 5.3 iliyopita kwa mafuriko makubwa ya kutisha.

Maji kutoka Bahari ya Atlantic yalibomoa daraja lililokuwapo katika Mlango wa Gibraltar, na kufanya mafuriko ya maji kuingia bondeni.

Bonde la Mediterrania awali  lilikuwa saehemu ya mtandao mpana wa bahari wakati mabara hayo mawili yalipopwelea hadi mahala yalipo sasa.

Ilitengwa na bahari kuu za dunia miaka milioni 5.6 iliyopita na lilikuwa linywee kabisa kipindi cha mamia kwa maelfu ya miaka iliyopita.

Lakini inadhaniwa kwamba kupanda kwa viwango vya maji baharini na mwenendo wa ganda la nje la dunia ilisababisha Mlango Bahari wa Gibraltar kuzama na kuiruhusu Bahari ya Atlantic kurudisha maji katika mabonde Mediterrania na hivyo uwepo wa bahari ya sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles