31.2 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga yatinga robo fainali Mapinduzi Cup

Pg 32 leo

TIMU ya Yanga jana ilitinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea visiwani Zanzibar baada ya kuichapa Polisi ya humo mabao 4-0, mchezo uliofanyika Uwanja wa Amaan.
Timu hizo zilizopo katika Kundi A ziliingia uwanjani zikiwa na kumbukumbu ya ushindi kwenye mechi zao za kwanza, ambapo Yanga iliifunga Jango’mbe kwa mabao 4-0, huku Polisi ikiifunga Shaba ya huko kwa bao 1-0.
Shujaa wa Yanga kwenye mchezo huo alikuwa ni winga wake wa kushoto, Mbrazil Andrey Coutinho, aliyefunga mabao mawili peke yake.
Polisi ilianza kwa kasi mchezo huo kwa kutumia mashambulizi ya pasi fupi fupi, lakini mabeki wa Yanga chini ya nahodha, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, walikuwa makini na kuzuia kiustadi mashambulizi hayo.
Yanga ilijibu mapigo hayo na kufanikiwa kupata bao la kwanza dakika ya 27 lililofungwa na winga, Andrey Coutinho, aliyefumua shuti kali lililomshinda kipa wa Polisi, Nasir Seleman, Coutinho alifunga bao hilo baada ya kupokea pande la Amissi Tambwe.
Wanajangwani hao walizidi kuliandama lango la Polisi ambapo dakika ya 34 mshambuliaji raia wa Liberia, Kpah Sherman alifanikiwa kuiandikia bao la pili kwa shuti akimalizia kazi nzuri ya Tambwe aliyeruka juu na kumpigia pasi ya kichwa kufuatia mpira mrefu wa winga, Simon Msuva.
Mwamuzi wa mchezo huo, Ramadhani Ibada ‘Kibo’, aliwaonyesha kadi ya njano wachezaji wa Polisi, Abdallah Mwalimu, aliyemfanyia madhambi Coutinho dakika 19 na Frank Temis, dakika ya 42 aliyemchezea rafu kiungo wa Yanga, Nizar Khalfan.
Hadi mwamuzi wa mchezo huo, Ibada anapuliza kipyenga cha kuashiria mapumziko, Yanga iliondoka kifua mbele kwa mabao hayo na ilikianza kipindi cha pili kwa kufanya mabadiliko ya kumtoa Nizar na kumuingiza, Hassan Dilunga.
Yanga ilizidi kuendeleza mashambulizi yake kwenye lango la Polisi na katika dakika ya 56 Coutinho aliifungia timu hiyo bao la tatu kwa njia ya adhabu ndogo ya moja kwa moja kupitia shuti kali alilopiga akiwa usawa wa kibendera cha kona lililomshinda kipa wa Polisi.
Dakika ya 65 Kocha wa Yanga, Hans Van Pluijm, aliwapumzisha Coutinho na Sherman na nafasi zao kuchukuliwa na winga, Mrisho Ngassa na Danny Mrwanda. Kocha wa Polisi, Khamis Sufian, naye aliwatoa Said Bakar na Samir Vicent, huku Abdallah Omary na Steven Emmanuel wakichukua nafasi zao.
Dakika ya 70, Mohammed Seif wa Polisi alishindwa kuifungia bao la kufutia machozi timu yake baada ya kukosa nafasi ya wazi kufuatia shuti alilopiga kudakwa na kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’.
Yanga ilifanikiwa kupata bao la nne dakika ya 80, lililofungwa na Msuva kwa shuti la kiufundi baada ya kupokea pasi safi ya kiungo, Salum Telela, bao hilo limemfanya kujikita kileleni kwenye ufungaji bora wa michuano hiyo akiwa na mabao manne.
Dakika ya 86 Yanga iliwatoa Cannavaro na Telela na nafasi zao kuchukuliwa na beki, Rajab Zahir na kiungo, Said Juma Makapu.
Hadi dakika 90 zinamalizika Yanga iliondoka na ushindi huo mnono na kufikisha jumla ya pointi sita na mabao nane ya kufunga.

Wakati huo huo, Simba leo inatarajia kujua hatima yake ya kuendelea na michuano hiyo pale itakapokuwa na shughuli pevu kuvaana na vinara wa Kundi C JKU, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Amaan saa 2 usiku.

Simba inahitaji matokeo ya ushindi tu ili kujihakikishia kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo. Mtibwa Sugar nayo itaingia dimbani kwenye mchezo dhidi ya Mafunzo kusaka ushindi au sare ya aina yoyote kutinga hatua hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles