23.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga wafuata nyayo za Simba

6Na ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM

BAADA ya kusikia watani zao wa jadi, timu ya Simba wameamua kumwaga fedha kwa wachezaji wao kama watashinda katika mechi yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara, itakayochezwa Oktoba Mosi mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga nao wameamua kujibu mapigo kwa kuamua kutenga fungu maalumu kwa ajili ya wachezaji wake na benchi la ufundi, iwapo watashinda mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa timu hizo.

Yanga wana rekodi nzuri ya kuifunga Simba katika mechi wanazokutana katika miaka ya hivi karibuni, wamefikia maamuzi hayo kwa lengo la kuongeza motisha kwa wachezaji na benchi la ufundi.

Hivi karibuni vigogo wa Simba wamekuwa na utaratibu wa kuwapa fedha wachezaji wao kila timu inaposhinda, lakini tayari kuna donge nono limetengwa kuelekea mechi hiyo iwapo watapata ushindi dhidi ya Yanga.

Habari ambazo MTANZANIA Jumamosi limezipata kutoka ndani ya uongozi wa Yanga zinasema kumekuwa na vikao vya siri kwa baadhi ya viongozi wa timu hiyo na wale wa matawi ambavyo vina lengo la kuweka mikakati ya ushindi katika mchezo huo dhidi ya Simba.

Habari hizo zinasema kuwa moja ya mikakati iliyowekwa ni kuona timu inapata mahitaji yote muhimu kulingana na benchi la ufundi, ikiwemo kuweka kambi mahali pazuri na penye utulivu.

Inaelezwa kuwa hadi sasa suala la kambi limekamilika kwa asilimia 100 na baada ya mchezo wao na Stand United utakaochezwa kesho, timu itapanda ndege na kwenda moja kwa moja Zanzibar kujichimbia, huku mikakati mingine ikiendelea.

“Tumeanza kukutana na viongozi wa matawi tangu Jumatano na kugawa majukumu ya ndani na nje ya uwanja, ikiwemo uhamasishaji wa mashabiki kujitokeza mapema na kuhakikisha wanajaza uwanja,” kilisema chanzo hicho.

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit, alipotafutwa kutaka kujua juu ya habari hizo, alisema kwa hivi sasa ni mapema kuuzungumzia mchezo wao na Simba, ingawa hayo yaliyozungumzwa yanaweza kuwepo.

“Kwanza tuuangalie mchezo wetu na Stand United, kwani wa Simba upo mbali sana, hivyo siwezi kuanza kuuzungumzia hivi sasa, ila ifahamike kuwa kila mechi kwetu tunahitaji pointi tatu, si vinginevyo na hayo yote yanayozungumzwa yanaweza kuwepo, kwani hayana ubaya katika kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri,” alisema.

Katika msimu uliopita, Yanga iliifunga Simba mabao 2-0 katika mzunguko wa kwanza na pia katika mzunguko wa pili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles