26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

YANGA YAENDELEZA MSAKO

MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAMTIMU ya Yanga leo itakuwa na kibarua kigumu cha kusaka pointi tatu ugenini dhidi ya Tanzania Prisons, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Yanga itaingia uwanjani ikiwa na morali ya juu, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Tanzania na  uongozi wa Ligi Kuu katika mchezo wake uliopita uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Miamba hiyo ya Jangwani ilikamata usukani wa ligi hiyo, baada ya kufikisha pointi 35 na kuiteremsha Azam FC iliyokuwa kileleni katika nafasi ya pili na pointi zake 33, huku wapinzani wao wakuu Simba wakishuka nafasi ya tatu na pointi 27.

Tayari Yanga imeshuka dimbani mara 13, ikishinda michezo 11 na kutoka sare mbili.

Prisons kwa upande mwingine wataikaribisha Yanga wakitoka kulazimishwa suluhu na Biashara United Uwanja wa Sokoine.

Katika msimamo wa Ligi Kuu wenye timu 20, Prisons inakamata nafasi ya 19, ikiwa na pointi 10, sawa na Biashara United iliyoko mkiani kutokana na tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Magereza, msimu uliopita ilivuna pointi nne katika michezo miwili iliyokutana na Yanga, ikianza kwa sare ya bao 1-1, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, kabla ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 Uwanja wa Sokoine, katika mchezo wa mzunguko wa pili.

Mara ya mwisho Yanga kuvuna pointi tatu Uwanja wa Sokoine ilikuwa msimu wa 2016/2017.

Rekodi zinaonyesha ilishinda michezo yote miwili dhidi ya Prisons, ikianza kushinda bao 1-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Uwanja wa Sokoine, kabla ya kupata ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo wa mzunguko wa pili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, aliliambia MTANZANIA jana kuwa kikosi chake kimejipanga vema kwa ajili ya kuhakikisha kinaondoka na pointi zote tatu katika mchezo wao wa leo dhidi ya Prisons.

“Tumejiandaa vizuri kwa mchezo huo, niliambiwa msimu uliopita hatukufanikiwa kushinda hapa, nafahamu ugumu wa kucheza ugenini.

“Lakini niseme kwamba hatukuja huku kutalii, vijana wangu wana ari ya kutaka kushinda, wanatambua umuhimu wa pointi tatu, nina amini hawatawaangusha mashabiki wa Yanga.

“Wanapoingia uwanjani fikra zao ni kupata matokeo mazuri mengine  wanayaweka kando, tunawakosa baadhi ya wachezaji kutokana na sababu mbalimbali, lakini atakayepewa nafasi anaonyesha juhudi, naamini tutaendelea kufanya vizuri,” alisema Zahera mwenye uraia wa DRC na Ufaransa.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Prisons, Abdallah Mohamed, alisema licha ya kikosi chake kukamata nafasi za chini kwenye msimamo wa ligi hiyo,  atahakikisha hawapotezi mchezo huo ili kulinda rekodi yake ya kutofungwa na Yanga msimu uliopita.

“Licha ya kuwa katika nafasi mbaya, lakini hatutakuwa wanyonge, tumejipanga kikamilifu kwa ajili ya kuhakikisha tunashinda ili kubakiza pointi tatu nyumbani, lakini kubwa ni kuondoka katika nafasi za chini.

“Tumekuwa na muda wa kutosha wa kujiandaa, tunajua wapinzani wetu wapo katika ubora mkubwa kwa sasa kwani hawajapoteza mchezo, tumejiandaa kuwavurugia,” alisema kocha huyo bora wa msimu uliopita.

Katika michezo mingine, Mwadui FC watakuwa nyumbani Uwanja wa Mwadui Complex kuumana na KMC.

Mwadui inashika nafasi ya 15, ikiwa na pointi 13, baada ya kushuka dimbani mara 14, ikishinda tatu, sare nne na kupoteza saba, wakati KMC inakamata nafasi ya 11, ikiwa na pointi 16, kupitia  michezo 13, ikishinda mitatu, sare saba na kupoteza mitatu.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,277FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles