24.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 7, 2022

YANGA YAISHUSHA DARAJA LIPULI

MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM 

 TIMU ya Lipuli imeshuka daraja kutoka Ligi Kuu Tanzania Bara hadi Ligi Daraja la Kwanza, baada ya jana kuchapwa bao 1-0 ikiwa nyumbani Uwanja wa Samora, Iringa. 

Bao la ushindi la Yanga lilifungwa na mshambuliaji wa timu hiyo David Molinga dakika ya 38. 

Lipuli imemaliza msimu ikiwa nafasi ya 18, ikiwa na pointi 44 ilizovuna kupitia michezo yake 38. 

Janga lililoikuta Lipuli jana lilizikuta pia Ndanda ya Mtwara na Alliance ya Mwanza, ambazo pia zimeifuata Singida United kushuka daraja moja kwa moja kutoka Ligi Kuu Bara hadi Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao (FDL). 

Ndanda, Lipuli na Alliance zilikuwa zikisubiri hadi dakika ya mwisho kujua hatma yao kama zitasalia au zitakwenda na maji. 

Kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Mbao katika mchezo wa jana kilizamisha jahazi la Ndanda na kuifanya timu hiyo kumaliza nafasi ya 19, ikiwa na pointi 41. 

Licha ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Namungo, Alliance imeangukia Ligi Daraja Kwanza, baada ya kumaliza nafasi ya 17 na pointi  45.

Wakati timu hizo nne zikishuka daraja moja kwa moja, Mbao na Mbeya City zilizomaliza nafasi ya 16 na 15 na sasa zinangojea hatma yao kama zitasalia Ligi Kuu zitakapokwenda kusaka fursa hiyo kwenye michezo ya mtoano(play offs).

Mbao ilikwepa panga la kushuka daraja moja kwa moja, baada ya kuvuna ushindi wa mabao 2-0 mbele ya Ndanda, mchezo uliochezwa Uwanja wa Kirumba, Mwanza.

Ushindi huo uliifanya Mbao kufikisha 45 na kushika nafasi ya 16.Kilichoibeba Mbao ni wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya Alliance imeteremka licha ya kuvuna pointi 45.

Mbao imefunga mabao 33 na kuruhusu wavu wake kutikishwa mara 43, huku Alliance ikifunga mabao 36 na kufungwa mabao 48.

Licha ya kazi kubwa alioifanya kocha Fred Minziro, atalazimika kushinda michezo miwili ya mtoano dhidi ya Ihefu ili kubaki Ligi Kuu.

Mbeya City ilimaliza nafasi ya 15, baada ya kuvuna ushindi wa 3-0 dhidi ya KMC na kumaliza na pointi 45 sawa na Mbao na Alliance.

Kilichoibeba Mbeya City ni uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa, ikipachika mabao 33 na kufungwa mabao 42. Kocha wa timu hiyo, Amri Said ana kibrua kizito cha kusaka ushindi katika michezo miwili ya mtoano dhidi ya Geita Gold.

Ushindi wa mabao 2-1 ilioupata kutoka kwa Ruvu Shooting uliifanya Mtibwa Sugar kunusurika kushuka daraja, baada ya kumaliza nafasi ya 14 na pointi 45.

Mtibwa Sugar imevuna pointi 45 sawa na Mbao, Alliance na Mbeya City.

Kitendo cha kuruhusu mabao machache tofauti na wapinzani wake kimeifanya kusalia katika ligi hiyo kwani imepachika 30 na kuruhusu 34. Yanga imemaliza nafsi ya pili baada ya ushindi wake wa bao 1-0 dhidi ya Lipuli, huku washindani wao wa karibu Azam wakimaliza watatu baada ya sare ya mabao 2-2 na Tanzania Prisons.

Mabingwa wa ligi hiyo, Simba ilimaliza msimu vizuri baada ya kuitungua Polisi Tanzania mabao 2-1, Uwanja wa Ushirika, Moshi.

Coastal Union ilifunga msimu kwa kuchapwa bao 1-0 na JKT Tanzania, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Mwadui iliilaza Kagera Sugar mabao 2-1 Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga wakati Singida United ikiaga ligi hiyo kwa kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Biashara United, mchezo uliochezwa Uwanja wa Liti, Singida.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,859FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles