28.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

Mtuhumiwa wa uhalifu atangaza kugombea urais

 BANGUI, CAR

ALIYEKUWA Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) Francois Bozize ametangaza kuwa atagombea urais katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi Desemba maka huu, licha ya kuwekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa (UN).

Pamoja na vikwazo hivyo vya UN, Bozize pia ametolewa hati ya kukamatwa dhidi yake, ili kumtia nguvuni kwa tuhuma za kutenda jinai dhidi ya binadamu.

Bozize alitangaza uamuzi huo juzi Jumamosi, Julai 25, 2020 katika hotuba aliyotoa mbele ya umati mkubwa wa wafuasi wake katika mkutano wa chama chake cha Kwa na Kwa uliofanyika katika Mji Mkuu wa nchi hiyo, Bangui.

Bozize, mwenye umri wa miaka 73, ambaye ni Jenerali mstaafu na mkuu wa zamani wa jeshi la Jamhuri ya Afrika ya Kati, aling’olewa madarakani mwaka 2013 na muungano wa waasi wa Seleka ambao wanamgambo wake wengi walikuwa ni Waislamu.Hatua hiyo iliitumbukiza nchi hiyo, ambayo idadi kubwa ya watu wake ni Wakristo, kwenye vita vya machafuko makubwa ya ndani yaliyoandamana na jinai za mauaji dhidi ya raia wengi Waislamu.

Katika hotuba yake ambayo ilikosoa utendaji wa rais wa sasa, Faustin-Archange Touadera, Bozize, ambaye aliingia madarakani mwaka 2003 kupitia mapinduzi ya kijeshi na kuiongoza Jamhuri ya Afrika ya Kati kama rais kwa kipindi cha miaka 10 kabla ya kutoroka kuelekea uhamishoni mwaka 2013, alisema nchi hiyo inahitaji mtu mwenye uzoefu na pia inahitaji amani na kuwabainisha hadharani waliofanya uhalifu. 

Japokuwa serikali ya sasa ya Jamhuri ya Afrika ya Kati imetoa waranti wa kumkamata Bozize kwa tuhuma za kutenda jinai dhidi ya binadamu na kuchochea mauaji ya kimbari, lakini haijachukua hatua yoyote ya kujaribu kumtia nguvuni tangu aliporudi nchini humo mwaka jana kutoka uhamishoni.

Bado haijaeleweka kama hati hiyo ya kukamatwa na vikwazo alivyowekewa Bozize na Umoja wa Mataifa vitaathiri ugombeaji wake au la.

Eneo kubwa la ardhi ya nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini ya almasi haliko kwenye udhibiti wa serikali kutokana na mapigano yanayoendelea baina ya makundi ya wanamgambo, ambayo yamewalazimisha watu zaidi ya milioni moja na nusu kuyahama makazi yao.

AFP

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles