21.4 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Ziara ya Rais Samia India yaleta neema

*Hospitali ya kwanza ya watoto kuanzishwa, dawa zikishuka bei

*Neema kugusa kilimo, maji na iwanda

Esther Mnyika na Betrice Kaiza, Mtanzania Digital

Serikali kwa kushirikiana na Hospitali ya Rainbow ya nchini India wanatarajia kuanzisha hospitali maalumu itakayohusika na magonjwa ya watoto pekee wenye umri wa siku moja hadi miaka 17.

Aidha, makubalianao mengine ni kuanzishwa kwa tiba mtandao (Medicine Digital) kwa kushirikiana na hospitali za Rainbow, Max Dkl na Hesta ambao ni wauzaji wa dawa za binadamu.

Hayo yamebainishwa Oktoba 12, Ikulu jijini Dar es Salaam katika mkutano na Waandishi wa Habari juu ya mafanikio ya ziara zilizofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na ujumbe wake kwenye nchi za Qatar na India.

Akifafanua zaidi kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika Sekta ya Afya, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kuwa wamesaini hati tatu za makubaliano katika sekta hiyo.

“Moja ya makubaliano ni kuanzisha kwa hospitali ya watoto nchini ambayo itakuwa maalum kwa watoto kuanzia siku moja hadi umri wa miaka 17, huu ni uwekezaji mkubwa sana kila kitu watajitegemea, hivyo hili ni moja ya mafanikio makubwa ambayo tumeyapata kama nchi kupitia ziara hii ya Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan,” amesema Ummy.

Sambamba na hayo, Waziri Ummy amesema kuwa hopitali hiyo inatarajia kuanzisha kituo cha tiba asili nchini ambapo wamenunua hekari 100 wilayani Mkuranga kwa ajili kupanda miti ya tiba

“Tumeanza na vituo saba hospitali za rufaa tiba asili ikiwa India tayari wana tiba hizo mgonjwa anachagua atibiwe kisasa au asili na madaktari washauri kutibiwa kiasili au kisasa ni makubaliano ya nchi hizi mbili,”amesema.

Amesema katika uzalishaji wa dawa wamepata mwekezaji kudhibiti bei za dawa na asilimia 80 zinatoka nje na asilimia 60 kutoka India.

Ummy amesema hatua ya kupatikana kwa mwekezaji wa kuzalisha dawa nchini atasaidia kushusha gharama za dawa na kupatikana kwa wakati.

Ameeleza ushirikiano wa kupandikiza figo na ini bado ni changamoto na kwa hapa nchini nakwamba bado hawajafanikiwa, hata hivyo amesema tayari Serikali inao madaktari bingwa na wanaamini baada ya miaka miwili upandikizaji ini nchini utaanza.

Amesema kuhusu afya ya akili bado ni changamoto ambapo Tanzania na India zitashirikiana katika mafunzo ya yoga kupanua afya ya akili kuhamasisha kuwa na mafunzo ya yoga.

Mbaazi nazo zapata soko

Naye Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akizungumzia suala la zao la mbaazi amesema wamepata soko la uhakika la mbaazi nchini India.

Amesema katika makubaliano ya kuuza zao la mbaazi nchini watapeleka tani 200,000 kila mwaka .

“Mahitaji yao ni tani milioni tano wanazalisha tani milioni 2.5 hivyo tutapeleka mbaazi yenye ubora na viwango vizuri,” amesema Bashe.

Amesema suala la bidhaa yoyote ni matokeo ya soko na kwamba wanatafuta kipato cha mkulima hivyo kupata soko kwenye soko la mbaazi ni msingi.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema India ni wadau muhimu katika sekta ya maji na miradi mikubwa ya mikakati hivyo wanatarajia kuanza kutumia teknolojia katika huduma za maji na kufanya mageuzi nchini.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema wametenga hekari 1,000 mkoani Pwani kwa ajili ya wawekezaji wa viwanda kutoka India ambapo watajenga viwanda 200.

Amesema wanaendelea kuongeza thamani ya mazao kilimo sayansi ya mazao, udongo na teknolojia.

Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus alisema ziara hizo za Rais Samia alisema lengo la ziara ilikuwa ni kuendelea kudumisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na India, hususan katika sekta za kimkakati kama afya, viwanda, biashara, ulinzi na usalama, elimu, teknolojia ya habari na mawasiliano, uchumi wa buluu, maji, na kilimo.

Amesema lengo la pili ilikuwa ni kutangaza fursa za biashara na uwekezaji za Tanzania ili kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara kutoka India.

Nchi hizo pia zilibadilishana hati za makubaliano 15, ambapo 10 zilihusisha Serikali na 5 sekta binafsi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles