BRIGHITER MASAKI-DAR ES SALAAM
HALMASHAURI ya Manispaa ya Kinondoni imewapa muda wa mwezi mmoja na nusu wafanyabiashara wa Ufukwe wa Coco (Coco Beach) kupisha eneo hilo kwa ujenzi wa ufukwe wa kisasa.
Tamko hilo limetolewa jana Dar es Salaam na Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta wakati akizungumza na wafanyabiashara wa mihogo katika ufukwe huo.
Alisema mwezi mmoja na nusu unatosha kwa wafanyabiashara hao kujipanga, kukamilisha na kujiandaa na eneo jipya.
“Nakubaliana na ombi lenu la kuwa karibu na hapa, tunalipokea na tunatoa mwezi mmoja na nusu hadi Novemba 5 tutapiga bati eneo lote ili kuendelea na ujenzi, biashara zenu mtapewa eneo jingine.
“Katika maendeleo lazima changamoto ziwepo, vumilieni wakati wa mpito huu mara baada ufukwe wa kisasa kukamilika mtarudi eneo lenu baada kukamilika ujenzi, mkandarasi atajenga kwa muda wa miezi sita,” alisema Sitta.
Alisema Ofisa Masoko wa Manispaa na Mtendaji wa Kata wataenda kuwaorodhesha na kujua idadi ya wafanyabiashara wote wanaotegemea eneo la ufukwe huo kufanya biashara zao na ujenzi ukikamilika waliokuwepo wote watapewa kipaumbele kurudi katika nafasi na kuendelea na biashara zao.
“Wale waliokuwepo hapa ni lazima mrudi hapa, nawatoa wasiwasi, lakini katika kipindi hiki cha matengenezo lazima tupafunge, tukubaliane ili tujuwe kipindi hiki cha mpito mnapendekeza muende wapi na mnataka mfanyiwe nini,” alisema Sitta.
Alisema ufukwe huo wa Coco ujenzi wake umeanza juzi rasmi na mkandarasi wa Kampuni ya Tanzania Bulding Works anajenga ufukwe wa kisasa kwa Sh bilioni 13.6 fedha kutoka Serikali kuu zilizotolewa na Rais katika miradi mkakati.
Alimpongeza Rais Dk. John Magufuli na alimuahidi kutomwangusha katika utekelezaji wa miradi hiyo katika kuunga mkono juhudi zake na kujenga Tanzania ya uchumi wa viwanda.
Awali kabla ya maamuzi hayo ya Meya Sitta, wafanyabiashara waliomba kupatiwa eneo la kuendelea na biashara zao.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Asha Machupa, alisema yeye ni mjane, anategemea kufanya biashara eneo hilo na pesa anayopata anasomesha watoto wake ambao wapo chuo.