*Yatishia kujitoa makundi Kombe la Shirikisho kisa ukata
NA ADAM MKWEPU, DA R ES SALAAM
WAKATI mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, timu ya Yanga wanaojulikana kama Wakimataifa wakila bata nchini Uturuki katika kambi ya maandalizi ya mechi za makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, wapinzani wao timu ya Medeama ya Ghana wapo mbioni kujitoa kwenye michuano hiyo kutokana na kukumbwa na ukata.
Yanga ilianza kambi Jumapili iliyopita katika Hoteli ya Rui mjini Antalya, Uturuki kwa ajili ya maandalizi ya mchezo dhidi ya Mo Bejaia ya Algeria ambao unatarajiwa kuchezwa usiku Jumapili hii.
Mabingwa hao mara 26 wa Ligi Kuu Tanzania Bara na wawakilishi pekee wa Tanzania, wanatarajia kucheza dhidi ya Medeama Julai 15 mwaka huu, katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, baada ya kumaliza mchezo dhidi ya TP Mazembe utakaochezwa Juni 28 mwaka huu.
Hatua hiyo ya kujitoa imekuja wakati Medeama ikikabiliwa na mchezo wa ugenini dhidi ya TP Mazembe, unaotarajiwa kuchezwa Juni 19 mwaka huu.
Taarifa kutoka nchini Ghana zinadai kuwa, Meneja Utawala na Mawasiliano wa klabu hiyo, Benjamin Kessie, alisema timu yao haina fedha hivyo watashindwa hata kujigharamia kuelekea nchini Kongo kwa ajili ya mchezo wao wa kwanza dhidi ya TP Mazembe.
Shirikisho la soka Afrika ‘CAF’ bado halijatoa fedha kwa klabu zilizofuzu hatua za makundi licha ya klabu hiyo kufanya kila jitihada kupata fedha hizo ili kwenda Kongo kucheza na Mazembe, juhudi hizo bado hazijatoa majibu yoyote.
“Klabu ipo katika hali mbaya kifedha na inahitaji msaada, tunajipanga kujitoa katika mashindano kama hatutapata msaada wowote,” alisema.
Yanga wenyewe hadi jana jioni walikua hawana taarifa yoyote juu ya wapinzani wao kujitoa katika michuano hiyo.