29.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali: Mpango wa MTaKEU utakuza na kuendeleza kisomo na elimu

Na Gustafu Haule, Pwani

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeandaa Mpango Mkakati wa miaka mitano kuanzia mwaka 2020 hadi 2025 ambao umelenga kukuza na kuendeleza Kisomo na Elimu kwa umma (MTaKEU).

Hayo yemabinishwa leo Alhamisi Oktoba 12, 2023 na Mratibu wa kongamano la Kitaifa la maadhimisho ya Juma la Elimu ya watu Wazima Dk. Sempeo Siafu wakati akifungua kongamano hilo lililofanyika Kibaha mkoani Pwani.

Dk. Siafu amesema mkakati huo uliandaliwa kwa makusudi kama nyenzo ya kuongoza wadau mbalimbali ambao wanatekeleza programu za kisomo na kwamba mpango huo unatambua kisomo kama haki ya msingi kwa maendeleo ya mtu binafsi, kijamii,kiuchumi na kisiasa.

Aidha, amesema mbali na mpango huo pia wizara tayari imeandaa miongozo mitano ambayo inasaidia katika utekelezaji wa kuimarisha ubora wa utolewaji wa Elimu ya Sekondari kwa njia mbadala (ASEP).

“Ili kukabiliana na changamoto ya kushuka kwa kiwango cha wanaojua Kusoma, Kuandika na Kuhesabu(KKK), wizara imeona ije na mpango huo madhubuti pamoja na miongozo yake mitano ambayo imewapa fursa vijana walio nje ya mfumo rasmi kuendelea na masomo hususani wasichana waliopata ujauzito,” amesema Dk. Siafu.

Dk. Siafu amewaasa wadau wote kutumia kongamano hilo kujadili na kuangalia namna ya kuboresha mazingira ya ujifunzaji katika programu za kisomo yanayozingatia ubora,usawa na ujumuishi wa makundi yote.

Amesema nchini Tanzania maadhimisho hayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka katika ngazi ya Mkoa au Wilaya kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali zinazotekeleza progaramu za Elimu ya Watu Wazima ambapo mwaka huu Wizara imeshirikiana na Tamisemi kuratibu maadhimisho hayo Kitaifa Mkoa wa Pwani.

Amesema, lengo la kufanya maadhimisho hayo ni kuimarisha ushirikiano miongoni mwa jamii pamoja na kupaza sauti kwa pamoja kuhusu umuhimu wa Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo .

Ameongeza kuwa, katika miaka ya 1980 Tanzania ilifikia rekodi ya kushuka kwa kiwango cha kutokujua Kuandika, Kusoma na Kuandika (KKK) kutoka asilimia 80 mwaka 1961 hadi kufikia asilimia 9.6 mwaka 1986 ambayo ilikuwa miongoni mwa viwango vya juu duniani.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tamisemi, Ernest Hanju,amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini Rais Dk. Samia Suluhu Hassan inafanyakazi kubwa ya kuhakikisha mipango na mikakati ya kuimarisha Elimu ya Watu Wazima inafikia kwa malengo.

Hata hivyo, Afisa Elimu Mkoa wa Pwani Sara Mlaki ameishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Tamisemi kwa kuleta maadhimisho hayo Mkoa wa Pwani.

Mlaki amesema Mkoa utayatumia maadhimisho hayo kama sehemu ya kujifunza katika kuleta mabadiliko chanya na hivyo kufikia idadi kubwa ya watu wazima kujua Kusoma,Kuandika na Kuhesabu pamoja na kufikia malengo mengine ya Kitaifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles