Ziara ya Majaliwa maumivu, mwingine asimamishwa kazi

0
589

MWANDISHI WETU-MOGORO

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amemsimamisha kazi Mhandisi wa Ujenzi Wilaya ya Morogoro, Brown Undule, baada ya kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, ikiwemo usimamizi mbovu wa ujenzi wa Kituo cha Afya Mkuyuni.

Amemsimamisha kazi mhandisi huyo jana baada ya kukagua ujenzi wa kituo hicho cha afya akiwa katika siku ya tano ya ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.

Majaliwa alisema hajaridhishwa na aina ya milango iliyotumika katika kituo hicho.

“Milango yote katika jengo hili ing’olewe leo leo (jana), huwezi kuweka milango ya hovyo namna hii, yaani mtu wa nje anamuona aliyeko ndani, nimesitisha kuendelea kukagua jengo. Yeye na usomi wake ameridhishwa na milango ya hovyo kama hii!” alisema Majaliwa.

Alisema aina ya milango iliyowekwa katika kituo hicho cha afya haiwezi kutumika hata kwenye nyumba ya mtu binafsi, lakini kutokana na uangalizi mbovu kutoka kwa watendaji, walikubali kuweka milango hiyo mibovu.

Majaliwa alisema Serikali imeamua kujenga vituo vya afya vitano katika wilaya hiyo kusogeza huduma za afya kwa wananchi na kuwapunguzia kutembea umbali mrefu kufuata huduma hizo, hivyo amewataka watendaji wasimamie ipasavyo miradi hiyo.

Alisema kuwa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli imedhamiria kuboresha huduma za afya kwa wananchi, hivyo amewataka wananchi waendelee kuwa na imani nayo.

Baada ya kukagua ujenzi wa kituo hicho cha afya, Majaliwa alikagua pia ujenzi wa hospitali ya wilaya, ambako nako ameagiza kung’olewa kwa mbao zote zilizotumika kupaulia jengo la mama na mtoto kwa kuwa hazina viwango.

“Fundi usiendelee na kazi hii ya upauaji kwa sababu mbao unazotumia hazikidhi viwango,” aliagiza.

Kwa upande wake, fundi anayejenga jengo hilo, Johnson Ishengoma, alisema changamoto kubwa anayoipata katika ujenzi huo ni ucheleweshwaji wa vifaa pamoja na kulazimishwa kutumia vifaa vilivyo chini ya kiwango.

Fundi huyo alitolea mfano kuwa aliomba mbao za urefu wa futi 20, lakini aliletewa zenye urefu wa futi 12 na kulazimishwa azitumie hivyo hivyo.

“Mhandisi wa Wilaya Brown Undule na mtu wa manunuzi, Grace ndio wanaoniletea vifaa hivi. Baadhi ya vifaa huwa navikataa kutokana na kutokuwa na ubora,” alisema.

Katika hatua nyingine, Majaliwa alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Steven Kebwe kuuangalia vizuri mkoa wake na kuhakikisha anauchunga vizuri kwa sababu umekithiri kwa matumizi mabaya ya fedha za umma.

“Wakati nikiendelea na ziara mkoani hapa, nimepata taarifa kwamba zaidi ya Sh milioni 9 zimetumika kwa ajili ya kulipana posho katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara.

“Posho hizo ni kwa ajili ya ziara ya Waziri Mkuu na imetoka kwa mtendaji wa Kata ya Viwanja 60, hili jambo halikubaliki.

“Nakukabidhi risiti zote na uwachukulie hatua wote waliohusika, Mkoa wa Morogoro ni shida,” alisema Majaliwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here