24 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Zaidi ya wakulima 6,000 wajiunga na mfumo wa kilimo cha mkataba

Na Hadia Khamis, Mtanzania Digital

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko(CPB), Dk. Anselm Moshi amesema zaidi ya wakulima 6,000 nchini wameingia katika mfumo wa kulima kilimo cha mkataba.

Akizungumza na Mtanzania Digital Dar es Salaam jana katika maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara maarufu Sabasaba, Dk. Moshi amesema kilimo hicho cha mkataba kitamsaidia mkulima kurejesha gharama zake alizotumia wakati wa kuandaa shamba na kuuza mazao yake yote aliyoyavuna.

Alisema bodi hiyo inaendesha kilimo hicho cha mkataba na tayari wameshaanza katika zao la ngano maeneo ya Kaskazini huko Kilimanjaro eneo la Siha, mkoani Arusha eneo la Monduli, Karatu, Semanjiro na Manyara eneo la Hanang.

“Maeneo hayo yote tumeingia mkataba na wakulima wa kilimo cha ngano kuzalisha zao hilo, lakini pia tunafanya kilimo cha mkataba kwenye maharage ya soya na tumeshaanza kwenye mkoa wa Songea,” alisema MOshi

Alisema wameshaanza kilimo mkataba kwenye zao la alzerti katika mikoa ya Singida, Dodoma na Simiyu huku mpango wao ni kuhakikisha kwenye mazao yote wakulima wanalima kwa kilimo cha mkataba ili kuwa na uhakikika wa mazao yao kununuliwa bila kupata hasara.

“Kilimo hicho cha mkataba huo unasainiwa na taasisi tano ambazo ni mkulima mwenyewe ambaye ndiyo mzalishaji, benki watoaji wa fedha, wasambazaji pembejeo pamoja na mtu wa bima ambaye ndiyo mnunuzi,”alisema Moshi.

Alisema ili kuhakikisha mkulima anakuwa na soko la uhakika kwa ajili ya mazao yao, bodi hiyo ya CPB inajenga viwanda kwa wingi katika kila eneo la nchi ambavyo pia vitatoa ajira kwa vijana, kuongeza thamani ya mazao yanayozaliishwa ili yaweze kuuzwa katika soko la kimataifa kwa faida kubwa zaidi kisha kuiletea nchi fedha za kigeni.

Alisema bodi hiyo lengo lake ni kuhakikisha mkulima mdogo mdogo wa Tanzania anapata bei shindani katika mazao yake anayoyazalisha kwa kujenga uwezo mkubwa wa kuweza kununua mazao ya mkulima kwa bei shindani.

“Tunatekeleza hayo kwa kufanya uchambuzi wa kufahamu na kujua mkulima anatumia kiasi gani shambani na kwamba tukinunua kwa bei gani mazao yake anaweza kurejesha gharama alizozitumia na kupata faida,” alisema Moshi.

“Kwa sababu tunanunua sisi kwa wingi inawafanya wafanyabiashara wengine kununua kwa bei hiyo hiyo ya kwetu, hivyo kufanya mkulima kurudisha gharama zake, kupata faida na kuhamasika kwenda kulima tena huku nchi kuwa na usalama wa chakula,” alisema Moshi.

Aidha, Dk. Moshi alisema Serikali imetoa maelekezo kwa bodi hiyo kuhakikisha kuwa ngano inazalishwa hapa nchini hadi kufikia tani milioni moja na zaidi ifikapo 2025.

Alisema katika kutekeleza mkakati huo mwaka 2021 waliagiza Mbegu za tani 210 nchini Zambia na kuzigawa kwa wakulima kwa mkopo katika kanda ya Kaskazini na matokeo yalikuwa mazuri.

Amesisitiza kuwa Mwaka huu wamejipanga kwasababu kuna mbegu zimezalishwa ndani ya nchi na serikali imeweka jitihada kupitia taasisi za Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na Kampuni ya kuzalisha mbegu ya ASA ili kuweza kuzalisha mbegu nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles